31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yatoa neno kuhojiwa kina Kinana, Makamba

ANDREW MSECHU –dar es salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaendelea kushughulikia wito kwa makatibu wakuu wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba, na Waziri wa Mambo ya Nje mstaafu, Bernard Membe kwenye Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho.

Akizungumzia wito huo juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema suala hilo ni la ndani na linashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, hivyo litakapokamilika umma utafahamishwa.

Katika mahojiano yake na MTANZANIA, alipoulizwa kuhusu iwapo wameshawaandikia barua wahusika kuwaita, Polepole alisema suala lolote linalohusu usalama na maadili, si la umma bali ni la ndani ya chama na kwamba umma utajulishwa matokeo ya vikao.

“Na kwa utaratibu tu, jambo la usalama na maadili litafanyiwa kazi kwenye ngazi ya kamati hiyo, kisha litakwenda kwenye Kamati Kuu na baadaye kwenye Halmashauri Kuu, kisha baada ya hapo ndipo umma utakapojuliswha,” alisema Polepole.

Alipoulizwa kuhusu ni lini chama hicho kinatarajia kukaa vikao vya Kamati ya Usalama na Maadili kisha Kamati Kuu na Halamashauri Kuu ikiwamo suala la kuhojiwa kwa viongozi hao wastaafu, Polepole alisema vikao hivyo vitakaa wakati wowote.

“Kwa sasa chama kina ratiba ndefu ya uchaguzi ambayo ndilo jambo la kipaumbele kwetu kwa sasa hivi. Kwa hiyo mambo mengine yatakuwa sehemu ya vikao hivyo kwa sababu ratiba yetu ya vikao, ukiacha vile vya kawaida kutakuwa na vikao vya ziada na kila vitakavyokuwa vinakuja tutawajulisha,” alisema Polepole.

Kuhusu suala la muda, Polepole alisema mambo yote yatafanyika chini ya utaratibu wa chama na watajadili suala hilo pale watakapoona inafaa.

“Chama chetu kina utaratibu tu, tuna vikao kwa mujibu wa kalenda na kuna vikao vya ziada ya kalenda vinaitwa vikao maalumu na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, yapo mambo mengine yanaendelea kama kawaida, lakini sisi kipaumbele chetu na vikao vitakavyokuwa vinaketi ni kwa ajili ya chama.

“Kwa hiyo mambo mengine yote ikiwemo hilo unaloulizia yanaendelea kwenye mchakato, kwa hiyo kikao kitakachokuja kiwe maalumu au cha kawaida kama hilo litakuwepo mtajulishwa,” alisema Polepole.

Alisisistiza kuwa suala hilo ni la ndani ya chama kwa sasa na si la umma, kwa hiyo suala la kujua iwapo barua zimeshaenda au hazijaenda hilo ni suala la ndani na la kiutendaji zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles