26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

CCM yatathimini Uchaguzi Mkuu 2020

*Yatamba kushinda kwa zaidi ya asilimia 90, ikiwa uchaguzi utafanyika wakati wowote

*Yaeleza idadi ya wanachama wake yafikia milioni 15

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina uhakika wa kuibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 90 iwapo uchaguzi utatangazwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Kimesema kwa mujibu wa tathimini waliyofanya, hadi sasa wana wanachama zaidi ya milioni 15, ambao ndio msingi wa ushindi kwenye uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,  Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema chama hicho tawala kina uhakika wa ushindi mkubwa katika uchaguzi kuanzia wa mwaka huu wa Serilali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Alisema walioandikishwa katika vitabu, wanaamini wote watakipigia kura chama hicho kwenye chaguzi zote zijazo.

“Tayari tuna wanachama wanaofikia milioni 15, na tunapoangalia idadi ya wapigakura katika chaguzi zijazo wanakadiriwa kufikia milioni 21, kwa hiyo kwa idadi hiyo tunawezaa kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 71,” alisema.

Polepole alikuwa akizungumzia mikakati ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Oktoba na Uchaguzi Mkuu utakaohusisha chaguzi za madiwani, wabunge na Rais Oktoba mwakani.

Alisema iwapo watahusisha kampeni, kwa idadi hiyo ya wanachama, wana uwezo wa kuongeza idadi ya wapigakura kufikia milioni 20, hivyo kuwa na uhakika wa kushinda kwa asilimia 90, kwa kuzingatia nafasi waliyonayo kwa sasa.

Akitoa ufafanuzi, Polepole alisema kwa tathmini yao ya kichama, hadi sasa wana wanachama hai zaidi ya milioni 15 walioandikishwa katika vitabu vyao, ambao tayari wako katika utaratibu wa kuwaandikisha upya kupitia mfumo wa kadi za kielektroniki, ili kuweka kumbukumbu sawa.

 “Tunapoangalia kwa sasa, iwapo tutaamua kwamba angalau kila wanachama wetu watatu watafute na kushawishi mwanachama mmoja mpya, hilo likifanyika tu, tayari tutakuwa na zaidi ya wanachama milioni 20, kwa hiyo tutakuwa na uhakika wa asilimia 90 ya kura kutoka kwa wanachama wetu tu.

“Na tukianza kampeni, kwa watu wetu tuliowapanga, kwa kutumia wasanii tulionao, tukipiga ‘hiyena hiyena’ hapa na kuzunguka na bendi ya TOT Tanzania nzima, wale wenye nongwa watajua sisi ni akina nani,” alisema.

Alisema safari hii vyama vidogo vidogo vyenye mazoea ya kususia uchaguzi vinatakiwa vijipange ipasavyo kushindana na chama chake, kwa kuwa tayari wameshauona ushindi wa kishindo.

MA-DED KATIKA CHAGUZI

Polepole alisema CCM haiwezi kuingilia mahakama katika suala la matumizi ya wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kwenye usimamizi wa uchaguzi, lakini ana uhakika suala hilo litapata suluhu.

Alisema chama chake kinatii mamlaka kwa kuwa suala hilo liko mahakamani, hivyo wameamua kukaa kimya kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Alikuwa akizungumzia kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya kuzuia wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kusimamia uchaguzi, kwa kuwa wengi walionekana kuwa makada wa CCM, uamuzi ambao Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliukatia rufaa.

“Sisi kama chama tumeamua tusizungumzie suala hili, tunasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa utolewe ndipo tutakapozungumza,” alisema.

Hata hivyo, Polepole alieleza kuwa hoja ya wakurugenzi kutotumika kusimamia uchaguzi iliibuka kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ambapo mamlaka zilikubali na kuzuia wasisimamie, lakini suala hilo lilikuwa na gharama kubwa.

Alisema baada ya kuajiri mawakala wa kusimamia uchaguzi, lilitokea tatizo la fedha za malipo kuchelewa, hivyo wakaamua kwenda nyumbani na maboksi ya kura na kusababisha uchaguzi huo kuvurugika katika maeneo mengi.

“Kwa hiyo katika hili tayari tulishajifunza na hatuwezi kukubali kurudia makosa. Tukumbuke kuwa baada ya kuteuliwa, hata kama walikuwa na itikadi, wakurugenzi hawa wanakula kiapo kwa kutumia Katiba na kwa dini zao. Wanaacha itikadi zao.

“Uchaguzi unasimamiwa kwa sheria na hawa ni watumishi wa umma waliokula kiapo, ambao wanawajibika kwa umma, hivyo hawawezi kupotea na masanduku ya kura au kuharibu uchaguzi,” alisema.

Alisema anaamini kwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishawasilisha nia ya kukata rufaa na kuwasilisha hati ya dharura kuomba maamuzi ya Mahakama Kuu kutotekelezwa hadi rufaa hiyo itakapotolewa hukumu, kwa sasa mambo mengine yataendelea kama kawaida hadi uamuzi wa rufaa utakapotolewa.

Polepole alisema kwa sasa wanaiomba Mahakama ya Rufaa iharakishe ili suala hilo lifikie tamati Watanzania waendelee kupata haki yao katika kusimamia na kutoa maamuzi yanayohusu maisha yao.

SUALA LA KOROSHO

Akizungumzia suala la korosho, Polepole alisema biashara yake ni ya kimataifa ambayo imekuwa sehemu ya mapambano makali ya kiuchumi, kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa kwa mataifa ya China na Marekani.

Alisema japokuwa kumekuwa na mkwamo, lakini CCM wanajivunia kwa kuwa lengo lao la kulinda heshima ya Serikali na wakulima wa Tanzania limefikiwa, hivyo kwa sasa suala linalofuata ni kutafuta masoko.

Alieleza kuwa kwa kuwa nchi kama Tanzania sasa imejipambanua kujisimamia na kujitegemea, wapo watu wasiofurahia hatua hiyo kutokana na mazingira ya mapambano ya kiuchumi, hivyo msimamo wa Serikali hautabadilika.

“Rais John Magufuli alitoa uamuzi wa kihistoria alipoamua kuingilia kati suala la korosho kwa ajili ya kulinda wanyonge na wakulima.

“Uamuzi wa kununua korosho zote kwa kutumia taasisi za fedha za ndani ulikuwa kwa ajili ya kuweka heshima ya Serikali.

“Kwa hiyo, kinachofuata tutatafuta mahala pa kuziuza. Na wakituchezea tutazila wenyewe hizo korosho. Tunaweza kuweka utaratibu wa kuzigawa kwa taasisi zetu za ndani kuna shule na nyinginezo, lakini kwa sasa bado tunaweka utaratibu wa kupata soko,” alisema.

VIKAO VYA CHAMA

Polepole alisema tayari vikao vya chama vilianza katika ngazi ya Sekretarieti inayoogozwa na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally, ambacho kitafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu kesho itakayoongozwa na Mwenyekiti wa chama, Rais John Magufuli na hatimaye mkutano wa Halmashauri Kuu.

Alisema wakati kikao cha kamati Kuu kikiendelea, kwa siku nzima ya kesho wajumbe wa Halmashauri Kuu watapata fursa ya kutembelea miradi muhimu inayoendelea nchini na kuona hatua mbalimbali zilizofikiwa.

Alisema wajumbe hao wa Halmashauri Kuu wanaofikia 167 watatembelea mradi wa Daraja la Selander, Reli ya Kisasa katika eneo la Gerezani na kiwanda cha kutengeneza zege nzito ya ujenzi wa madaraja ya reli ya kisasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles