25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ccm yatambua kusafisha upepo

 

-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ametamba kuisambaratisha ngome ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.

Katika uchaguzi mdogo uliofanyika juzi, chama hicho kilishinda ubunge Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma.

Pia kilishinda  udiwani katika kata 36, huku kikiwa na madiwani 41 waliopita bila kupingwa baada ya wapinzani kuenguliwa katika hatua za awali.

Kati ya kata hizo, sita ni za Monduli  huku moja mgombea wake akipita bila kupingwa baada ya mpinzani wake kuenguliwa katika hatua za mwanzo.

Akizungumza na waandishi wa habari,  katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu CCM Lumumba, Dar es Salaam jana, DK Bashiru alisema kuna kila dalili kwamba chama hicho kinaanza kuwa na mvuto.

“Monduli ilipitiwa upepo wa mapepo na CCM ilipoteza kila kitu, sasa kuna upepo mwanana.

“Hewa safi imetanda Monduli inayosafisha uongozi ndani ya chama chetu na kuwapa imani wananchi. Usafi wa siasa, uongozi na mshikamano.

“Mbunge Kalanga (Julius Kalanga, aliyekuwa Mbunge wa Monduli kupitia Chadema, sasa kahamia CCM) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli (Isaack Joseph) wote wamerejea CCM.

“Na wakati Kalanga anarejea tulifanya usiku kwa sababu mashambulio yake lazima yawe ya usiku, watu walisema hizi ni dalili za woga lakini vita haina mchana wala usiku.

“Jemedari ndiyo anaamua shambulio lifanywe wakati gani,” alisema.

Katibu Mkuu huyo wa CCM  pia alivitaka vyama vya upinzani vijipange kwa kile alichodai kuwa CCM ya leo si ya jana.

“Waache kutumia porojo na kukaa kwenye mitandao bila kwenda ‘site’ kuona kinachoendelea, wengine wanazungumza mambo ya Buyungu hawajawahi kwenda. Nilikuwapo Monduli sikuona maandamano wala malalamiko.

“Watu wanataka maji si porojo, wanataka barabara, elimu bora, afya, umeme, masoko na hayo tukiyafanya, tukipata mia kwa mia wanalalamika,” alisema.

Alisema ziko kata ambazo tangu uanze mfumo wa vyama vingi nchini zilikuwa hazijawahi kushikwa na CCM kama vile Kata za Lyoma (Kwimba – Mwanza) na Baray (Karatu – Arusha), lakini sasa zimenyakuliwa na chama hicho tawala.

“Kata ya Lyoma hatukuwahi kushinda tangu enzi za Mzee Mapalala ilikuwa ni CUF tu. Kata ya Baray Karatu hatujawahi kushika uongozi kwa miaka 25 na yenyewe ilipitiwa na upepo wa mapepo lakini hivi sasa kuna upepo mwanana unavuma, tumeshinda,” alisema Dk. Bashiru.

BUYUNGU

Dk. Bashiru alisema licha ya kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 58 Buyungu lakini CCM ilishinda kwa taabu.

“Buyungu tulipata taabu kidogo kwa sababu mgombea aliyekuwapo alikuwa anapendwa sana na wananchi, alikuwa ni mwalimu, wanampenda tu na wamemtumia wale watu,” alisema.

Alisema wakati wa kampeni kila kata ilipangiwa mbunge maalumu wa CCM na wote walifanya kazi nzuri kwa kufanya mikutano zaidi ya 25, kuzungumza na viongozi wa dini zaidi ya 12, walimu wa sekondari na shule za msingi, bodaboda na wafanyabiashara wadogo wadogo.

“Wote walituelewa na matokeo yake tumeyaona. Ninashawishika kusema tumeanza kufanya kazi inayowapa matumaini walio wengi hasa wanyonge, kila tulikopita tumezungumza lugha inayoeleweka kwa maisha ya wanyonge, tunasikiliza kero na maeneo mengine tunatatua kero papo kwa papo.

“Wanaokwenda kwa kasi ndogo tunawasukuma na wengine wakiteleza tunawaweka pembeni  safari iendelee,” alisema Dk. Bashiru.

KURA YA MAONI

Katibu Mkuu huyo wa CCM aalisema kuwa kura ya maoni si njia pekee ya kupata mgombea lakini chama hicho kinafuata sheria za nchi.

“Ziko taratibu zetu hazijaandikwa popote lakini zinapotufaa zinatumika, kuna mazingira ambayo yanapita kwenye vikao.

“Songea tulifanya kura ya maoni mshindi wa kwanza, wa pili hawakuteuliwa, hiyo ndiyo CCM.

“Mwenyekiti wa Monduli alikuwa ni diwani alisema anarudi CCM na anakuwa mwanachama wa kawaida hatagombea,  je, utamlazimisha?

“Tunapiga hesabu tunaangalia uamuzi utakaotuhakikishia ushindi na umoja kwa sababu kwetu umoja ni jambo muhimu sana,” alisema.

Hata hivyo alisema kuna haja ya chama hicho kujiimarisha na kuangalia mifumo ya ndani na kuihoji.

“Morali wa wapigakura kwangu mimi unaniumiza, 2015 mgombea wa urais pamoja na juhudi na sifa zake lakini matatizo ya makundi ndani ya chama tulipata asilimia 58 ya ushindi wake, haijawahi kutokea katika chama hapo morali ilikuwa imeshuka.

“Leo tunapandisha morali kwa kushinda Buyungu, kata 36 na kupita bila kupingwa kata 41, hakuna anayebeza.

“Sisi ndani ya CCM hatukuwahi kuwa na idadi ndogo ya wapigakura tangu nchi ipate Uhuru. Mwaka 2010 zaidi ya asilimia 50 waliokuwa wamejiandikisha hawakupiga kura.

“Jambo hilo sisi linatuumiza sana kwa nini wananchi wakati wa kwenda kutoa sauti yao ya uongozi wamekaa kando na mpaka leo si jambo jema.

“Tulikuwa tunapata wapigakura kati ya asilimia 70 na kwenda juu, 2010 kuna jambo liliwakera Watanzania na mojawapo ni kugeuza kura kuwa biashara,” alisema.

Alisema pia nusu ya ilani ya uchaguzi ya CCM imetekelezwa na kwamba kuna shabaha kubwa za kupambana na umaskini hasa wa wanyonge, kutengeneza nafasi nyingi za ajira, kupambana na rushwa na ufisadi na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama   Taifa liendelee kuwa na amani.

Alisema kadiri  misingi ya Azimio la Arusha na Mapinduzi ya Zanzibar inavyoimarishwa, chama hicho kinazidi kuwa karibu na wavuja jasho, kuaminiwa na kuungwa mkono.

“Tunaridhika na namna tunavyoaminiwa, tunachokifanya ndani ya CCM si kipya, kimefanywa na waasisi wa chama chetu. Ndiyo wameweka misingi ya utaifa wetu, utu, haki, na usawa, misingi ya kutetea uhuru wa taifa letu,” alisema.

Alisema pia kuna haja ya kudadisi na kuhoji ni aina gani ya mfumo muafaka wa vyama vya siasa na aina ya

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa mkoani Dodoma jana.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa mkoani Dodoma jana.

demokrasia inayohitajika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles