31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yahimiza siasa za amani, mshikamano

Mwandishi Wetu – Kagera

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetimiza miaka 43 ya kuzaliwa, huku bado kikiendelea kuwa imara na kuwataka Watanzania kuendelea kukiamini katika kuliongoza taifa.

Pamoja na hayo, chama hicho tawala kimehimiza ufanyaji wa siasa zinazohimiza umoja, amani na mshikamano kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama.

Akizungumza jana mjini Bukoba mkoani Kagera, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu UVCCM Bara, Galila Wabanh’u, alisema miaka 43 ya kuzaliwa kwa chama hicho ni sehemu ya tafakari kwa taifa na wana CCM kwa ujumla, kwa kuhakikisha wanaimarisha umoja na mshikamano kwa nchi.

“CCM inatimiza miaka 43 ikiendelea kuaminiwa na umma kutoa uongozi wa nchi yetu, sababu kubwa ikiwa tunahimiza umoja na amani kwa nchi yetu.

“Tunahimiza mijadala kwa hoja, kusikilizana na kuvumiliana. Kamwe hatukubali tofauti zetu za kiitikadi kuwa chanzo cha kutoa lugha zinazojenga chuki, migawanyiko na zenye viashiria vya vurugu,” alisema Galila.

Aliwaasa wanachama wa CCM Mkoa wa Kagera, hususani Jimbo la Bukoba Mjini, kuepuka siasa za makundi, mizengwe na fitina ili kuweza kulirejesha jimbo hilo mikononi mwa CCM.

“Siasa za makundi, mizengwe, rushwa, fitna na majungu hufanywa na watu wasiojiamini na wenye uwezo mdogo kiuongozi. Waepukeni wanaozipa nafasi ili kulinda umoja ndani ya chama chetu,” alisema Galila.

Katika hatua nyingine, aliwataka wanachama wa CCM wenye nia ya kugombea udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu kupitia CCM waheshimu taratibu za chama kwani wapo wanaoamini kwa kuwaweka mfukoni viongozi wachache majina yao yatarudi.

Alisema ni lazima watambue kwamba kufanya hivyo ni kosa kwani majina hurudishwa na vikao vya uteuzi vya chama na si mtu wala kikundi cha watu.

“Wenye jukumu la kuchuja na kurejesha majina ya wagombea ndani ya CCM kwa kuzingatia taratibu na kanuni ni vikao sio mtu au kikundi cha watu,” alisema Galila.

Aliwataka wanachama wa CCM watakaoomba kuteuliwa na chama kuwa wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kujua uongozi ni utumishi, ikitokea kwa sababu za kikanuni na utaratibu hawakuteuliwa wasihame chama au kukihujumu kisishinde, badala yake watulie na kuwaunga mkono wale walioteuliwa.

“Ikiwa haki ilitendeka katika uteuzi wa wagombea, huna sababu ya kukihama chama, kususa au kukihujumu chama,” alisema Galila.

Katika hatua nyingine, aliikumbusha Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kagera kuendelea kuihamasisha jamii kuhusu suala zima la lishe kwa watoto ili kujenga taifa lenye afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles