22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

CCM yahamishia nguvu Zanzibar Uchaguzi 2020

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa sasa kinahamishia nguvu zake visiwani Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Wakati CCM ikitamba na hilo, Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amenukuliwa hivi karibuni akiwataka wanachama wa chama hicho wajiandae kwa ushindi wa urais, wabunge, wawakilishi na madiwani katika Uchaguzi Mkuu mwakani.

Maalim Seif alisema kuwa ACT Wazalendo haitaacha nafasi yoyote ya uongozi kwani mikakati iliyotumika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu ni funzo na katu hakitaacha wala kususa nafasi yoyote kuelekea mwaka 2020.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ambaye ameanza ziara ya siku 10 visiwani Zanzibar, alisema kuwa ni lazima mikakati na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu visiwani hapa yaanze kwa wana CCM kuandaa mikakati ya ushindi.

“Awali ya yote nawashukuru kwa kazi nzuri na kubwa ambayo mmeendelea kuifanya katika kuhakikisha kuwa chama chenu kinaendelea kuwa imara, hivyo nami niseme tu kwamba wembe ni uleule.

“Hivyo nina raha kusema kwamba tumewapiga mapema wapinzani wetu kwenye uchaguzi wa juzi kule Bara na sasa nguvu zote tunazielekeza Zanzibar kwani kazi yetu ni ileile,” alisema Dk. Bashiru.

Akizungumzia lengo la ziara yake visiwani Zanzibar, alisema ni kukiimarisha chama hicho na kuongeza kuwa ataitumia kushauriana na wanachama kuangalia namna bora zaidi ya kujiimarisha.

 “Tunashukuru kwamba kwa sasa tuna raha kule bara kwani tumewapiga mapema na sasa kituo kinachofuata ni Serikali ya Zanzibar kwani nina uhakika kwamba tutahamishia ushindi huo huku ili tuwapige mapema.

 “Hivyo nitazungumza na wanachama wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kujiimarisha,” alisema Dk. Bashiru.

Akizungumza katika mkutano wa ndani na wazee wastaafu wa Zanzibar kwenye ziara yake kisiwani Unguja, Dk. Bashiru alieleza msimamo wa CCM kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kutaka kutotumika kamati za nje ya CCM.

Dk. Bashiru alisema akijibu baadhi ya hoja za wazee hao ikiwamo kutaka kamati halali zinazotambulika katika uchaguzi ambazo huwa zikisahaulika na kuundwa kamati nyingine nyingi nje jambo ambalo hukidhohofisha chama hicho.

“Niwaeleze hili wazi wazee wetu, Chama Cha Mapinduzi, kuanzia uchaguzi ujao wa mwaka 2020 hatutakuwa na kamati za uchaguzi nje ya kamati zilizotajwa kikatiba, CCM ina kamati za uongozi na za uchaguzi kuanzia ngazi za mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa na  katika ngazi ya taifa ipo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema kazi zote za kuratibu masuala ya uchaguzi zitafanywa na viongozi waliotajwa kikatiba, kama ni kuchangisha michango, itachangishwa na viongozi wanaotambulika na sio kamati zinazoundwa nje ya Katiba ya CCM. 

“Mfumo wa Katiba ndio utakaofuatwa katika shughuli zote za chama na si vinginevyo ambapo baadhi ya kamati zilikuwa zikiundwa kwa kujuana na kuwaacha wajumbe wanaotambulika na wanachama na waliochaguliwa na wanachama,” alisema Dk. Bashiru.

WABUNGE, WAWAKILISHI

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru alisisitiza msimamo wa CCM kuendelea kuwafuatilia wabunge na wawakilishi ambao muda wote hutumia kwa kuwahudumia viongozi wa chama watakaowapigia kura za maoni mwaka 2020 badala ya kufanya kazi za kuwahudumia wananchi na kuimarisha chama.

“Kuna wabunge na wawakilishi kutwa kucha huwahudumia wajumbe wa mikutano mikuu ya majimbo, badala ya kuwahudumia wananchi, kuna wabunge mipango yao ni kuwanunulia wajumbe pikipiki na baiskeli,” alisema Dk. Bashiru.

MAALIM SEIF NA 2020

Novemba 21, mwaka huu, Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo, Maalim Seif, alisema kuwa watapita katika kila kata, majimbo na wilaya ili kuandaa sera bora ambazo ni sehemu ya mkakati wa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kongamano maalumu la kina mama wa chama hicho lililofanyika Vuga.

Alisema baadhi ya wajumbe wa chama hicho watapita kila kata kukusanya maoni ya wananchi kwa lengo la kuhakikisha wanatengeneza sera bora zitakazoweza kukiuza chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema ili chama kiwe na ilani bora na yenye kuwagusa wananchi, ipo haja ya kuwashirikisha wananchi wenyewe kutoa maoni yao.

“Lengo kuu la kukusanya maoni ya wananchi ni kutaka kujua kwa undani zaidi yanayowakereketa wananchi, hatimaye yawekwe kwenye ajenda zao ambazo watakwenda kuziunganisha katika ilani ya uchaguzi  ya chama hicho,” alisema Maalim Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles