Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaomba Watanzania waendelee kukiamini kwa kuwa kimeweka mikakati kuhakikisha wanapata wagombea bora wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Ahadi hiyo imetolewa leo Julai 8,2024 na Katibu Mwenezi CCM Taifa, Amos Makalla, wakati wa mkutano wa hadhara katika Jimbo la Segerea uliofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Liwiti, Dar es Salaam.
Amesema kabla ya uteuzi wa wagombea watakaa na wakuu wa wilaya, wenyeviti wa wilaya na uongozi wa mkoa kuweka mikakati ya kuchagua watu walio safi.
“Muendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi, ahadi yetu ni kuwaletea wagombea safi, wananchi mnajua changamoto katika mitaa yenu, mnawajua wenyeviti wa mitaa mlionao sasa kwahiyo, tunajua mtatuadhibu tutakapowaletea wagombea wenye kashfa, ambao kila tatizo wapo.
“Tunawahakikishia tumeshaongea na viongozi ngazi ya mkoa na wilaya wawaletee wagombea wasio na makandokando, ambao watafanya kazi za kuwaletea maendeleo.
“Ushindi wowote wa uchaguzi ni namba, hatutawaletea watu ambao siku ya kwanza tunashindwa uchaguzi au miguno inaanza,” amesema Makalla.
Makalla pia amewataka wanachama wa chama hicho kuhamasishana kuhakikisha watu wanajitokeza na kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kupiga kura ili chama kipate ushindi wa kishindo.
“Mwana – CCM lazima utafute mashabiki wanaokipenda Chama Cha Mapinduzi ili kuongeza hamasa na nguvu ya kukisaidia chama chetu kupata ushindi wa kishindo, ombi langu tuendelee kukiamini chama kuna mambo mengi yamefanyika ya Ilani.
“Natambua zipo changamoto lakini kwa mazuri yaliyofanyika ni wazi tuna kila sababu ya kuwashawishi mtuazime imani hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, CCM kipewe nafasi ya kushinda mitaa yote katika nchi na mkoa wote wa Dar es Salaam,” amesema.
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, licha ya kuishukuru serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, amesema bado kuna changamoto za miundombinu na kuiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2).
Aidha amesema Barabara ya Kinyerezi – Bonyokwa ambayo ujenzi wake ulizinduliwa Februari mwaka huu, mpaka sasa haijaanza kujengwa na kuiomba Serikali kuharakisha ujenzi huo.
Katika mkutano huo Makalla pia aliwaelekeza viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali kujibu kero zilizoibuliwa na wananchi ambapo Meneja wa Tarura Ilala, John Magori, amesema mradi wa DMDP wako katika hatua ya kumpata mkandarasi.
Kuhusu kero ya maji Makalla amewahakikishia wananchi kuwa changamoto hiyo itapungua baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji katika eneo la Bangulo lenye ujazo wa lita milioni tisa.