NA MWANDISHI WETU, DODOMA
KAMATI Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake Philip Mangula, imeanza vikao vyake mjini Dodoma kupitia taarifa za utekelezaji wa adhabu kwa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais mwaka 2015 kabla ya wakati.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kiliiambia MTANZANIA kuwa kikao hicho kilianza jana saa 6 mchana, kuanza kupata taarifa za kamati za maadili za mikoa.
Hatua hiyo inatokana na agizo la Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, alilolitoa Februari 8, mwaka huu kwa kuzitaka ofisi zote za ngazi ya mikoa na wilaya kufungua mafaili hayo ili kupitia mienendo ya wagombea walioanza kampeni za uchaguzi wa kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati.
Makada hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
“Leo (jana) tangu saa 6 mchana Kamati Ndogo ya Maadili ilikuwa na vikao mfululizo, na kazi kubwa walikuwa wanapitia mafaili ya wagombea waliotangaza nia ya kuwania urais mwaka 2015.
“Walichokuwa wanakifanya ni taarifa ya utekelezaji wa adhabu hiyo kwa kila mgombea pamoja na kufuatilia mienendo yao… ila kinachoonekana kuna baadhi ya makada huenda adhabu zao zikaongezwa na hata kupoteza sifa za kuwania nafasi hiyo.
“Unajua tangu walipopewa adhabu, baadhi yao wamekuwa wakikiuka na hata kuendelea na mikakati ya kampeni kwa kukusanya watu wao kupanga nini cha kufanya kuelekea mwaka 2015, pia wengine walitumia Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani kuandaa futari ambazo zilikuwa na harufu ya kampeni,” kilisema chanzo hicho kilichopo Makao Makuu ya CCM Dodoma.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho cha Kamati Ndogo ya Maadili na Nidhamu, zinaeleza kuwa katika kipindi cha miezi kadhaa, timu za maofisa usalama wa chama zilisambazwa mikoa yote na kukusanya taarifa za makada hao.
Kikao hicho kimefanyika kabla ya kuanza kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC), kilichoitishwa kwa dharura mjini hapa leo chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
Hatua hiyo ya kuitishwa kikao hicho imekuja baada ya kuwapo kile kinachodaiwa ni shinikizo kutoka kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kumtaka Rais Kikwete aliahirishe Bunge la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini hapa.
Hatua ya Rais Kikwete kuitisha CC inatokana na uamuzi wa kamati hiyo, iliyoketi Julai 16, mwaka huu ambapo ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais.
Kutokana na hali hiyo, CC iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao sita kama wanatekeleza ama la.
Hatua hiyo ya CCM kupitia mienendo ya makada hao waliopewa onyo Februari mwaka huu inawafanya kukalia kuti kavu, kwani ikiwa watabainika kuvunja utaratibu wa chama wanaweza kupoteza sifa za kuwania urais mwakani.
Julai 17, mwaka huu Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili itabaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa, watapoteza sifa.
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara ya 6 (7)(i).
Nape alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea, ni muhimu wakazingatia Katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo,” alisema Nape.
Alisema kama itabainika makada hao hawakutekeleza masharti ya adhabu zao kama zilivyotolewa na CC, kuna hatari ya kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
“Kila mmoja anafuatiliwa mwenendo wake, kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo.
“Kama watakuwa hawajatekeleza adhabu zao, kamati itapeleka mapendekezo CC ili waweze kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na taratibu za chama,” alisema Nape.
Alisema ni muhimu kwa wanachama wote kukumbuka chama ni pamoja na Katiba, kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga jambo ambalo halivumiliki.
Kwamba nia ya CCM ni kusimamia na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa katika kuelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Kamati Kuu, zinasema aliyetoa hoja kuendelea kufuatiliwa kwa makada hao ni Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Mangula aliyesema amefungua faili kwa ajili ya makada hao.
Alisema suala jingine alilowasilisha Mangula ni ripoti ya ziara yake aliyoifanya katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Tanga.
Februari 18, mwaka huu CCM kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete.
waachwe kwa wanaoutaka urais wajitangaze mapema ili tuwajue na kupima dhamira zao, kujua mienendo yao na kuwa na maamuzi sahihi kuwahusu. Urais siyo suala la kuamua leo na kesho kutangaza nia..hata uenyekiti wa kitongoji unahitaji maandalizi..kiongozi anaandaliwa, na urais ni uwekezaji wa muda mrefu.
Naungana na bwana Fadhil,ni vema CCM ingeweka utaratibu wa kuwapa uhuru wenye nia kujitangaza mapema hata mwaka mmoja hadi miwili kabla ya uchaguzi ili waweze kuji chuja wenyewe kutokana na wananchi kupitia taarifa zao kwa kina na kuwahoji inapowezekana, na hata wenyewe kujiandaa ili tupate kiongozi bora.
Nafikiri makamu mwenyekiti na wenzake wako sahihi kwasababu kila chama kina taratibu,miiko,irani na mipanglio yake hivyo basi kila mwanachama lazima afuate taratibu hizo