27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

CCM MISUNGWI YAMCHONGEA MKURUGENZI KWA MAGUFULI


Na PETER FABIAN    |      

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Misungwi, kimemuomba Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli kutuma vyombo vyake vya uchunguzi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.

Kimedai hiyo ni kutokana na utendaji usioridhisha wa Mkurugenzi Mtendaji, Eliud Mwaiteleke ili kuinusuri halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Misungwi, Daud Gambadu alikuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi.

Alidai hali katika halmashauri hiyo siyo nzuri kwa kuwa kumekuwa na utafunaji wa fedha ambao unaonekana kufumbiwa macho na mkurugenzi huyo.

Alisema katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kilichomalizika hivi karibuni ilielezwa baadhi ya watendaji wa vijiji na kata wametafuna mamilioni ya fedha walizokusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani.

“Tuombe Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa chama, ainusuru Misungwi kwa kumuondoa mkurugenzi huyu.

“Inaonekana ameshindwa kusimamia mapato ya fedha za wananchi hivyo inatupa wasiwasi kuwa huenda naye ni sehemu ya tatizo,” alisema.

Alisema kwa sasa ndani ya halmashauri hiyo kuna mgogoro baina ya mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na watendaji wengine.

Mkurugenzi Mtendaji Eliud Mwaiteleke alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alisema hana taarifa na mambo hayo.

Alisema wanaoendesha kampeni za kumuondoa wamebanwa naye ndiyo sababu wameanza kutapatapa.

Hata hivyo, Gambadu alisema hali hiyo imekuwa ikichangia utafunaji fedha za mapato na kutotekelezwa miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za mapato yake ya ndani.

Alisema kutokana na mgogoro huo Misungwi imekwama kutekeleza Ilani ya CCM.

“Roho ya halmashauri ni mapato yakiendelea kushuka utekelezwaji wa Ilani ya chama utasuasua na kutupa wakati mgumu kwa wananchi wakati wa kunadi wagombea wetu katika chaguzi zijazo.

“Tulipata taarifa kama Uongozi wa Chama Wilaya kuwa wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri hii waliokuwa wakikagua vyanzo vya ukusanyaji mapato walizuiliwa na kushushwa kwenye gari na mkurugenzi.

“Hivyo  tunatarajia hivi karibuni kumwita Mkurugenzi, Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani wenzake wa CCM na Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda kujadili hali iliyopo,”alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles