29.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

CCM Kilimanjaro yawaonya wagombea ubunge

Na Safina Sarwatt-Kilimanjaro

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewataka watia nia nafasi ya ubunge katika majimbo mbalimbali mkoani hapa  kuvunja makundi ndani ya chama hicho mara baada ya kumalizika kwa kura za maoni.

Boisafi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi na watia nia wapatao 388 katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira.

“Zoezi la kura za maoni limeshamalizika na kila mgombea amepata alichokipanda, na sasa ni wakati wa kuvunja makundi makundi ya wagombea uchaguzi na kuwa kitu kimoja ili kukiimarisha chama ili kiweze kushinda katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,” alisema Boisafi. 

Alisema mwaka huu CCM Mkoa wa Kilimanjaro inakusudia kukomboa majimbo yote tisa ya uchaguzi na mkoa kuwa wa kijani kwani hata idadi ya watia nia waliojitokeza katika kuwania kuteuliwa kuwa mgombea ubunge ni kubwa na inaonyesha mkoa ulivyo na hazina kubwa ya wasomi na watia nia wenye sifa.

Boisafi alisema katika Uchaguzi Mkuu uliipita mwaka 2015, Mkoa wa Kilimanjaro haukuwa na matokeo rafiki kwa kura za Rais ambapo Dk. John Magufuli alipata  asilimia 38 ya kura, lakini uchaguzi wa mwaka huu atapata asilimia 95 .

Alisema uchaguzi wa kura za maoni ulikuwa wa huru na haki na hakuna mgombea yoyote aliyekamatwa kwa rushwa, huku akitoa rai kwa watia nia wote kutumia elimu walizonazo na ahadi walizotoa kwa wanachama ili kuleta maendeleo ya wananchi.

Aliwataka wagombea hao kuachana na tabia za usaliti kwani inaonyesha wagombea wengi wakishindwa katika kura za maoni mchana utawaona wamevaa nguo za CCM, na usiku wanavaa nguo za baibui na kwenda kambi ya upinzani na kukisaliti chama.

Boisafi alisema CCM ya sasa sio ya mchezo mchezo na kwamba itakapombaini mwanachama, kiongozi ama mgombea amekisaliti chama watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kusimamishwa uanachama ama kufukuzwa.

Alisema CCM haitakubali kuona mbunge atakayechaguliwa na wananchi hawezi kutekeleza majukumu yake na kwamba kila mbunge atakaguliwa kazi zake anazozifanya kila mwaka na atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake, CCM haitasita kumfukuza uanachama kwa kumnyang’anya kadi ya chama hicho.

Mmoja wa watia nia katika Jimbo la Vunjo, Chrispin Meela ambaye katika kura za maoni alipata kura 47 na kupata nafasi ya tatu, alisema kuwa uchaguzi ulikuwa wa haki na kwamba atakwenda kumuunga mkono mgombea atakayepitishwa na chama hicho. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,701FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles