26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM ilivyojipatia ushindi kabla ya sanduku la kura

Na WAANDISHI WETU – mikoani

WAKATI Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukifanyika leo maeneo mbalimbali nchini, mikoa mitatu haitafanya uchaguzi huo kutokana na wagombea wake kupita bila kupingwa.

Tayari baadhi ya vyama vya upinzani, vikiwamo vile vikubwa vya Chadema na ACT-Wazalendo vilikwishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo kwa madai kwamba hatua ya uchukuaji na urejeshaji fomu iligubikwa hujuma na upendeleo.

Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo, mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume) na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi la wanawake) katika mamlaka za miji.

Nafasi nyingine ni mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji (kundi mchanganyiko wanaume na wanawake), wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.

Akizungumzia uchaguzi huo jana Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema maandalizi yote yamekamilika.

Alitaja mikoa ya Tanga, Katavi na Ruvuma haitafanya uchaguzi huo kutokana na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa.

“Mara baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu kukamilika na zoezi la kampeni kukamilika, kesho (leo) tunaingia kwenye zoezi la upigaji kura, niwaombe wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura,” alisema Jafo.

Alisema katika uchaguzi huo wazee na wajawazito wanatakiwa kupewa kipaumbele.

Jafo alisema mambo ambayo hayahitajiki wakati wa uchaguzi huo ni wagombea kufanya kampeni wakati wa upigaji kura na kuvaa sare za chama.

Alisema upigaji kura unatarajiwa kuanza saa 2.00 asubuhi na kukamilika saa 10.00 jioni.

“Niwatoe hofu, kura zitahesabiwa katika mitaa husika na jioni matokeo yatakuwa yamepatikana na Jumatatu nitatoa tathmini ya jinsi zoezi lilivyoenda,” alisema Jafo.

Aliwataka wasimamizi wa uchaguzi huo kufuata sheria kanuni na taratibu zilizowekwa wakati wa upigaji kura.

Alipoulizwa ni vyama vingapi vitashiriki uchaguzi huo, Jafo alisema vipo 19 ambavyo vimepewa usajili wa kudumu na kuahidi kueleza zaidi kesho.

Katika hatua nyingine,CCMMkoa wa Mwanza imesema ahadi za wagombea wa Serikali za mitaa na vijiji zilizotarajiwa kutolewa majukwaani, zitatangazwa baada ya kuapishwa kwa kuwa wagombea wao wamepita bila kupingwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salim Kalli alisema hawakufanya kampeni kwa sababu hakukuwa na vyama vingine vinavyoshiriki, hivyo wameamua kuendelea kujenga umoja wa wanachama wao.

 “Baada ya wagombea wetu kutangazwa washindi na Tume ya Uchaguzi na kuapishwa, hapo ndipo sasa watakuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano wa wananchi na kuwashukuru, vilevile watatumia mwanya huo kuwaeleza mambo watakayotekeleza ndani ya miaka mitano,” alisema Kalli.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Gavenga aliwataka waliokuwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa mitaa kushirikiana na wale waliopitishwa ili kujenga umoja na ushirikiano ndani ya chama hicho.

Gavenga aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwa kuwa inawajali wanyonge.

Hivi karibuni CCM Mkoa wa Mwanza ilitangaza kupita bila kupingwa kwa asilimia 100 katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela ambako wagombea 346 wa nafasi ya mwenyekiti wanasubiri kuapishwa Novemba 25.

CCM Simiyu yapita bila kupingwa vijiji 585

Katika Mkoa wa Simiyu, CCM pia imepita bila kupingwa katika vijiji 585 kati ya 586 vilivyoko mkoani humo.

Wananchi wa Kijiji cha Senani, Kata ya Chinamili, Wilaya ya Itilima mkoani humo, ndio watalazimika kupiga kura kuwachagua viongozi wao, mwenyekiti wa kijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe mchanganyiko.

Vyama viwili – CCM na United Democratic Party (UDP) ndivyo vitachuana kutokana na wagombea wao kuteuliwa kuwania nafasi hizo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili ofisini kwake jana, mratibu wa uchaguzi mkoani humo, Maganga Simon alikiri vyama vingine vya kisiasa kujitoa katika kinyang’anyiro hicho. 

“Kwingineko hatutafanya uchaguzi kwa sababu wagombea kutoka CCM walipita bila kupingwa, CCM imepita bila kupingwa katika vijiji 585 sawa na asilimia 99… Baada ya maelekezo ya Waziri Jafo walishindwa kutekeleza maagizo (waraka) juu ya walioridhia kujitoa baada ya rufaa,” alisema Maganga.

Jumla ya wananchi 1,200 wanatarajiwa kupiga kura Kijiji cha Senani ambao kati yao wanaume wako 508 na wanawake 692.

WASIMAMIZI WAONYWA

Wakati huohuo, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, umewaonya watendaji na wasimamizi wa uchaguzi huo kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Onyo hilo lilitolewa jana na msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, Mbawala Kanoti katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa mara kwa mara wasimamizi wa uchaguzi katika vituo vya kupigia kura ndio wamekuwa wakisababisha wananchi kutokuwa na imani na matokeo kutokana na baadhi yao kukiuka madili yao ya kazi.

“Uzoefu unaonyesha sisi watendaji wa Serikali ndio tumekuwa vinara kwa tukisababisha kuibuka malalamiko kutoka kwa wapigakura, hivyo lazima mkumbuke kuwa vyombo vya sheria havitawavumilia endapo mtakwenda kinyume na utaratibu,” alisema Kanoti.

Alisema vitongoji 78, vijiji 33 na kata 14, ndio vitashiriki katika uchaguzi huo.

Alisema kuwa katika wilaya hiyo jumla ya vijiji 78, vitongoji na kata 344, hakutakuwa na uchaguzi kutokana na wagombea wa baadhi ya vyama vya upinzani kujitoa.

Habari hii imeandaliwa na RAMADHAN HASSAN (DODOMA), BENJAMIN MASESE (MWANZA), DERICK MILTON (SIMIYU) na GURIAN ADOLF (KALAMBO)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles