24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

CCM Ilala watuma salamu walioanza kampeni kabla ya wakati

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kimewaonya wanachama walioanza kampeni kabla ya wakati na kutahadharisha kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alikemea wanachama walioanza kampeni kabla ya wakati na wanaotukana wenzao kwamba watashughulikiwa.

Akizungumza Februari 21,2025 wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya kilichokuwa kikipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Sylivester Yared, amesema hawatabeba mgombea yeyote na hakutakuwa na mgombea atakayepita bila kupingwa.

“Tukizingatia maelekezo ya Katibu Mkuu (Dk. Nchimbi) aliyoyatoa Dodoma nasi Wilaya ya Ilala tumeweka msisitizo, katika kipindi hiki hatutaruhusu wanachama wa CCM kupitapita kukusanya wajumbe na kugawa fedha. Wale wote watakaothibitika wanazunguka hatutasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu ikiwemo kutowaweka katika orodha ya wagombea.

“Katiba, kanuni za uchaguzi, kanuni za usalama na maadili ndani ya chama zinaelekeza. Tumewaelekeza madiwani, wabunge na wenyeviti wa mitaa watimize wajibu wao, hakuna mtu atakayekuwa na mbeleko kwa diwani, kwa mbunge ama mwenyekiti atakayeshindwa kutimiza wajibu wake,” amesema Yared.

Katika hatua nyingine chama hicho kimesema kimeridhishwa na utekelezaji Ilani ya Uchaguzi kupitia taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

Aidha kimetoa siku saba kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha tanki la maji Bangulo linaanza kufanya kazi na wananchi wanapata maji.

Katibu huyo pia amesema wamebaini baadhi ya wakandarasi wamechelewesha miradi ya ujenzi licha ya kulipwa na kuelekeza mikataba yao ivunjwe au watozwe faini pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema wamepokea zaidi ya Sh bilioni 317 kutoka Serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, miundombinu na maji ambazo zimeboresha utoaji huduma kwa wananchi na kuwaondolea adha walizokuwa wakikumbana nazo.

Mpogolo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi kwa njia ya Tehama ambayo ilionyesha miradi mbalimbali ilivyotekelezwa kama vile ujenzi wa shule za sekondari kwa mtindo wa ghorofa, vituo vya afya na utoaji mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha nyingi alizoleta katika wilaya yetu, kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika ili kuwaondolea kero wananchi katika kupata huduma mbalimbali,” amesema Mpogolo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema watafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na chama na kwamba katika tanki la Bangulo maji yanaendelea kujazwa na wanatarajia wakati wowote kuanzia sasa yataanza kutoka katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles