22.8 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

CCM ILALA INAFANYA KAZI KUBWA KUIMARISHA MATAWI, MASHINA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


KAZI kubwa ya chama chochote cha siasa ni kushika madaraka na kuongoza Serikali na harakati hizo huwa zinafanikishwa kwa ushirikiano wa ngazi mbalimbali katika chama husika.

Hii ni kwa sababu katika ngazi hizo kuna ushawishi mkubwa wa wanachama na pia vyama huweza kushughulikia matakwa ya wananchi kwa ukaribu.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinazo jumuiya zake ikiwamo Jumuiya ya Wazazi ambazo zote kwa pamoja zinahakikisha kwamba chama hicho kinaendelea kushika dola.

Katika kuadhimisha Wiki ya Wazazi mwaka huu, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala iliamua kutembelea kata zote 36 kuangalia uhai wa jumuiya hiyo.

Inaeleweka wazi kwamba nguvu ya chama chochote cha siasa ipo kwenye matawi na mashina kwani huko ndiko ambako watu wengi wanaishi hivyo kunapaswa kuimarishwa.

Katika ngazi hizo kunatakiwa kuwe na watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za chama, wanaoweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea.

Kwa viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hizo wanatakiwa wawe ni wale wanaojua vyema kazi zao za utendaji kulingana na shughuli wanazozifanya.

Ikiwa ni takribani mwaka mmoja umepita tangu CCM kipate viongozi wapya katika ngazi mbalimbali zikiwamo za mashina matawi na kata, katika baadhi ya maeneo kimeanza kujipima kuangalia utendaji wa viongozi husika.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Ubaya Chuma, alisema kuna changamoto hasa katika ngazi ya mashina kwani viongozi wengi hawana uelewa.

“Asilimia 90 ya mabalozi hawajui kuandika mihtasari na hata waliopewa cheo cha Katibu wa Shina tumegundua hawana uelewa.

“Weledi hakuna, kazi ya ukatibu haitendewi haki hivyo tunajipanga kuhakikisha tunafanya semina za mabalozi, viongozi wa matawi na kata,” alisema Chuma.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, walitembelea  zaidi ya matawi 200 na mashina 3,860 na kwamba makatibu 90 tu ndio walioweza kukabidhi taarifa zao za utendaji kazi.

“Tukisema tuwafukuze hakutakuwa na chama katika wilaya hii (Ilala), inavyoonekana mtu alipata cheo lakini cheo hakikupata mtu.

“Tunasema ni marufuku kuokota mwanachama, ni lazima mwanachama apatikane kwa balozi lakini balozi na katibu wake hawajui kuandika mihutasari.

“Tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunaimarisha matawi na mashina ambako ndiko kwenye ushindi…tukirudi tena (akimaanisha wakifanya ziara nyingine) tutaondoka na watu ili mwakani tuingie vizuri kwenye uchaguzi,” alisema Chuma.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala, Lucas Rutainurwa, alisema wamebaini baadhi ya viongozi hawana uzoefu na wengine hawako tayari kuongoza.

“Kuna tatizo la ushirikiano baina ya viongozi wa chama na jumuiya na tatizo ni kubwa sana,” alisema Rutainurwa.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala, Sophia Hamad, alisema jumuiya hiyo ina wanachama 27,591 na kati ya hao wanawake ni 16,368 na wanaume 11,368.

Alisema walifanikiwa kutembelea kata zote za Wilaya ya Ilala lakini wamebaini kuwapo kwa changamoto kadhaa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Tumegundua kuwa viongozi waliochaguliwa wengi wao hawajui majukumu yao hivyo, tunajipanga kuandaa semina za viongozi. Tunaamini ustawi na uhai wa jumuiya unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha chama,” alisema Sophia.

Katibu huyo alisema katika maeneo mengine viongozi wa matawi wameshindwa kufungua akaunti kwa sababu hawana miradi ya kuwaingizia kipato lakini wamewaelekeza jinsi ya kuanzisha miradi.

Alisema mikakati yao ni kubuni miradi ili kuimarisha uchumi wa umoja wa wazazi katika wilaya hiyo pamoja na kulinda na kuhakiki mali zote za jumuiya hiyo.

“Tumejipanga vizuri na tuna mategemeo makubwa kwa wanachama kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Frank Kamugisha, alisema jumuiya hiyo ina wanachama hai 98,000 na kwamba inapitia changamoto mbalimbali lakini ni muhimu viongozi wakajipanga na kutimiza majukumu yao.

“Tusimamie utekelezaji wa ilani, busara itawale katika tunayoyafanya ili kusiwapo na mgawanyiko. Kuwe na vikao vya mara kwa mara kuangalia kama tunatekeleza yale tuliyopaswa kwa wakati husika,” alisema Kamugisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles