30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM HAWALIONI JANGA HILI?

Rais Dkt. John Magufuli

Na Balinagwe Mwambungu,

NCHI yetu inaonekana katika uso wa kimataifa kuwa na waoga na wanafiki, tunatumia vibaya rasilimali fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo ya nchi yetu.

Tamko la Rais John Magufuli la kutowasomesha watoto wanaopata ujauzito wakiwa bado wanasoma, limewaacha midomo wazi wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi.

Tangu tupate uhuru, nchi kadhaa duniani—hasa za Scandinavia—Sweden, Norway na Denmark, zimemwaga fedha nyingi za walipakodi wao kwa ajili ya kuinua sekta ya elimu. Mfano wa kudumu ni uwepo wa Shirika la Elimu Kibaha. Aidha, kuna shule mbalimbali za sekondari zilizojengwa kwa msaada wa nchi hizo—mfano ni Shule ya Sekondari Bagamoyo. Nchi hizo zimegharimia upanuzi na ukarabati wa shule mbalimbali, hasa wakati wa utawala wa Rais Mwalimu Julius Nyerere.

Si hivyo tu, nchi hizo zimesaidia kuendesha miradi ya elimu kwa watoto waliokosa kwenda shule kwa sababu mbalimbali, zikiwamo mimba za utotoni na zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike walio sekondari.

Rais Magufuli amesema wakati wa utawala wake, watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, hawataweza kuendelea na masomo tena.

Hakuna kiongozi yeyote—kuanzia mawaziri wa elimu, afya na ustawi wa jamii—wanaoogopa kumweleza Rais Magufuli ukweli kwamba elimu ndio msingi wa maendeleo na hatutaweza kuendelea na kufikia nchi ya uchumi wa kati, kama sehemu ya jamii yetu imeachwa nje ya mfumo wa elimu na kwamba wizara zao tayari zilikuwa zinatekeleza programu iliyowalenga watoto wa kike—walioshindwa kuendelea na masomo sababu ya kupata ujauzito.

Tanzania ni kati ya nchi zinazoendelea ambazo zimesifiwa katika anga za kimataifa kuhusiana na hatua yake ya kumwelimisha mtoto wa kike na utekelezaji wa haki ya mtoto kupata elimu. Sijui wadau ambao wamekuwa bega kwa bega na nchi yetu katika kuendelea na kuboresha elimu kwa ujumla!

Inashangaza jinsi jamii ya Kitanzania ilivyobadilika ghafla na kuwa kama kondoo (ambaye hata anapopelekwa kuchinjwa, hunyaa tu). Hivi viongozi wenye dhamana ya elimu, afya na ustawi wa jamii hawana uthubutu wa kumwambia Rais kwamba tamko lake ni pigo kubwa kwao—kwa kuwa wamekuwa wakitekeleza mipango mbalimbali kuhusiana na mimba za utotoni na namna ya kumnasua mtoto wa kike aliyepata ujauzito akiwa shuleni.

Afya na Uzazi wa Mpango na ajenda ya kupunguza mimba za utotoni. Katika programu hii wabunge walipewa majukumu, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa wanawahamasisha watoto wa kike kuendelea na masomo pindi wanapopata ujauzito.

Serikali za mitaa, mashirika ya kiraia na makundi mengine, yalikubali kutekeleza mpango huu. Wizara ya Elimu ilikuwa na programu ya MEMKWA na MMEM, zote zikiwalenga zaidi watoto wa kike waliokuwa nje ya utaratibu wa shule. ‘Mabinti Tushike Hatamu’ ni mradi uliokuwa unaendeshwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na UNICEF.

Chukua hili kwa mfano, kwamba mtoto wa kike akipata ujauzito, asirudi shuleni baada ya kujifungua—kwa maelezo kwamba watoto wa kike wataona kuwa ni jambo la kawaida na wataendelea kufanya ngono zembe bila kujali kuwa kuna uwezekano wa kupata mimba.

Rais Magufuli alishangiliwa aliposema wakati wa uongozi wake, hakuna mwanafunzi atakayeruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua. Bila shaka, hili ni kama bomu kwa Mama Salma Kikwete (Mbunge), ambaye kwa mwongo mmoja, kupitia taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), amekuwa anampigania sana mtoto wa kike.

Chakushangaza zaidi ni pale viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Amina Makilagi, anaunga mkono kauli hiyo. (Majira Julai 5, 2017). Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alinukuliwa Aprili mwaka huu, akisema watoto wa kike warudi shuleni baada ya kujifungua.

“Tunapowakataza watoto wa kike wasiendelee na masomo pindi wanapopata ujauzito wakiwa shuleni, tunawaadhibu watoto wa masikini washindwe kutimiza malengo yao ya wakati waliotarajiwa,” alisema.

Aidha, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, Februari, 2016, alitoa mwongozo wa namna ya kumruhusu mwanafunzi wa kike kurejea shuleni baada ya kujifugua. Lakini yote haya inaelekea yamefutwa kwa kauli ya Rais Magufuli.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Unicef, Unesco, Shirika la Afya (WHO), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP), yamekuwa yakifanya kazi na Serikali ya Tanzania kutokana na azma yake thabiti ya kutoa huduma, elimu na mafunzo mbalimbali kwa watoto na vijana.

Hii inatokana na ukweli kwamba, hata kabla ya Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu elimu, ilikwishaingiza kwenye Katiba yake na kutamka kwamba binadamu wote ni sawa, ikapiga marufuku ubaguzi wa aina yoyote, na ikaridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto. Mwaka 2009, Bunge likatunga Sheria ya Mtoto ambayo inasema kuwa ni haki ya mtoto kupata elimu bila ubaguzi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wenye ujauzito.

Leo hii kwa tamko tu, mtoto wa kike atakayepata mimba akiwa shuleni, atakuwa amekatishwa ndoto ya ‘kuwa anachotaka’. Wabunge, hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwa madarakani kwa miongo minne, chama ambacho kiliasisi Elimu kwa Wote (UPE), kimekaa kimya! Vijana wa chama hicho—ambao suala hili linawagusa wao moja kwa moja, wamekaa kimya, badala yake wanaandama viongozi wa vyama vingine ambao wanaikosoa Serikali kwamba inatakiwa kutenda haki kwa wananchi wake wote—wadogo kwa wakubwa. Kama vijana wa CCM hawalioni hili kama ni janga la kijamii, basi wanaugua uzezeta.

Katika mwaka 2015, ambao ndio mwaka wa Uchaguzi Mkuu uliomwingiza Dk. John Magufuli madarakani, watoto wa kike 1,271 kutoka mikoa ya Mbeya (322), Morogoro (260), Mwanza (258), Kilimanjaro (235) na Dodoma (196), walikatishwa masomo kutokana na kupata ujauzito. Je, kwa nchi nzima itakuwaje—maana kama Taifa, hatujapata mwarobaini wake.

Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaonyesha kuwa wasichana kati ya umri wa miaka 15 hadi 20 (umri ambao wanatakiwa wawe shuleni), wanaachishwa masomo kwa sababu ya ujauzito.

Taarifa hiyo inasema idadi ya wasichana wanaopata mimba imepanda kutoka asilima 10, mwaka 2010 na kufikia asilimia 27, mwaka 2015/16.

Hata kwa mtazamo wa juu juu tu, hali hii inatishia si tu kuongezeka kwa umasikini, bali pia kuvuruga mipango ya Serikali kwa sababu ya kuwapo duniani watoto ambao hawakuwa katika mipango ya nchi.

Serikali inapigana na umasikini kupitia Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini (TASAF), na mipango mingine ya kupambana na umasikini—huku kukiwa na ongezeko la watoto wasiotarajiwa. Hii ni sawa na kuchota maji na kujaza kwenye ndoo iliyotoboka chini.

Matokeo yake ni wazi—ndoo hiyo kamwe haitajaa. Mipango ya uchumi na kijamii, haitaweza kufaulu. Kutakuwa na midomo mingi ya kulisha, ongezeko la ombaomba, ‘dada poa’ mijini, na watoto wa mitaani, makundi ambayo Jeshi la Polisi linasumbuka nayo kila uchao! Matatizo haya yanatakiwa kutibiwa kwenye vyanzo vyake—si kwenye matokeo.

Vijana wa CCM wanatakiwa kujiongeza. Waache kugombana na wanasiasa ambao hawatakuwapo miaka 50 ijayo, watafute ufumbuzi wa masuala yanayowahusu vijana, hili likiwa mojawapo.

Elimu ni ufunguo wa maisha. Mnyime mtoto elimu, utakuwa umemfungia mlango wa maendeleo. Tunataka Tanzania ya viwanda, ni lazima wawepo watu—hasa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa—vijana waliojizatiti katika fani mbalimbali na watakaoweza kulisukuma gurudumu la maendeleo. Asiwepo atakayeachwa nyuma na boti ya elimu. Usiwepo ubaguzi—kuwabagua waliokoseshwa elimu (sio kwa mapenzi yao).

Kama mtoto wa kike hatapewa nafasi maalumu, basi malengo ya Elimu Bure, hayatafanikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

7 COMMENTS

  1. Balinagwe Mwambungu kwa heshima zote nilizokuwa nakupa kwa articles zako nzuri huko nyuma, nafuta kabisaa kwa uozo huu ulio utoa kuhusu watoto wanaopata mimba wakiwa Shuleni. Unaonyesha kuwa wewe ndiye sasa uko kwenye dimbwi la uzezeta tayari. Mashirika yote uliyoyataja ya umoja wa mataifa kwa fikra zako unadhani yaliletwa ili kusomesha wenye ziada ya tamaa za miili yao huku wakiwa Shuleni ! Huo ni opotoshaji, watasomeshwa ambao wanatambua umuhimu wa malengo yao katika maisha. Ila ukipenda, washauri watoto wako wafurahie hiyo raha ya mwili na uwapongeze kwa kuwasherehesha kwa kukuletea mjukuu/wajukuu. Bravo, Raisi wetu kwa maamuzi ya busara. Am proud of you my President JPM. Mungu akulinde.

    • Ndugu Masingiriri, kwa heshima kidogo niliyokuwa ninampa Balinagwe, ninajuta nilikuwa ninafanya kosa kubwa mno. Mwandishi ameandika kimantiki sana, na ameiwekea mzani sawia hoja yake tena kwa ‘references’ makini. Ila kwako wewe uliyejibu hoja ya Mwambungu sijui unafikiriaje unaposema kuwa wasichana wanaopata mimba wana ‘ziada ya tamaa za miili yao?’ Ningependa kuusoma utafiti uliofanya kuthibitisha hili. Nikiuona na kujiridhisha madai yako, nitamwuunga mkono JPM

  2. kweli selikari hii imekwisha kuwa na uonevu wa hari ya juu Maana haiwezekani ukamkatisha mtoto kisa vishawishi vya vijana wa kiume.

  3. Ni weee uliotoa ni utumbo. Hwa wtaoto ni athari kipitia mila dume na desturi zrtu za kibantu kumwona mwanamke kama duni. Chombo, si sawa. Huyu mtoto kuna mwanaume nyuma ya pazia ambayo ndugu raisi hsjamtaja na anamtetea ndo aliyembaka kws nguvu, kumhonga pesa, na kutumia ukubwa wake. Unajua huyu no mtoto.kumwingolia mtoto ni kosa la jonsi. Kuna majobaba kama wewe mslaya wengine wameoa nfo wanaostaholi adhabu. Lini elimu itanufaisha umma, italeta sheria safi yenye nguvu na kulinda mwanamke.lini wanaume wasomi viongozi watatumia elimu zao kwa manufaa ya umma. Loni sheria itampa uhuru mwanamke akajivunia elimu na kumpa uhutu kujitetea mwenyrwe, kujiendeleza, kumiliki. No uoga wa mwansume msomi asiyejiamini kgicha ufhaifu wake kwa ukandamizi wa jinsia ili tu kuonekana mtawala. Hata akiwa hastahili hsyo madaraka lakini hajijui sababu tu ya sheria kandamizi inamruhusu.
    Aibu na inachefua.maana na fsida ya elimu si udharalishaji, si mabavu, si uonevu, di kusekwa jera kwa miaka ya karne ya ishirin ns moja. Jamani tumieni utashi..

  4. Hiyo Heshima unayoisema itabaki,Soma vizuri Article yake usikurupuke na kuanza kutoa maoni bubu juu yake, Jiongeze kwanza halafu tafakari kabla ya lawama.

  5. Nadhani huyu jamaa hajamuelewa kabisa Rais amesema nini na anataka nini.Tafadhali,Naomba rudia tena kusikiliza hotuba zote za Rais kuhusu hii issue.

  6. Ni makosa kudhani kwamba kwa kuwaruhusu wanafunzi waliopata mimba na kuzaa ndio ubora wa elimu. Ubora wa elimu, iliyo rasmi, ni pamoja na kuwafanya watoto kutambua umuhimu wa elimu dhidi ya zinaa wakiwa shuleni na kuiepuka, kuimarisha miundo mbinu ya mashule, upatikanaji wa zana za kufundishia na kujifunzia, kuwa na mitaala yenye malengo ya kumfanya mtoto kumudu maisha baada ya kuhitimu elimu, n.k. n.k.
    Ninachofahamu kutokana na kauli ya raisi, isiyoyumbishwa,ni kwamba, aliyepata mimba na kuzaa atakuwa amejitoa rasmi katika ufadhili wa serikali katika shule za serikali za elimu ya msingi na sekondari.Kwa muktadha huu, janga liko wapi la kuitahadharisha CCM?
    Lakini pia, kwa akili za kienyeji, mtoto anayepata mimba itabidi akae miezi tisa nyumbani na baada ya kuzaa (sijui kama kwa utaratibu wenu akina Balinagwe, atapewa likizo ya uzazi) atakaa nyumbani kwa miezi kadhaa ili kumnyonyesha mtoto wake; je akirudi shuleni anaanza alipoachia au anaendelea na wenzake aliokuwa nao? Akipata mimba tena kumbuka mchovya asali hachovi mara moja), iwe hivyo hivyo! Huu utakuwa ni utani!
    Kumbuka mlango mmmoja ukifungwa, kuna mingine mingi iko wazi! Watumie milango mingine ya elimu. Kwani elimu haina mwisho na si ya aina moja tu!
    Jitafakarini!!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles