NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
NAHODHA wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema kuwa wamepania kupata ushindi dhidi ya Malawi ‘The Flames’ kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam keshokutwa ili kuondoa mdudu wa sare tangu Charles Mkwasa apewe kibarua cha kuinoa timu hiyo.
Stars itamenyana na Flames katika mchezo wa awali wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, Mkwasa ataingia kwenye mechi hiyo akiwa hajaambulia ushindi katika mechi mbili za mashindano alizoiongoza Stars, akiambulia sare mbili.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Cannavaro alisema sare dhidi ya Uganda na Nigeria zimetosha na sasa watahakikisha wanaanza kupata ushindi.
“Hatuhitaji sare nyingine kwenye mchezo huu wa tatu tangu tuwe na kocha wetu Charles Mkwasa, hizo zinatosha na sasa ni ushindi tu tutahakikisha tunaanza na timu hii ili kujiwekea mazingira mazuri ugenini,” alisema.
Nahodha huyo wa Yanga, alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wote nia yao ni moja ya kuhakikisha wanalipatia ushindi Taifa na kuongeza matumaini kwa mashabiki wa soka nchini na kuongeza mapenzi yao kwa timu hiyo.