22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

CAG, Bunge mtegoni

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusisitiza msimamo wake wa kukataa kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na kukubali kufanya kazi na Ofisi anayoiongoza, msimamo huo umezidi kuliweka njia panda jambo hilo.

Wakati baadhi ya wanasheria wakiona bado kauli hiyo ya Spika Ndugai inazaa  utata kwa kuwa si rahisi kumtenganisha  CAG Assad na Ofisi ya CAG ambayo yeye ndiye mtendaji wake Mkuu, Katiba nayo ina maelezo yake.

Katika Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaeleza kuwa Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuainisha majukumu yake, maelezo yake hayo nayo yanaacha maswali iwapo Bunge litaweza kujitenga na CAG ambaye kwa sasa ni Prof. Assad.  

Mfano wa wazi ambao baadhi wanaona ni vigumu Bunge kumkwepa CAG, Prof. Assad, umo katika Ibara hiyo ya 143 (4) ambayo inaainisha kuwa;

“Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.

Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge, basi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu wa Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge”.

Kutokana na maelezo hayo na mengine yaliyofafanuliwa katika ibara hiyo ya Katiba, lakini pia kauli hiyo ya Spika Ndugai, aliyekuwa Mjumbe wa 

Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambaye kwa taaluma ni Mwanasheria, Awadh Ali Said, amesema ni vigumu Bunge kumkwepa CAG, Prof. Assad, kwa sababu Assad ni CAG na likifanya hivyo litakuwa linavunja Katiba.

Awadh ambaye ni Wakili visiwani Zanzibar akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kutoka visiwani humo, alisisitiza kuwa Bunge kama mhimili mmojawapo wa dola haliko juu ya Katiba na kwamba Katiba iko juu ya mihimili yote.

“Yale yaliyoelekezwa kwenye Katiba huwezi kuamua tofauti, GAG anawajibika kikatiba kufanya kazi yake, sasa yeye Spika akiamua kusema sifanyi kazi ya huyu nafanya ya yule ni kinyume na Katiba.”

“Yule alipohojiwa kule alihojiwa kama CAG hakuhojiwa kama Prof. Assad na kama alichokisema yalikuwa maoni yake binafsi angesema, hakusema, lakini tangu lini Bunge linafanya kazi na Assad, Bunge linafanya kazi na CAG, yule umtake usimtake amewekwa na Katiba, Bunge linapangiwa na Katiba,” alisema Awadh.

Awadh ambaye alishiriki mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania ambayo hadi sasa mchakato wake haujakamilika, alisisitiza kuwa Bunge linaweza kumkwepa GAC Assad lakini lijue litakuwa linavunja Katiba.

“Wewe ni msimamizi wa matakwa ya wananchi (Bunge) na yeye CAG anakuletea vitu vinavyokufanya utimize majukumu yako, ni kama vile mpishi halafu wewe mpishi uanze kusema sipikii viungo vyake utaweza kupika chakula kweli?” alihoji Mwanasheria huyo.

Alipoulizwa iwapo Spika Ndugai anaona kufanya kazi na Ofisi ya CAG ni tofauti na kufanya kazi na Prof. Assad, Mwanasheria huyo alisema hilo ni jambo lisilowezekana kwa sababu Katiba haiteui Ofisi ya CAG inamteua CAG na kwamba hata ripoti zake zinasomeka ripoti ya CAG na ofisi inasimamiwa na CAG ambaye kwa sasa ni Prof. Assad.

“Sasa wewe ukipingana na Katiba unakuwa umevunja Katiba,” alisema Awadh ambaye alisema hata mchakato wa kumwondoa CAG ulioainishwa kwenye Katiba unahusu kama amekiuka maadili na si suala la kupeleka ripoti.

Tangu Bunge litangaze kususa kufanya kazi na Prof. Assad, msimamo huo umeibua mjadala mkali ambao ulimlazimisha CAG mwenyewe kusema suala hilo inabidi liangaliwe kwa busara zaidi kwani linaweza kuwa na athari kubwa kuliko linavyotazamwa.

 “Mimi nafikiri tukae chini tutazame halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka tatizo ambalo linaweza kutokea.

“Ninaamini kuna watu wana busara na ‘probably’ wanatoa busara zao, wasiwasi wangu ni kwamba linaweza kuwa tatizo kubwa kuliko lilivyo sasa hivi.

 “‘Technically’ inaweza kuibua ‘constitutional crisis’ (mgogoro wa kikatiba) kwa sababu ripoti (Ripoti za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za mwaka 2017/18), imeshawasilishwa kwa Rais na mimi siwakilishi ripoti bungeni.

“Kwa hiyo Rais atasababisha ripoti zile ziende bungeni… na kama Bunge litakataa kuzipokea, hiyo itakuwa tatizo kubwa zaidi. Kwa hiyo wasiwasi wangu ni huo. Na zikishawasilishwa bungeni zinakuwa ‘public document’, mimi ninapata fursa ya kuzungumza.

 “Tafsiri ya kwamba hatutafanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana, inatakiwa tuijue vizuri,” alikaririwa CAG Prof. Assad mapema wiki hii.

Yeye mwenyewe Prof. Assad amekwishasema hana uamuzi wowote wa kuchukua na kwamba anachokifanya sasa ni kufanya dua watu waongoze vizuri, wafanye maamuzi ambayo yana faida na nchi hii basi.

NDUGAI

Juzi baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai alisema: “Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti tofauti kuhusiana na lile azimio la Bunge kwamba tumekataa kufanya kazi na Ofisi ya CAG.

“Hakuna sehemu yoyote ambayo Bunge limekataa kufanya kazi na Ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu ambaye ni Profesa Assad basi, tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma kwa kuuchanganya.”

Juzi hiyo hiyo jioni Ndugai alipofanya mkutano na waandishi wa habari na alipoulizwa kama ataipokea ripoti ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad, alisema: “Hii habari ya saini hilo halinihusu, sisi hatufanyi kazi na Assad.”

Alisema yeye ameaminiwa na watu wa Kongwa na wabunge wengine pia wameaminiwa na wananchi si mbuzi.

“Huyu aliyetudharau sisi, mimi kule Kongwa ndio wameniamini, tena hii mara ya nne, mimi si mjinga, ndivyo walivyoingia wote, mtu kaaminiwa na watu si mbuzi na hatujamchokoza yeye anakwenda huko anasema.

“Hii vipi na mnajua kwanini tunakasirika, baadhi yetu huwa mnaingia kwenye Kamati ya PAC, mmewahi kukuta kikao ambacho hakina maofisa wa CAG? Ni lazima wawepo wale.

“Yaani tofauti na ofisa yeyote Ofisi ya CAG ni ‘part’ ya kila kitu. Hivi mtu ambaye umeshirikishwa kiasi hicho unawezaje kukaa pembeni na kusema dhaifu, yule si mimi wakati wewe ni ‘part’ (sehemu) na hii ni tabia fulani ambayo si ya kiungwana, lile jambo lilitukera,” alisema Spika Ndugai.

Alisema alipoulizwa CAG alisema anajibu kihasibu akaambiwa tupe kamusi ya kihasibu.

“Hatuendi hivyo duniani, kama mtu analalamika neno lako linanikwaza unaomba msamaha mambo yanaendelea kama kawaida,” alisema.

ILIVYOKUWA SAKATA LA CAG NA BUNGE

Januari 20 mwaka huu, Profesa Assad alifika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku kamati hiyo ikitumia zaidi ya saa tatu kumhoji.

Kuhojiwa huko kulitokana na wito wa Spika Ndugai wa Januari 7, kutokana na kauli yake ya kuliita Bunge dhaifu.

Profesa Assad alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, baada ya kuulizwa juu ya ripoti zake za kila mwaka ambazo baadhi ya watu wanaona kama hazifanyiwi kazi.

Akijibu swali hilo alisema: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles