27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CAG atoa mbinu vita dhidi ya rushwa

CHRISTINA GAULANGA NA ASHA BANI – Dar es Salaam

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Asad, amesema rushwa katika sekta mbalimbali za umma nchini haitaweza kuondoka kama hakutakuwa na uwazi.

Profesa Assad aliyasema hayo jana katika kongamano la maadhimisho ya siku maalumu ya kutafakari mapambano dhidi ya rushwa iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) ikishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kongamano hilo lilifanyika katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu sabasaba, viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Profesa Assad alisema endapo kutakuwa na uwazi katika kila jambo, ikiwemo tenda mbalimbali na masuala ya ajira nchini, rushwa itakwisha.

“Hakuna asiyefahamu kuwa mwarobaini wa rushwa ni uwazi, hasa katika tenda mbalimbali kwenye sekta za umma na hata ajira, kukiwa na uwazi tatizo la rushwa litakwisha,” alisema Profesa Assad.

Katika kongamano hilo kulijadiliwa mada tatu ambazo ni mwelekeo wa Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, wajibu wa sekta binafsi katika mapambano hayo na athari za rushwa katika uchumi.

Akizungumzia mada iliyojadiliwa kwenye kongamano hilo, wajibu wa sekta binafsi katika mapambano dhidi ya rushwa, Profesa Assad alisema anashangaa kuachwa sekta ya umma.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kuzungumzia utii wa sheria, kama hakutakuwa na kutii sheria, kama kutakuwa na mambo ya ujanja ujanja na kukunja kunja bila kutii sheria, kesho mtu atakwenda mahakamani na gharama itakuwa kubwa ya kulipa,” alisema.

Aliongeza kuwa njia pekee ya kuhakikisha rushwa inakwisha ni kuhakikisha kuna uwazi kwa kila tenda na huo uwazi kila mtu aweze kuuona na kusiwe na baadhi ya taarifa ambazo wengine hawawezi kuziona.

Alisema majadiliano kuhusu tenda mbalimbali yanatakiwa kufanyika kwa uwazi, kila mmoja aone na kusikia badala ya watu fulani kuweka usiri.

MKURUGENZI TAKUKURU

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athuman, alisema suala la rushwa linamgusa kila Mtanzania, bila kujali dini wala itikadi, na kwamba kupitia mjadala huo watafanikiwa kujadili changamoto katika sekta ya biashara na kushirikiana na sekta binafsi kwa  mapambano dhidi ya rushwa.

“Suala la rushwa linamgusa kila Mtanzania bila kujali dini wala itikadi, hivyo linatakiwa kuwa changamoto ya kipekee na ishirikishe na sekta mbalimbali za biashara nchini,” alisema Athuman.

MKUCHIKA

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Mkuchika, alisema tafiti zinaonesha Tanzania imeanza kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora.

Alisema Serikali inatumia nguvu kubwa kupambana na rushwa ili kuiletea maendeleo nchi na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Mipango yote ya Serikali ya kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hauwezi kufikiwa pasipo na mapambano dhidi ya rushwa, ndiyo maana tumekuwa wakali sana,” alisema.

Mkuchika alisema matokeo ya mapambano hayo ni kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa huduma kwa Watanzania, ikiwemo elimu bure.

Alisema ifikapo mwaka 2020/25 Tanzania inaingia katika uchumi wa kati huku sekta ya viwanda ikifanywa kuwa kiungo cha kufikia malengo hayo.

Alisisitiza sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kutokana na kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa Watanzania.

“Tangu kuanza kwa ujenzi wa viwanda mkoani Pwani, ni ajira 50,000 zimezalishwa zikiwamo za muda na kudumu, hivyo matokeo hayo yanaashiria uimara wa sekta hiyo katika kukuza uchumi,” alisema Mkuchika.

Alisema sekta hiyo ndiyo itakayobadilisha maisha ya Watanzania kwa kuwa Serikali imejipanga kufanya mabadiliko ya sheria kandamizi kwa wawekezaji, kupunguza utitiri wa tozo na kutoa mafunzo mbalimbali yatakayosimamia ukuzaji wa viwanda na usimamizi wa kodi na viwango vyake.

MKURUGENZI TANTRADE

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka, alisema rushwa imekuwa kikwazo cha uwekezaji kwani wengi wanakata tamaa na kuondoka kutokana na kushindwa kuhimili milolongo.

Alisema wawekezaji wengi wanahofu kupoteza muda mwingi wa ufuatiliaji, matumizi makubwa ya rasilimali fedha na hatimaye kumaliza mitaji.

“Mlolongo wa rushwa kwa wawekezaji ndiyo sababu ya wananchi kukosa huduma ya bidhaa bora na kusababisha uingizwaji wa bidhaa kwa njia zisizo rasmi,” alisema.

KATIBU MKUU CCM

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, alisema ilani ya chama chao iliweka lengo la kukabili mambo manne aliyoyataja kuwa ni ajira, umasikini, rushwa na ufisadi na usalama na amani ya nchi, ndiyo maana kumekuwa na upungufu wa matukio ya rushwa nchini.

Alitaja sehemu ambazo zimegubikwa na rushwa zaidi kuwa ni vyama vya ushirika, migogoro ya mirathi na ndoa, migogoro kazini, migogoro ya ardhi, kodi, usalama barabarani na shughuli za uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles