22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

CAG ABAINISHA VURUGU YATAWALA SEKTA YA NISHATI

Na Mwandishi wetu


UENDESHAJI shughuli bila nidhamu ya fedha, ahadi hewa za malipo na ubabe zimetawala sekta ya nishati, kiasi kwamba kama juhudi za ziada hazitafanywa, kuna hatari mambo mengi yatakwama na uchumi wa nchi kudorora.

Akizungumzia matendo ya sekta hiyo ya mwaka 2015 hadi 2016, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad,  ameonesha kuna udhaifu mkubwa kwenye mikataba yake isiyojali masilahi ya wahusika wakuu wa sekta hiyo wakiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), TPDC, Benki ya EXIM ya China  na EWURA na wateja wao na kuonekana kuchezeana shere tu.

Mapungufu mengi yameonekana katika upangaji bei, malipo ya huduma na kukosekana sera na mikataba thabiti ya malipo inayofanya ionekane kuwa mdai na mdaiwa kuwa ni sawa na kukosa uwezo wa kuchukuliwa hatua kwa wale wanaoboronga au kushindwa kutekeleza mapatano.

Dhana ya watoto wa baba na mama mmoja imetamalaki sekta hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa mmiliki ni Serikali yenyewe na hivyo kuleta simanzi, jakamoyo na sintofahamu nyingi kwa wadau wake.

TPDC  limekuwa jalala la lawama wakati wakosaji ni Tanesco na Ewura ambao matendo yao yanakwamisha mwenendo mzima wa shughuli na kufanya sekta isikue kwa kukosa mwenendo mwafaka wa fedha (financial flows) na miradi kutetereka au kusinyaa.

Uwezo wa bomba la gesi toka Mtwara ni asilimia 6 tu ndio inatumika vilivyo na Tanesco  na ushahidi upo wazi kuwa bomba limeletwa Dar wakati mikataba ya kutumia gesi  hiyo haijafanywa na wateja na ilipofanywa imeonesha kukosa umahiri  na kuna udhaifu mkubwa wa viwango vya bei kwa  kuweka bei moja kwa wote bila kujali matumizi na mahali.

Gesi asilia inaweza kutumika kiwandani kama malighafi au kama nishati na hivyo inadai viwango tofauti kwa watumiaji kwani kama malighafi haina kodi wakati nishati inakodi ya ongezeko la thamani.

“Ni makosa kimkakati kwa wateja wote kuwa na bei moja bila kujali umbali wao kutoka chanzo ikiwamo yule wa Mtwara kulipa bei sawa na yule wa Dar es Salaam  aliyeko kilomita zaidi ya 500,” alibainisha Profesa Assad.

Ankara za TPDC za gesi asilia hazilipwi na Tanesco bila sababu yoyote kwa madai kuwa hakuna fedha wakati inakusanya fedha kwa wateja wake inapowauzia umeme. TPDC inadaiwa kutotekeleza majukumu yake ikiwa kupanga bei wakati shughuli hiyo ni ya Ewura kisheria.

Kipengele cha kuibana Serikali kulipia gesi hata kama isipoitumia kwa maana ya  gharama ya ujazo (capacity charge), ni kitendawili kilichokosa uteguzi. Vilevile suala la mabaki ya gesi bado ni ajenda iliyokosa mwenyewe.

“Ni makosa kwa Tanesco kuendelea kununua gesi asilia kwa bei isiyo tofauti kutoka wale wanaoiuzia wakati wengine wako kwenye biashara hiyo kwa miaka 25 iliyopita na kuwa wamerudisha kwa kiasi baadhi ya gharama zao,” anahoji CAG.

Prof Assad ana wasiwasi kuwa deni halitalipwa kwani matumizi yanayoacha asilimia 94 bila mteja ni hatari na kutaka juhudi ya ziada zifanyike kupata wateja wanaolipa ili deni kwa Benki ya Exim lisidode.

“Inahitajika Tanesco imalize miradi yake ya uzalishaji umeme ikiwamo Kinyerezi II ili deni liweze kulipwa kama livyopangwa badala ya kutegemea Serikali kwa kila kitu,” anadai CAG.

Inaonekana Ewura imeshindwa kuandaa rasimu ya bei kwa wateja mbalimbali na hivyo kuleta vurugu katika soko na kutaka  hali irekebishwe.  

CAG anataka madeni wanayodaiana  TPDC na Tanesco ambayo yamefikia zaidi ya Dola za Marekani milioni 61.35 na dhamana iliyotakiwa kuwekwa na Serikali, ifanye hima kuitekeleza ili mfumo uende mbele, vinginevyo ufanisi unapungua kwa mashirika hayo kwa kudai kuwa fedha hakuna na hivyo kuboronga kazi na hakuna wa kulaumiwa.

“Serikali haijaweka dhamana hiyo na deni halijalipwa na hivyo kufanya mzunguko wa mkwamo wa malipo, kwani TPDC inashindwa kuwalipa waliompa gesi asilia na wao kushindwa kuwalipa wafanyakazi wao mishahara,” alibainisha Prof Assad.

Wachunguzi wa mambo katika sekta hiyo wanashauri uwajibikaji wa hali ya juu ushamiri katika sekta nzima na kutaka wizara ichukue nafasi  yake kukwamua mambo, kwani kihesabu lazima kuonekane kupokea na kutoa katika vitabu vya hesabu na vionekane sawa na sahihi.

“Ni makosa kwa gesi asilia kukosa wateja kwani inakuwa kinyume cha matarajio ya kila mtu na hivyo kufifisha ari ya uchumi wa viwanda.”

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles