Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Taasisi Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ameelezea misingi ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliiacha kuwa ni pamoja na haki ya kusema na kushiriki demokrasia.
Butiku aliyasema hayo juzi wakati wa kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais Dk. John Magufuli.
Butiku alisema Mwalimu Nyerere alikuwa gwiji wa utamaduni na sanaa na alikuwa ni mtu wa imani kwa Mungu na binadamu wenzake aliwapenda.
“Misingi ya taifa hili hakuanza na Azimio la Arusha, ilianza na Katiba ya Tanu kwamba binadamu wote ni sawa na sisi ni familia moja.
“Hiyo ndiyo Tanzania kwamba sisi ni familia moja kwa sababu sisi wote ni sawa hivyo tuna haki sawa, haki ya uhuru, haki ya kusema na haki kushiriki demokraisa, Tanzania haina ubaguzi na hiyo ndiyo misingi inayotawala mambo haya tusiyasahamu,”alisema Butiku.
Alisema Mwalimu Nyerere aliwaachia Watanzania ujamaa lakini siku hizi hakuna anayezungumzia hilo.
Aliwataka wasanii hao kutosahau misingi mingine miwili aliyoacha Mwalimu Nyerere kuwa ni itikadi na vyombo vinavyosimamia itikadi na chombo cha mwisho ni binadamu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally alisema Mwalimu Nyerere alitaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lugha ya Kiswahili vidumishwe.
Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema mambo yanayofanywa na Rais Magufuli kwa sasa ni kuwapitisha kwenye misingi ya Mwalimu Nyerere.
“Sasa hivi tuna ndege wakati hapo awali kulikuwa na mjadala wa kununua ndege ndogo ya rais na kukawa na hofu ya watu kula nyasi. Sasa hivi tunazungumzia dreamliners.
“Ameondoa ufisadi, rushwa na wizi wa rasilimali sasa hivi madini tunaona mapato yake, haya yote mnataka mtu afanye nini ili aonekane anafanya kazi,”alisema Spika Ndugai.