22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Butiku ataka demoksia, uhuru wa habari udaiwe kwa busara

Eliya Mbonea -Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema uhuru wa habari na demokrasia siku zote hauletwi kwenye sahani, bali hutafutwa kwa hatua na gharama. 

Kauli hiyo ameitoa juzi mjini Arusha alipokuwa akifanya majumuisho ya warsha ya wadau wa vyombo vya habari kuhusu ujenzi wa amani nchini. 

Akizungumza na wadau hao Butiku aliwataka wakubali gharama za kuutafuta uhuru, huku akiwatahadharisha kuutafuta kwa unyenyekevu ndani ya Katiba na Sheria.

“Endeleeni kuzungumza mapungufu, lakini mzungumze kwa busara, tambueni mnazungumza na binadamu mwenzenu. 

“Pale wanapokuwa wamefanya makosa wangependa kujitetea kama ambavyo mngefanya ninyi. Kwa hiyo muwe na busara lakini msife moyo na msichoke kwa sababu haki haifi,” alisema Butiku.

Aliwataka wanahabari kujaribu kuwasiliana na kuzungumza kwa busara na hekima lakini iwe kwa kunuia. 

“Haya ni maneno ya wazee na kazi yetu ni kusimamia misingi, nina miaka 81 nitakwenda kaburini nikisikitika ntakapojua mmepoteza uwezo wa kutafuta haki yenu,” alisema Butiku. 

Katika majumuisho hayo, aliwataka wanahabari nchini kuanza kujikomboa kwani bila kufanya hivyo watakuwa risasi hatari.

Awali mwandishi Kulwa Mayombi aliwasilisha mada ya maadili, uzalendo na utaifa kama nyenzo za uandishi wa habari kabla na baada ya uchaguzi ili kulinda amani na umoja wa taifa. 

Naye mwanahabari Novatus Makunga aliwasilisha mada inayozungumzia dhima ya vyombo vya habari katika kudumisha amani na umoja wa taifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi. 

“Wanahabari mnapaswa kuepuka kutangaza taarifa za uchaguzi kwa ushabiki lakini pia wanatakiwa kuzingatia kanuni taratibu na maadili ya uandishi wa habari,” alisema Makunga. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles