Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ameelezea historia ya jengo la taasisi hiyo lililozinduliwa leo na marais wawili jijini Dar es Salaam huku akiwataja marais wastaafu Ally Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete kuhusika.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali na viongozi wastaafu wakkiongozwa na Rais John Magufuli na mgeni wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
Akizungumza katika uzinduzi wa jengo hilo, amesema wazo la kulijenga lilitokana na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kutumika na watu wote na kupata fedha kupitia jengo hilo.
Amesema Mwalimu alimwambia Mwinyi wazo hilo akawapatia kiwanja lakini eneo hilo halikuruhusiwa kujengwa majengo marefu hivyo Kikwete akawapatia kiwanja kingine ambacho wamejenga jingo hilo.
“Kwa kujua kwamba jengo halina fedha, Mwlaimu alimuomba Rais Mwinyi ampe kiwanja na katika kiwanja hicho lijengwe jengo litakalofanya kazi mbili, moja wakae wafanyakazi yaani bodi na sekretarieti na Waafrika wengine watumie jengo hilo kwa kazi ya amani na mambo mengine, kwa hiyo si jengo la taasisi peke yake ni jengo la watu wote.
“Pili jengo hilo ili lipate fedha za kutosha lipangishwe, kwa hiyo jengo mlilomo sasa ndiyo maagizo ya baba wa taifa. Ni mali ya taasisi, ni mali yenu, ni mali ya Waafrika wenzenu na Mwalimu kwa kuwa alisema Waafrika zote ni ndugu zake nadhani hata Rais Trump ni ndugu yake, jingo hili ni la amani halina mipaka,” amesema.
Aidha, akitaja ramani ya jengo hilo, Butiku amesema lina sehemu mbili moja ni ofisi ya watafiti na chuo ambacho wanakiandaa na eneo la pili ni maktaba ya nyaraka za Baba wa Taifa, vitabu na machapisho mengine na kwamba watu wote wanaruhusiwa kwenda kutazama.