Na JIMMY CHIKA
UNAUKUMBUKA wimbo maarufu wa Kila Munu ave na kwao, ulioimbwa katika lugha ya Kimakonde na mwanamuziki, Halila Tongolanga?
Maana ya maneno ya wimbo huo kwa Kiswahili ni kila mtu ana kwao.
Je unalikumbuka kundi la wanamuziki wenye vipaji vya kuimba kwa masikitiko, Bana Mwambe, lililoundwa na marehemu Tx Moshi William?
Kama unakumbuka vyote au kimoja kati ya hivyo, basi unatakiwa kufahamu kwamba muhimili mkubwa katika matukio hayo ni Halila Tongolanga ambaye hatunaye tena duniani.
Tongolanga au Mzee wa Mchichira amefariki jana katika Hospitali ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Tandahimba huko Lindi.
Msiba huu umetonesha kidonda kwa wadau wa muziki wa dansi, hii inatokana na kuzidi kupungua kwa wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi la Bana Mwambe.
Licha ya kutokuwepo kwa sauti za Moshi William na marehemu Muhidin Gurumo, kundi hilo sasa linaikosa pia sauti pekee ya Tongolanga.
Jina la mwanamuziki huyo lilipata umaarufu kutokana na kuimba zaidi kwa lugha ya Kimakonde ambayo huzungumzwa zaidi za wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na nchi jirani ya Msumbiji.
Kwa maana nyingie Tongolanga alikuwa maarufu sana nchini Msumbiji na hata kifo chake kwa mujibu wa mitandao ya kijamii, kimewagusa mashabiki wengi wa miji ya Maputo, Pemba na Msimbati.
Katika maisha yake, Tongolanga hakupenda kuajiriwa na bendi, hii ilitokana na msimamo wake wa kutaka kuimba nyimbo zenye asili ya kabila lake la Kimakonde, hivyo katika maisha yake amewahi kuyatumikia makundi mawili tu, Makondeko six band lililokuwa likimilikiwa na mwanasiasa maarufu miaka ya 1980 Dk Alex Khalid pamoja na kundi alilolianzisha yeye mwenyewe aliloendeleza jina hilo hilo la Makondeko Band.
Wanamuziki wakubwa waliowahi kusikia kazi zake walimshawishi sana kujiunga na bendi mbalimbali, mojawapo ni marehemu Moshi ambaye alipenda sana kuimba na Tongolanga, lakini misimamo yake ilimkatisha tamaa na ndipo alipompa wazo la kuunda kundi la Bana Mwambe ambalo alilikubali.
Katika kundi hilo pia walikuwepo wanamuziki Tx Moshi, Gurumo, Shukuru Majaliwa, Huruka Uvuruge, Hamza Mwanamasongi na Hussein Mtambile.
Maudhui ya kundi hili yaliangalia zaidi wanamuziki wanaojua kuimba kwa masikitiko, ndiyo hadi leo unaposikiliza nyimbo zake unapata hisia iliyo tofauti na bendi nyingine za muziki wa dansi.
Mara ya mwisho alipozungumza na mwandishi wa makala haya kiasi cha miezi sita iliyopita, alieleza mikakati yake ya kuimarisha ziara zake katika nchi ya Msumbiji.
Alipata maamuzi hayo kufuatia kukubalika kwa albam yake maarufu aliyoiita Kilambo cha Vene ambayo ilimsaidia kupata mashabiki wengi nchini humo.
Tutaendelea kuikumbuka sauti ile ya juu, 'high pitch' iliyokuwa ikisikika katika nyimbo nyingi na pia rap zake za Kimakonde zilizokuwa zikisindikiza nyimbo za kundi la Bana Mwambe.
Tunamuombea mapumziko mema Peponi- Amin.