28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge: Wadau Muswada Vyama vya Siasa njooni

ANDREW MSECHU, Dar es Salaam

Ofisi ya Bunge   Dodoma imetangaza vikao vya kamati tatu za bunge kwa ajili ya kupokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu miswada  mitano ya sheria, ukiwamo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018.

Hata hiyo, ofisi ya Bunge imechukua hatua hiyo wakati vyama 10 vikiwa vimefungua kesi Mahakama Kuu   kupinga muswada huo kupelekwa bungeni.

Kesi hiyo  ilifunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), Salim Bimani (CUF) na Joram Bashange (CUF) kwa niaba wenzao na ilianza kusikilizwa kwa hati ya dharura Januari 4, mwaka huu.

Kesi hiyo inatarajiwa kutolewa uamuzi wa awali leo   kuhusu kuzuia muswada huo kujadiliwa katika hatua zote.

Taarifa iliyotolewa   na Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge   Dodoma jana, ilisema wadau hao ambao ni wawakilishi kutoka kila chama cha siasa kilichosajiliwa, watatakiwa kutoa maoni yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, Januari 19 na 20, mwaka huu katika ukumbi namba 9 jengo kuu la utawala, baada ya kusikilziwa   maoni ya wadau wengine wa siasa Januari 17 na 18.

“Kamati zinawaalika wadau kufika na kuwasilisha maoni yao kwa lengo la kusaidia katika uchambuzi wa miswada hiyo ambayo inapatikana katika tovuti ya Bunge … maoni ya wadau yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya Posta au baruapepe,” ilisema taarifa hiyo.

Hatua hiyo  imepolekewa kwa hisia tofauti na wadau hasa viongozi wa vyama vya siasa  ambao wameeleza ipo haja ya Bunge kuonyesha heshima kwa muhimili mwingine muhimu ambao ni   Mahakama.  

Maoni ya viongozi

  Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema ofisi ya Bunge inajua vyama vyote vya siasa, isipokuwa CCM,  vimepeleka shauri hilo mahakamani kwa hati ya dharura.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo wameyaomba mahakamani, ni kuzuia muswada huo kupelekwa bungeni hadi uamuzi wa shauri hilo utakapotolewa na mahakama.

“Sasa mahakama imeshasema itatoa uamuzi wa awali Januari 14 (leo), kwa nini Bunge lisiwe na subira? Au ina maana limeshajua uamuzi utakaotolewa…kwa nini wanaita wadau wa muswada huo baada ya siku mbili baadaye?”  alisema.

Alisema hata kama mahakama itaamua kwa matakwa ya Bunge, sheria inaruhusu kukata rufaa iwapo walalamikaji watakuwa hawajaridhika.

Polepole

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema chama hicho kitaendelea kupokea maagizo ya Bunge na kitashiriki kwa ukamilifu kwa kukusanya maoni kutoka kwa wanachama kisha viongozi watawasilisha maoni hayo kwenye kamati kama ilivyoelekezwa.

Alisema katika suala hilo, wananchi waachwe wajadili bila hofu kwa kuwa wanatumia haki yao ya  demokrasia na hata waliokwenda mahakamani wametumia haki yao ya  demokrasia, kwa hiyo hicho si kuizuizi cha kuendelea  mchakato huo.

“Hata ukiwa na hofu zako unaweza pia kukimbilia mahakamani kama hao wengine walivyofanya. Lakini kimsingi hofu nyingine ni za kufikirika tu. Tuwaache wananchi na wadau wajadili kama utaratibu unavyoelekeza, pia kamati husika ifanye kazi yake kwa mujibu wa taratibu za Bunge,” alisema.

Zitto Kabwe

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema hata kama Bunge limechukua hatua hiyo, wao wataendelea mahakamani, hivyo bunge liendelee na shughuli zake.

“Meles Zenawi (Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia) aliwahi kusema tunapigana wakati tunaongea na tunaongea wakati tunapigana.

“Tutaendeela na shughuli za Bunge wakati tupo mahakamani, tutaendelea na kesi wakati tupo bungeni. Sisi tuna imani na mahakama na tunaamini itatenda haki,” alisema.

Miswada mingine

 Kuhusu miswada mingine inayotarajiwa kujadiliwa na kamati, taarifa hiyo ya Bunge ilieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji    itapokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa mwaka 2018.

“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, itapokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini wa mwaka 2018.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, itapokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles