26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge na mchakato wa kujinyima uwepo wake

Bungeni-DodomaWakati wa uchaguzi, wabunge hurandaranda kila kona ya nchi kuomba kura. Ahadi ni kuwa watakapopewa kura na kuchaguliwa na wananchi kuingia bungeni kazi kubwa itakuwa ni kutetea haki za wananchi. Wananchi wanaamini katika ahadi hizo, wanatoa kura zao.

Wakifika bungeni, wabunge wanakaa chini ya vyama vyao, miongozo inatolewa na mmoja unasema, “Hapa ni kutetea maslahi ya chama… chama kikishindwa dhidi ya wapinzani mjue mmeshindwa…” Mimi sielewi nini maana ya aibu ya kushindwa hoja bungeni, nilidhani hoja ni kwa ajili ya kuipatia mwongozo Serikali sio kwa ajili ya kuwafanya walioianzisha waonekane wameshindwa na kuwa Serikali inapokiri na kukubaliana na hoja ya mbunge na hasa akitoka upinzani, basi chama kimeshindwa… sijaelewa! Lakini kuna wabunge wa upande wa wanaoogopa kushindwa na wanaodhani walichaguliwa kutetea maslahi ya taifa, yaani maslahi ambayo wananchi waliahidiwa wakati ule wa uchaguzi….Wanaambiwa watulie kwanza. Miongozo inaonyesha zile zilikuwa ahadi za kupatia kura, kinachofanyika wakati wa kupiga kura sio kile kile kinachofanyika wakati Bunge limeundwa.

Msingi wa Bunge ni kuisimamia Serikali ili iweze kupanga, kuamua na kutekeleza sera au sheria au mipango ya maendeleo kwa faida ya wananchi. Kuwa kila kinachofikiriwa na Serikali, mikataba, miradi na kadhalika ni kwa faida ya Taifa, wananchi. Na sio chama! Bunge ni mhimili unaojitegemea kwa msingi huo, ingawa kuna kasoro kadhaa katika kuufanya mhimili huo! Moja ya kasoro hiyo ni kuwa baadhi ya mawaziri wanatokana na wabunge wa kuchaguliwa na kukubali kwao kuteuliwa kuwa mawaziri, ili waitetee Serikali, badala ya kutetea wananchi wapiga kura, kama walivyoahidi wakati wa uchaguzi ni usaliti! Lakini kasoro nyingine ni kuwa yule ambaye anatakiwa kusimamiwa, Serikali, ndiye anayelipa mshahara na maslahi mengine na huyu anatumia nguvu hiyo ya fedha kuwatishia nyau wabunge. Hizi ni kasoro ambazo najua tunaweza kuzirekebisha kwa kuimarisha vifungu vya sheria.

Lakini kuwa na nguvu ya fedha kunatokana na wabunge kuisimamia Serikali ili ikusanye fedha na sio kuwa wakishakusanya fedha watumie nguvu hiyo kuwabana wabunge. Lakini hili, hata hivyo, sijawa na ushahidi kuwa linafanyika, linalofanyika ni lile ambalo wabunge wenyewe wanaamua kuwa wana Serikali badala ya kubakia wabunge, na ndicho tulichodhani watakuwa wakati wa uchaguzi.

Kasoro ya siasa za vyama vingi hapa Tanzania ni kudhani kuwa Bunge ni mahali pa kulinda Serikali ya chama. Serikali ya chama kwa kweli! Chama kikiunda Serikali basi lazima kitetewe, kwa uzuri na uozo. Tumeshuhudia uteteaji huo katika kila Bunge na matokeo ya uteteaji huo ni haya madudu ambayo CAG anayaweka wazi, wizi, wizi, wizi, wizi, katika kila nyumba ya Serikali ambayo chama imekuwa ikiitetea. Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita Serikali imepotea, matrilion za shilingi, fedha za umma ambazo wabunge walitakiwa kuhakikisha haziibiwi, lakini hilo limetokea kwa sababu wabunge wanaambizana, “Ukisikia habari ya wizi ndani ya Serikali ya chama hiki unatakiwa unyamaze na useme hakuna kitu kama hicho! Na ikiwezekana basi hata ushahidi unaotolewa kuthibitisha hoja za wanaoiumbua Serikali sema ni za uongo. Ukishindwa kabisa fanyeni vurugu ili chama cha upinzani watoke nje ya Bunge na wakitoka nje kwa hasira ya mkizi, mtakuwa sasa mnatumia muda wote kuwasema, kuwatusi, kuwasimanga na kuhakikisha hoja inazimwa… na tutapiga kura kupinga hoja yao… au kuunga mkono hoja ya Serikali.

Lakini katika mikakati hiyo hakuna anayetabiri nini CAG atavumbua katika ukaguzi ujao, ingawa najua kuwa CAG anafanya hivyo kama sala tu, kila Ijumaa tunaenda msikitini… tunasali.. tunaonywa juu ya hatari ya kufanya dhambi,  tunasikiliza, tunarudia tena kufanya dhambi… Ijumaa nyingine tunaenda tena kusikiliza mawaidha yanayotuonya hatari ya kufanya dhambi, lakini tunarudi nyumbani tukipanga kufanya dhambi tena na tena!

Ndiyo ilivyo kwa CAG, kila mwaka anatumia fedha nyingi kufanya kazi yake, anachapisha matabu makubwa makubwa, lakini ni kama mahubiri yale ya Ijumaa kwa wabunge… Amefanya kazi yake, kwani si amelipwa mshahara wa kuhalalisha kazi yake? Hapa bungeni mambo ni yale yale, kutetea sSerikali ya chama chetu. Na pengine tufikirie namna ya kufanya taarifa za CAG kuwa siri, ziwe mali za Serikali tu, ili wananchi wasijue udhaifu wa Serikali ya chama chetu… najua kuna wakati lilifanyika, lakini namshukuru, John Magufuli kwa kulipindua hilo.

Kinachonisikitisha zaidi ni kuona wabunge vijana… wabunge watoto.. kwa uwezo wa kufikiri na uzoefu wao wa siasa… nao wanaiga misemo ya kuzuia Bunge lisiwe mhimili huru. Nasoma kwenye magazeti, naambiwa mbunge aliyeiingia ndani ya Bunge kwa mara ya kwanza akikariri kuwa Bunge kuonyeshwa “live” ni kujionyesha kwa wananchi, na mbunge mwingine wa umri huo naye anapokea kinasa sauti na anasema hayo hayo… Spika anatabasamu, wabunge wanaunga mkono, tunawafundisha nini wabunge hawa ambao ndio wameanza safari yao ya kisiasa na mbele ya safari wataweza kushika nafasi ya juu… kuwa wewe zungumza tu ili mradi hilo ni kwa ajili ya kuilinda Serikali ya chama chako.

Wabunge waliahidi kuwa wakifika bungeni watalinda haki za wapiga kura na moja ya haki zao ni kupata taarifa na habari kwa wakati. Na Bunge ni moja ya chanzo hicho cha habari ambazo wananchi wanazitaka… lakini tunaingia bungeni tunasema kuwa kuweka “live” ni kuwakuza wabunge wanaotaka wawe wanaonekana kama ‘Stage showers… Serikali inafurahia kwa sababu wanajua sasa wabunge wamejibadilisha, bila kushurutishwa, kutoka kundi la mhimili wa kuisimamia Serikali, kuwa kundi la mhimili wa kuwa sehemu ya Serikali. Serikali huendeshwa kwa kutaka mambo yake yasiyote nje, isipokuwa yale wanayoyataka na Bunge limeamua kuwa litajiendesha kwa kuwa na mambo ambayo hayatatoka nje na wananchi wasisikilize, wasiwaone wabunge wakibishana, wakitetea hoja na kulinda hoja zao. Wananchi hawana haki hiyo tena, wananchi ni mhimili, ngazi yaani walishapandiwa wakati wa kupiga kura. Hawana haki tena.

Nimeandika mahali fulani kuwa kazi ya Bunge ni kuweka Serikali sawa, na sio kuwatetea katika mambo ambayo mtu unaona kabisa kuwa ni uozo. Bunge litakuwa limejinyang’anya uhalali wake kama wataona kuwa kazi yao ni kulinda Serikali! Ni afadhali nisiwe na Bunge, kuliko kuwa na Bunge hili ambalo mikakati yake ni kutetea maslahi ya chama, na kukubali kuwa sehemu ya Serikali!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles