33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE LASUBIRI HUKUMU WABUNGE NANE CUF

GABRIEL MUSHI NA ESTHER MBUSSI, DODOMA

BUNGE limesema linasubiri hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya wabunge wanane wa viti maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF), kisha litathmini na kutangaza kwa umma hatua za kuchukua.

Kauli ya Bunge imekuja baada ya mahakama hiyo kuzuia wabunge hao na madiwani wawili wa viti maalumu kujadiliwa na kuvuliwa uanachama hadi uamuzi wa kesi yao ya msingi utakapotolewa.

Uamuzi huo ulitolewa juzi na Jaji Lugano Mwandambo, kutokana na maombi yaliyofunguliwa na waliokuwa wabunge wanane na madiwani wawili wa viti maalumu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, alisema wanasubiri hukumu ya mahakama iwafikie ndipo wajue hatua za kuchukua.

“Hiyo hukumu sijaiona, hadi ionekane tujue hatua za kuchukua. Mahakama ndiyo ina jukumu la kusambaza hiyo hukumu hivyo tunasubiri,” alisema.

Pia MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Spika wa Bunge, Job Ndugai, lakini halikumpata na lilipozungumza na Katibu wake, Said Yakubu, alisema Spika atalitolea ufafanuzi suala hilo kesho (Jumatatu).

“Kwanza tunasubiri hiyo hukumu na baada ya hapo wanasheria wetu watakaa na kuichambua ndipo Spika atakapoweza kulitolea ufafanuzi.

“Kwa hiyo tusubiri hadi Jumatatu kwa kuwa ni siku ya kazi, hivyo hukumu inaweza kutufikia na Spika akapata muda wa kuipitia na kutolea ufafanuzi,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alisema hukumu hiyo iliyotolewa haina athari yoyote dhidi ya uamuzi wa awali uliotolewa na vikao vya chama hicho.

Sakaya alisema hukumu hiyo ingekuwa na athari kama ingetaka vikao vya chama vilivyowavua uanachama na ubunge wao virudiwe.

“Wale walipeleka kesi wakati hawajajadiliwa na uamuzi haujatoka, walitaka waweke zuio ili wasijadiliwe. Lakini hilo halikufanyika kwa muda mwafaka sasa wamekuja kufanya hivyo wakati vikao vimeshakaa na kutoa uamuzi.

“Kwa hiyo huwezi kuzuia kitu ambacho kimeshafanyika, kingekuwa hakijafanyika hapo ingewasaidia kwa hiyo sasa haina impact yoyote. Hivyo uamuzi uliotoka hauwezi kurudi nyuma,” alisema.

Pia alisema Mahakama na Bunge ni mihimili miwili tofauti hivyo mahakama haiwezi kulilazimisha Bunge kurudishia wanachama hao ubunge wao.

“Bunge lilishafanya uamuzi halirudi nyuma na mahakama haiwezi kulielekeza Bunge lifanye hiki au kile. Kama wakati ule walivyokuwa wanaitwa wakajadiliwe wao badala ya kwenda kwenye kikao cha maadili wakakimbilia mahakamani, sasa hukumu inatoka wakati vikao vya chama vimeshamaliza. Kwa hiyo haina impact katika kitu ambacho kimeshafanyika. “Labda mahakama ingesema vikao ambavyo vimeshafanyika virejee hapo sawa,” alisema.

Wabunge na madiwani waliofukuzwa uanachama wa CUF ni Miza Bakari Haji, Saverina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwasa, Raisa Abdallah Mussa, Riziki Shahri Ng’wari, Hadija Salum Ally al Qassim, Halima Ali Mohamed, Saumu Heri Sakala na madiwani viti maalumu, Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madibi.

Huku nafasi zao zilijazwa na Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Azizi Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainab Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Aporinary Kahigi, Nuru Awadhi Bafadhili ambao Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alipeleka majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles