Bunge lapitisha sheria kubana wanaotuma picha, video za ajali

0
916

ANDREW MSECHU – DODOMA

BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba sita wa mwaka 2019, yanayohusisha kuweka adhabu kwa watu wanaotumia au kusambaza picha za maiti au wahanga wa ajali na kubadilisha muundo na majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA).

Akiwasilisha muswada huo uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho katika sheria tisa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema mabadiliko hayo yanahusisha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 iliyotungwa mwaka 1930 kwa lengo la la kuainisha adhabu kwa makosa mbalimbali.

Alisema tangu kutungwa kwa sheria hiyo, imerekebishwa mara 67 kupitia sheria mbalimbali na marekebisho ya sasa yanalenga kuongeza adhabu ya faini kwa makosa chini ya kifungu cha 29, ili kuondoa adhabu zilizopitwa na wakati kutokana na hali ilivyo sasa.

“Kifungu kipya cha 162 kinapendekezwa kuongezwa ili kutoa adhabu kwa watu wanaotumia na kusambaza picha au video za maiti, waathirika wa majanga na matukio ya kutisha yanayohatarisha amani au kuingilia utu wa mtu,” alisema.

Katika mabadiliko hayo, adhabu zimebadilishwa katika Ibara ya 29 kutoka Sh 100 iliyokuwa ikisomeka awali na kufikia Sh 50,000 kwa makosa tofauti ambapo watuhumiwa wanaweza kutozwa hadi zaidi ya Sh 1,000,000.

SSRA YABADILISHWA

Profesa Kilangi alisema katika mabadiliko, Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi za Jamii Sura ya 135, iliyotungwa na Bunge mwaka 2008 imesharekebishwa mara tatu kupitia Sheria Namba 5 ya 2012, Sheria na 10 ya 2013, na Sheria Na 2 ya 2018.

Alisema katika muswada aliouwasilisha jana, marekebisho yalilenga kuifuta Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii na kuhamisha jukumu la usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenda kwenye divisheni inayowajibika kwa masuala ya hifadhi ya jamii.

“Aidha, muundo wa kitaasisi uliopo sasa kwenye Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), Sura ya 135 unapendekezwa kufutwa na badala yake majukumu ya usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kuhamishiwa kwenye divisheni hiyo,” alisema.

Profesa Kilangi alisema eneo la usimamizi wa masuala ya fedha na uwekezaji wa mifuko litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania kama ilivyo sasa.

Alisema kifungu cha pili cha sheria hiyo kitabadilishwa ili kuendana na mfumo wa utawala unaopendekezwa, na kifungu cha nne kinachoanzisha SSRA kimependekezwa kufutwa na kuipa divisheni hiyo mpya mamlaka ya kusimamia sekta ya hifadhi ya jamii.

Profesa Kilangi alisema vifungu vingine vinane vinavyoanzisha bodi, kuweka majukumu ya bodi na masuala yanayohusu watumishi wa mamlaka, vitafutwa, pia vifungu vingine vinne vitarekebishwa ili kuondoa rejea zote za neno “Mamlaka” na badala yake kuweka rejea ya neno “Divisheni”, mabadiliko yanayoendana na dhumuni la kuifuta mamlaka na bodi.

“Pia, mabadiliko ya kifungu cha 44 yanalenga kuondoa muda wa uwasilishaji malalamiko ya mnufaika wa fao. Lengo la marekebisho haya ni kutoa haki na fursa kwa mnufaika kuwasilisha malalamiko muda wowote. Haki hiyo ingepotea ikiwa mnufaika atawekewa ukomo wa muda wa uwasilishaji wa malalamiko,” alisema.

Profesa Kilangi alisema kuwa vifungu viwili, yaani cha 57 na 58 vinavyohusu kinga ya wajumbe wa bodi na mamlaka kutunga kanuni vinapendekezwa kufutwa kwa kuwa havitumiki tena katika mfumo wa utawala unaopendekezwa katika sekta.

“Sehemu ya nane ya sheria inayohusu masuala ya fedha inapendekezwa kufutwa. Sehemu ya kumi inayohusu masharti ya uhifadhi inapendekezwa kuongezwa katika sheria hii. Dhumuni la marekebisho ni kuweka utaratibu mzuri kufuatia mabadiliko ya kitaasisi yanayopendekezwa,” alisisitiza.

SHERIA YA UTUMISHI WA UMMA

Profesa Kilangi alisema katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 marekebisho yanalenga kumwezesha Katibu Mkuu Kiongozi kuwa na mamlaka ya jumla ya uhamisho wa watumishi wa umma, yakilenga kuboresha masharti ya uhamisho wa watumishi katika utumishi wa umma.

Alieleza kuwa mapendekezo hayo yanahusisha pia kumjumuisha Katibu wa Bunge kwenye orodha ya watumishi wa umma wanaopokea mafao maalumu, kutokana na Sheria ya Hifadhi ya Jamii katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2018 kumtambua kuwa miongoni mwa wanufaika wa mafao maalumu, lakini utambuzi huo ulikuwa haujafanyika kwenye Sheria ya Utumishi wa Umma.

“Kifungu cha 27 kinaongezwa ili kumpa Katibu Mkuu Kiongozi mamlaka ya kumsamehe mtumishi yeyote wa umma kutotimiza vigezo au masharti ya kupata mafao ya pensheni.

“Lengo ni kwamba ikiwa kuna mtumishi ambaye baadhi ya nyaraka anazopaswa kuambatanisha wakati wa kufanya maombi ya mafao yake yana upungufu wa viambatanisho, Katibu Mkuu Kiongozi atakuwa na uwezo wa kutoa maelekezo ya mtumishi huyo kupata mafao yake bila vigezo au masharti hayo kutimia,” alisema.

Sheria nyingine zilizowasilishwa kwa marekebisho na kupitishwa katika muswada huo ni Sheria ya Mamlaka ya Nishati na Huduma za Maji Sura ya 414, Sheria ya Vivuko Sura ya 173 na Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura ya Nne.

Nyingine ni Sheria ya Usafirishaji Majini Sura ya 165, Sheria ya Tafsiri ya Sheria Mbalimbali Sura ya Kwanza na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148.

MAONI YA KAMATI

Akitoa maoni ya kamati kuhusu Mabadilio ya Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Andrew Chenge (CCM), alisema kamati yake inahitaji kuwepo uangalizi wa namna ya kutoa adhabu, kwa kuzingatia maombi ya msingi.

Chenge alisema ni vyema kuweka wazi madhumuni ya kuruhusu upigaji picha kwa baadhi ya matukio kama vile kwenye mazishi yaliyoruhusiwa na ndugu wa marehemu, upigaji picha kwa ajili ya kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama au kwa ajili ya matumizi ya ushahidi kielektroniki.

“Lengo la mapendekezo ni kubainisha matukio yanayoweza kuruhusiwa kupiga picha. Aidha ni kwa kuzingatia ukweli kwamba maudhui ya kifungu kinachopendekezwa yanaweza kuondoa uhuru wa watu binafsi pale panapokuwa na matukio binafsi ikiwemo misiba, kuingilia uhuru wa kazi za kawaida za wanahabari pamoja na masuala ya matumizi ya picha kama ushahidi wa kielektroniki,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here