30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

BUNGE LAMWITA MAKONDA

MAREGESI PAUL, DODOMA

BUNGE limeiagiza ofisi ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, imtake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ajieleze juu ya kauli za kashfa anazodaiwa kuzitoa dhidi ya wabunge.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alipokuwa akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM)

“Nimepokea mwongozo wa mheshimiwa Abdallah Ulega na nimemwelewa ingawa sijayasikia yale maneno yanayodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Lakini, kwa kiongozi makini na anayefahamu kuongoza na anayejua shughuri za Bunge, niseme moja tu, kwamba yule aliyeathirika na kauli hizo, awasilishe malalamiko yake kwa Spika na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge itajadili.

“Suala hili sitamfikishia Waziri Mkuu na wala sitahitaji aombe radhi. Lakini, kitu chochote kinachoonekana kudharau au kushusha heshima ya Bunge, hakikubariki kwa sababu Bunge ni moja ya mihimili mitatu katika nchi yetu.

“Unaweza ukawa hunipendi mimi, lakini Bunge lazima liheshimiwe. Kwa hiyo, ili ithibitike ameyasema wapi na ameyasema lini, naagiza Ofisi ya Katibu wa Bunge, wamtake RC wa Dar es Salaam, alete maelezo yake juu ya tuhuma hizi kisha Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, ijadili maelezo hayo,” alisema Chenge.

Awali, katika maelezo yake, Ulega alisema kauli ya kulidharau Bunge haiwezi kukubaliwa kwa sababu nao wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya dawa za kulevya kama anavyofanya mkuu huyo wa mkoa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amezungumza na vyombo vya habari na ametoa lugha za dharau kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba kazi yetu sisi wabunge ni kulala.

“Mheshimiwa mwenyekiti, sisi wabunge tuko mstari wa mbele kupambana na kumsaidia Rais Magufuli katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

“Ikumbukwe kwamba, hiyo sheria ya dawa za kulevya, imetungwa na Bunge hili na kama haitoshi, siku mheshimiwa rais alipokuja kuzindua Bunge hili, tulimpigia makofi aliposema atapambana na dawa za kulevya.

“Mheshimiwa mwenyekiti, Makonda ni mdogo wangu, ni kijana mwenzangu na ni rafiki yangu, lakini Bunge  lazima liendelee kuheshimika kwa namna yoyote ile.

“Kwa hiyo, naomba kutoa hoja zifuatazo kwa sababu sisi tuko mstari wa mbele kumsaidia mheshimiwa rais katika vita hii.

“Kwanza kabisa, naomba waziri mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali, amchukulie hatua ili kulinda heshima ya Bunge, au Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ichukue hatua kupitia Bunge hili au aombe radhi kwa alichokisema dhidi ya wabunge,” alisema Ulega na kushangiliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles