NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
OFISI ya Bunge imebadilisha ratiba ya Kamati za Bunge kutokana na kuwapo kwa mabadiliko ya tarehe ya kupokea mapendekezo ya mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano inaeleza kuwa kuelekea mkutano wa tatu wa Bunge (mkutano wa Bajeti) ofisi hiyo imeamua kufanya mabadiliko ya ratiba ili kuendana na masharti ya Kanuni za Bunge kuhusu shughuli hizo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa shughuli za kamati itakuwa Kamati ya Kudumu ya Kisekta itakutana Machi 29 hadi Aprili 4, mwaka huu na zitatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi.
“Mwaka wa fedha wa 2015/2016 kwa mujibu wa kanuni ya 98 (1) ya kanuni za Bunge hapo awali kazi hii ilipangwa kufanyika Machi 3 hadi Aprili 5, mwaka huu,” ilieleza taarifa hiyo.
Pia ilieleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 96 ya Kanuni za Bunge, Serikali itawasilisha dondoo na randama za vitabu vya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 ambapo awali kazi hiyo ilipangwa kufanyika Machi 29, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Aprili 6, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni ya 97(1)-(2) ya Kanuni za Bunge kutakuwa na mkutano wa wabunge wote na Serikali itawasilisha mapendekezo ya mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 kazi iliyopangwa kufanyika Machi 30, mwaka huu.
Pia Aprili 7 hadi 15, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni ya 98 (2) ya Kanuni za Bunge, kwa kipindi cha siku tisa, Kamati za Kudumu za Kisekta zitachambua taarifa za utekelezaji wa bajeti za wizara zinazosimamiwa na kamati hizo.
Katika kipindi hicho, Kamati ya Bajeti itafanya uchambuzi wa mapendekezo ya mpango na kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 kazi ambayo awali ingefanywa Machi 31 hadi Aprili 6, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema kwa mujibu wa Kanuni ya 98(3) ya Kanuni za Bunge Aprili 15, mwaka huu kutakuwa na kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti ili kujadili mambo muhimu yaliyojitokeza katika Kamati za Kisekta.
Katika hatua nyingine, Aprili 16 na 17, mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali wabunge wataelekea Dodoma tayari kwa Shughuli za Mkutano wa Tatu wa Bunge na watajadili utekelezaji wa bajeti za wizara mbalimbali.