25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge la tunga sheria kubana wale wa ‘nitumie kwenye namba hii’

ANDREW MSECHU-Dodoma

BUNGE limepitisha Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Sura ya 306, ambao utawabana wanaotumia simu kufanya utapeli.

Sheria hiyo ni miongoni mwa sheria saba zilizowasilishwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof Adelardus Kilangi jana, kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba Tano wa mwaka 2019.

Akiwasilisha mudwada huo, Kilangi alisema sheria hiyo iliyotungwa na Bunge mwaka 2010 ililenga kushughulikia masuala ya mawasiliano ya kielektroniki, kuweka mfumo wa kudhibiti na kusimamia watoa huduma katika sekta ya mawasiliano ya kielektroniki na posta.

 “Marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuimarisha udhibiti wa matumizi ya huduma za mawasiliano ya kielektroniki, kudhibiti watumiaji wa mawasiliano wenye lengo la kurubuni watu kwa kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina tofauti na majina yao halisi.

“Pia umenuia kuimarisha usalama wa watumiaji wa huduma za kimtandao na kupunguza wimbi la uhalifu na kuhuisha sheria hii ili iendane na hali ya sasa ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole,” alisema.

Kwa upande wa muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Baraza la Taifa la Mitihani Sura ya 107, mabadilio yanayohusu kupanua wigo wa baraza hilo kwenye upimaji wa wanafunzi na kuongeza aina mpya ya makosa na adhabu zitakazotolewa kutokana na ukiukwaji wa taratibu za mitihani.

Prof Kilangi alisema kifungu cha pili cha sheria hiyo iliyotungwa na Bunge mwaka 1973 kinarekebishwa kwa madhumuni ya kufafanua baadhi ya maneno na misamiati inayotumika chini ya sheria hiyo.

Alisema marekebisho yanafanywa katika kifungu cha 11 ili kuipa mamlaka Kamati ya Mitihani kufanya uchunguzi kwa suala lolote linalohusiana na ukiukwaji wa masuala yanayohusu mitihani.

 “Sehemu hii pia inapendekeza kuongeza sehemu ya Tatu ‘A’ mpya kwa lengo la kuongeza sifa za uadilifu, uwajibikaji na uaminifu kwa maofisa wanaojihusisha na masuala yanayohusiana na mitihani.

“Marekebisho haya yanalenga kupambana na kukua kwa teknolojia ndani ya jamii ambapo inaweza kusababisha uvujishaji wa mitihani. Aidha inaongeza aina mpya ya makosa yanayohusiana na mitihani na kuongeza adhabu zitakazotolewa kutokana na makosa hayo,” alisema.

Alisema mabadiliko ya kifungu cha 20, yanalenga kurahisisha utekelezaji wa maelekezo ya waziri na mapendekezo ya kifungu cha 25 yanalenga kutambulika kisheria uanzishwaji wa nafasi za maofisa elimu wa mikoa watakaokuwa wawakilishi wa baraza hilo katika mikoa husika.

Sheria nyingine ziliorekebishwa ni Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Milipuko Sura ya 223, Sheria ya baraza la Sanaa la Taifa Sura ya 204,  Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa Sura ya 61, Sheria ya Vipimo Sura ya 340 na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Sura ya 283.

Katika Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Milipuko Sura ya 223, iliyotungwa mwaka 2015, Prof Kilangi alisema mabadiliko yatafanywa kwa kuweka kifungu kipya cha 21A kinacholenga kuharamisha uingizaji ndani ya nchi, utengenezaji au umiliki wa fataki bila ridhaa ya Inspekta Jenerali wa Polisi.

Prof Kialngi alisema kuwa katika Sheria ya Baraza la Taifa la Sanaa Sura ya 204, inapendekezwa kuongeza kifungu kipya cha 3(4) kwa lengo la kuanzisha kamati za sanaa za mikoa na wilaya na namna ya uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo.

Akizungumzia Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa Sura ya 61, Prof Kilangi alisema marekebisho yanalenga kurekebisha tafsiri ya neno ‘Vyombo vya Ulinzi na Usalama’ kwa lengo la kuzitambua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kuwa miongoni mwa vyombo hivyo.

Ends

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles