MKUTANO wa pili wa Bunge la 11 unaanza leo mjini hapa, huku wabunge wakitengewa siku tatu kujadili hotuba ya Rais, Dk. John Magufuli, aliyoitoa bungeni Novemba 20 mwaka jana.
Shughuli nyingine zilizopangwa kufanyika leo mbali ya maswali ya kawaida ni uchaguzi wa wenyeviti wa Bunge na kiapo cha uaminifu kwa wabunge wapya 11.
Akizungumzia mjadala wa hotuba ya rais, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, alisema kila mbunge atachangia hotuba hiyo kwa dakika 10, badala ya 15 zilizopo katika kanuni.
“Bunge hili lina wabunge 380, kwa kuwa ni siku tatu wabunge wote hawatapata nafasi ya kuchangia, hivyo kesho (leo) itawasilishwa hoja ya kutengua kanuni kupunguza muda wa kuchangia.
“Lakini pia kwa kuzingatia umuhimu wa hotuba hiyo, badala ya kipindi cha jioni kuanza saa 11.00, kitaanza saa 10 jioni kuhakikisha wabunge wengi wanapata fursa ya kuchangia,” alisema.
Owen alisema hatua hiyo itawezesha kuongeza idadi ya wachangiaji kutoka 63 ambao wangepatikana kwa utaratibu wa kawaida hadi wachangiaji 114, baada ya kanuni husika kutengeuliwa.
Itakumbukwa wakati akizindua Bunge Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alizungumzia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwaomba Watanzania kumwombea kwa Mungu wakati akitumbua majipu kwa kukabiliana na watendaji wabadhirifu na ufujaji wa fedha za umma.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli pia alionyesha masikitiko yake kutokana na kukosekana kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuahidi kupunguza safari za vigogo nje ya nchi ambazo hazina tija kwa taifa.
Kiapo
Shughuli nyingine itakayofanyika leo ni kiapo cha uaminifu ambako wabunge 11 ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na Rais Magufuli, baada ya kumalizika kwa mkutano wa kwanza wa Bunge.
Wabunge wateule watakaoapishwa leo na majimbo yao katika mabano ni Goodluck Mlinga (Ulanga-CCM), Shaaban Shekilindi (Lushoto-CCM), Godbless Lema (Arusha Mjini-Chadema) na Omar Kigoda (Handeni Mjini-CCM).
Wengine ni Deogratias Ngalawa (Ludewa- CCM), Rashid Chuachua (Masasi-CCM), Dk. Abdallah Posi (Kuteuliwa), Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Kuteuliwa), Profesa Joyce Ndalichako (Kuteuliwa), Dk. Philip Mpango (Kuteuliwa) na Dk. Augustine Mahiga (Kuteuliwa).
Kwa mujibu wa Owen, wabunge wote wanatarajiwa kuapishwa leo ispokuwa Profesa Ndalichako ambaye ameomba kuapa kesho na Dk. Mahiga Februari 2.
Wenyeviti
Shughuli nyingine itakayofanywa leo ni uchaguzi wa wenyeviti wa Bunge baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge juzi kupitisha majina matatu ya wabunge watakaowania nafasi hiyo.
Waliopitishwa ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Mbunge mwingine wa Viti Maalumu, Najima Murtaza Giga, wote kutoka CCM.
Mpango wa Taifa
Januari 29 mwaka huu baada ya kipindi cha maswali ya kawaida, Serikali itawasilisha Mpango wa Taifa wa Miaka mitano ambao utajadiliwa kwa siku mbili kabla ya Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango itakayoketi kwa siku nne kuanzia Februari Mosi, 2016.
Yatakayotikisa
Katika mkutano huo wa Bunge la 11 unaoanza leo mjini Dodoma, hoja kadhaa zinatarajiwa kuibuka likiwamo suala la Muundo wa Kamati za Bunge, uchaguzi wa marudio Zanzibar, agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzuia mikutano kwa vyama vya upinzani.
Mbali na hoja hiyo masuala ya uchaguzi wa meya Dar es Salaam, Akaunti ya Tegeta Escrow, Hotuba ya Rais Magufuli, Bomoabomoa, Sera ya elimu bure, Katiba Mpya na maagizo ya mawaziri, nayo yanatarajiwa kujadiliwa kwa undani.
Uchaguzi
Kabla ya Bunge kuahirishwa Februari 5 mwaka huu, kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe wa tume mbalimbali, ikiwamo uchaguzi wa wajumbe saba wa Tume ya Utumishi wa Bunge.
Nyingine ni uchaguzi wa wajumbe watano wa Bunge la Afrika (PAP) na wajumbe watano wa Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF).
Nyingine ni uchaguzi wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) na wajumbe watano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).