30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE KUJADILI HALI YA CHAKULA

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


MKUTANO  wa Sita wa Bunge unatarajiwa kuanza leo mjini hapa, huku mjadala mzito kuhusu hali ya chakula nchini ukitarajiwa kutawala.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mkuu wa  Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya alisema mkutano huo unatarajiwa kumalizika Februari 10, mwaka huu ambapo kutakua na kauli mbili za Serikali zitakazowasilishwa na mawaziri.

Mwandumbya alizitaja kauli hizo, kuwa ni kuhusu hali ya chakula, deni la Taifa na hali ya uchumi. Deni hilo kwa sasa linakadiriwa limefika Sh trilioni 40

“Kauli mbili za mawaziri zitawasilishwa kesho (leo), ni kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula na hali ya uchumi,’’ alisema.

Pia alisema mkutano huo, utakuwa ni mahususi kwa ajili ya kupokea taarifa za kamati za kudumu za Bunge ambapo  Kamati 14 za kisekta zitawasilisha taarifa zake.

“Mkutano huu, ni mahususi kwa ajili ya kupokea taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge ambapo Kamati 14 za kisekta zitawasilisha taarifa zake bungeni katika kipindi hiki,’’ alisema.

Owen alisema pia kutakuwa na kiapo cha uaminifu kwa wabunge wanne, huku watatu wakiwa ni wa kuteuliwa na Rais  Dk. John Magufuli  na mmoja wa kuchaguliwa.

Aliwataja wabunge walioteuliwa na Rais Dk. Magufuli, kuwa ni Abdallah Bulembo, Profesa Palamagamba  Kabudi  na Anne Malecela, huku Ali Juma Ali akichaguliwa na wananchi katika Jimbo la Dimani, Zanzibar.

Alisema katika mkutano huo, maswali ya kawaida 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa.

“Kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge wastani wa maswali 16 ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu yataulizwa na kujibiwa siku za Alhamisi,'' alisema.

“Katika Mkutano waTano wa Bunge uliomalizika Novemba, 2016 Miswada mitatu ya sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza bungeni na kupelekwa kwenye kamati husika ili ifanyiwe kazi,’’alisema.

Aliitaja miswada hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa kwa mara ya pili, kuwa ni  ule wa Sheria ya Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa mwaka, 2016 (The Medical, Dential and Allied Health Professionals Bill 2016).

Mwingine, ni wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016) na Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.4) wa mwaka 2016.

 

RAIS MAGUFULI

Akiwa mkoani Simiyu wakati wa ziara ya kikazi, Rais Dk. John Magufuli alisema Taifa halikabiliwi na njaa na kuwa taarifa hizo ni za uzushi, huku akisema  yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za njaa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

“Wapo wafanyabiashara wengine wachache waliokuwa wamezoea panapotokea matatizo kidogo tu ya ukame, wanatumia vyombo vya habari ikiwa pamoja na magazeti wanayoyaamini wao sio magazeti yote.

“Pamoja na baadhi ya wanasiasa kuzungumza Tanzania kuna njaa, anayejua njaa ni Rais na sio gazeti fulani, mimi ndiyo niliyepewa dhamana ya kuwaongoza Watanzania,” alisema.

 

Waziri Mkuu

Januari 16, mwaka huu akiwa mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema nchi haijakumbwa na baa la njaa na aliwataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.

Alisema Serikali ndiyo yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula.

 “Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula.

“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini, msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” alisema Majaliwa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles