TEHRAN, IRAN
KUNDI la watu wenye silaha limelishambulia Bunge la Iran na jengo lenye kaburi la mwasisi wa mapinduzi ya Kiislamu ya taifa hilo na kuua watu 12 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Kwa mujibu ya mashirika ya habari ya ISNA na Fars, washambuliaji kadhaa waliingia bungeni kupitia lango la Kaskazini na mmoja wa waliojeruhiwa ni mlinzi wa Bunge.
Mbunge mmoja ameliambia Shirika la Habari la IRIB kuwa jumla ya washambuliaji wanne waliingia bungeni wakiwa wamebeba bunduki na bastola.
Aidha katika shambulio jingine, mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliingia katika jengo lenye kaburi la mwanzilishi wa mapinduzi ya Iran, Ruhollah Khomeini, akafyatua risasi kadhaa kabla ya kujilipua mwenyewe.
ISNA limesema walioshambulia Bunge wamezingirwa, lakini bado hawajakamatwa.
Kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) limedai kuhusika na mashambulizi hayo.