29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

BUNGE EALA KUZIPATANISHA RWANDA, BURUNDI?

Na MARKUS MPANGALA

UCHAGUZI wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ulikuwa na shamrashamra, ushindani na matokeo yakaonyesha sura mpya zikiibuka na ushindi.

Kutokana na umuhimu wa EALA kwa wananchi wa Afrika Mashariki, tunakuletea mfululizo wa makala za uchambuzi wa kina juu ya changamoto zinazolikabili Bunge jipya katika nyanja ya demokrasia, diplomasia, uchumi na biashara, ugaidi, ulinzi na usalama.

Kwa kuanzia, tunaangazia eneo la diplomasia kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda na Burundi. Endelea…

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo ni mbaya mno. Unatia doa katika mchakato mzima wa Jumuiya hiyo kwenye masuala ya uchumi, ulinzi na usalama pamoja na mapambano dhidi ya ugaidi na kutokomeza vikundi vya waasi.

Ubaya huo unajidhihirisha kutokana na hali halisi inayoendelea baina ya nchi hizo, ambazo zinategemewa kuwa chachu ya amani, demokrasia, ulinzi na usalama pamoja na ujirani mwema.

Nchi zote za Jumuiya hiyo zimekuwa kwenye harakati nyingi za kuimarisha demokrasia, uchumi na uhusiano mzuri baina yao kwa lengo la kuchochea maendeleo kwa maslahi ya wananchi wao.

Mataifa hayo mawili yaliingia kwenye mgogoro mkubwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Serikali ya Burundi chini ya Rais Pierre Nkurunziza iliituhumu Serikali ya Rwanda inayoongozwa na Rais Paul Kagame kuwasaidia waasi wanaoisumbua Serikali ya Bujumbura.

Ugomvi huo ulishamiri zaidi katika kipindi cha mwaka 2015, baada ya Rwanda kujibu mapigo kwa kuituhumu Serikali ya Burundi kuwasaidia waasi wanaopigana dhidi ya Kigali. Hali hiyo ilichochea matukio yaliyozidisha msuguano baina ya Serikali za Burundi na Rwanda.

Mathalani, Novemba mwaka 2015, Serikali ya Burundi iliwarudisha nyumbani wabunge wake wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), baada ya kutokea matukio ya mauaji nchini mwao.

Serikali ya Burundi ilibainisha kuwa, vitendo vya mauaji vilivyokuwa vikifanywa nchini humo vilichochewa na kikundi cha waasi wanaopingana na utawala wa Nkurunziza.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Refugee International  iliyotolewa Desemba 14, 2015, ilibainisha kuwa Rwanda ilikuwa ikiwafadhili waasi wanaopigana dhidi ya Serikali ya Burundi.

Baada ya kutoka ripoti hiyo, Msemaji wa Rais wa Burundi, Willy Nyamitwe, aliviambia vyombo vya habari kuwa wakimbizi wa Burundi walioko kambini nchini Rwanda wamekuwa wakisajiliwa kujiunga na kundi la waasi, na kwamba nchi hiyo inawapatia mafunzo na silaha.

Ilielezwa kuwa, kundi la waasi linalofadhiliwa na Rwanda ndilo lililofanya jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali ya Burundi Mei 2015.  Zaidi ya majenerali 10 na maofisa wa kijeshi waliotuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi walifikishwa mahakamani mjini Gitega, Burundi.

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa, wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda wanapatiwa silaha na kikundi ambacho si cha kiserikali kwa minajili ya kuishambulia Burundi.

Nayo ripoti ya siri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya Februari 2016 inaituhumu Rwanda kuwa inawapa mafunzo wakimbizi wa Burundi kwa shabaha ya kumwondoa madarakani Rais Nkurunziza. Ripoti hiyo ilitolewa baada ya kuhojiwa waasi 18 wa Burundi katika Mkoa wa Kivu Kusini, huko Mashariki mwa Kongo.

Kwa upande wake, Serikali ya Rwanda ilikanusha  shutuma hizo. Waziri wa nchi hiyo anayehusika na masuala ya wakimbizi na kupambana na majanga, Seraphine Mukantabana, alibainisha kuwa shutuma hizo ni madai yasiyo na msingi wowote.

Waziri huyo alisisitiza kuwa, hata wakimbizi wachache wa Burundi wanaoamua kurudi nyumbani, hufanya hivyo kupitia njia zinazotambulika kisheria.

Takwimu za Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) zinaonyesha kuwa watu 220,000 raia wa Burundi wameikimbia nchi hiyo na kuwa wakimbizi katika nchi za kigeni.

Julai 2016, Serikali ya Burundi ilijitoa kuhudhuria mkutano wa 27 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mjini Kigali, nchini Rwanda. Sababu kubwa iliyotolewa na serikali hiyo ni usalama mdogo wa ujumbe wake kwa kipindi chote cha mkutano. Ndiyo kusema msuguano baina ya Burundi na Rwanda ulichochea uamuzi huo.

Machi mwaka huu, wabunge watano kati ya 9 wa Burundi katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), walikataa kuhudhuria kikao cha Bunge hilo kilichoketi mjini Kigali, Rwanda.

Wabunge hao hawakuhudhuria kikao kilichoketi kuanzia Machi 5 hadi 17, mwaka huu. Sababu kubwa iliyotolewa ni tofauti za kisiasa na msuguano uliopo kati ya Rwanda na Burundi, hivyo kuzua hofu juu ya usalama wao.

Aidha, wabunge hao waliandika barua kwa Spika wa EALA, Daniel Kidega, kueleza sababu za kutohudhuria vikao vya Bunge. Uamuzi wa kuandika barua hizo ulitokana na kikao kati ya wabunge hao na Spika, kilichofanyika Januari 18, mwaka huu kuelezea wasiwasi wa usalama wao endapo watakwenda Kigali.

Matukio yote hayo yanaonyesha hali mbaya kati ya Rwanda na Burundi, hivyo kuwa changamoto kwa wabunge wapya wa EALA namna ya kuzirudisha nchi hizo katika hali ya kawaida na ujirani mwema.

Kama wabunge wa EALA wanaowakilisha Burundi hawahudhurii vikao vinavyofanyika Kigali, ni dhahiri hali hii itadumu hata kwa Bunge jipya (bila kujali wawakilishi wapya watakaoingia).

Inatarajiwa pia kwa wabunge wa Rwanda kutohudhuria vikao vya EALA endapo vitafanyika Burundi. Tunafahamu pia Burundi inakabiliwa na tatizo la usalama, tangu jaribio la mapinduzi la mwaka juzi pamoja na vurugu za uchaguzi kupinga Nkurunziza kugombea tena.

Kwa muktadha huo, Bunge jipya la EALA linakabiliwa na changamoto kubwa ya kusuluhisha ugomvi uliopo baina ya Rwanda na Burundi. Bunge la EALA linakabiliwa na jukumu hilo kutokana na hatua ya Burundi kuhofia usalama wao wakiwa ndani ya Rwanda.

Uamuzi huo unajenga dhana kuwa Burundi inatumia uzoefu wa kukabiliana na vikundi vya waasi, kutunguliwa kwa ndege iliyombeba Rais wao wa zamani, ni miongoni mwa mambo yanayofanya wazidishe hofu na kuchochea msuguano baina yao.

Ikumbukwe kuwa, Rais Kagame ni miongoni mwa wanaotuhumiwa kuchochea vita huko Kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatua ambayo Burundi inaweza kutumia kama nyenzo ya kuepuka kuhujumiwa na Serikali ya Kigali.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles