MBUNGE wa Bunda mjini mkoani Mara, Ester Bulaya amewataka wakazi wa jimbo hilo kutokuwa na wasiwasi kuhusu changamoto zinazomkabili.
Amesema yeye bado ni mbunge wao na atatimiza ahadi zake alizowaahidi wakati wa kampeni za kuwania ubunge mwaka 2015.
Bulaya aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikabidhi jezi na mpira kwa timu 23 za mpira wa miguu Bunda mjini, pikipiki mbili katika Saccos za vijana ya ‘Ulipo tupo, Sh milioni moja kwa Saccos ya akina mama ya Furahisha na Sh 1,000,000 na viti 20 kwa Saccos ya Nyasura .
Alisema hiyo ni miongoni mwa hatua za kutekeleza ahadi ya kuwainua katika uchumi na kuongeza ajira kwa vijana na kina mama.
“Napenda niwahakikishie kuwa mimi bado ni mbunge wenu na nitahakikisha natimiza ahadi zangu kwenu… nilisema nikiwa muongo katika ujana wangu. Nitakuwa mchawi nitakapokuwa mzee.
“Hizi fedha ni nje ya fedha ya jimbo, nimezitafuta kwa njia mbalimbali lakini pia fedha za jimbo zitakapotoka pamoja na zile za bajeti ya halmashauri yetu tutapeleka katika maeneo yaliyokusudiwa.
“Kwa mwaka huu pekee mbali na fedha wa mfuko wa jimbo nimetenga Sh milioni 15 kuongezea nguvu Saccos zilizoko tayari lakini pia nimetumia Sh milioni 12 kwa ajili ya jezi na mipira kwa timu zote ndani ya jimbo langu,” alisisitiza Bulaya.
Alisema zipo changamoto za maendeleo jimboni humo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara, umeme, maji, Elimu na afya na kwamba atazishughulikia hatua kwa hatua.
Mbunge huyo hivi sasa anakabiliwa na kesi ya kupingwa ushindi wake huku ofisi ya ubunge ikiwa imempa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya bunge.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake kwa mbunge huyo, Mwenyekiti wa Saccos ya Nyasura, Samwel Mbasa alisema Bulaya ameonyesha mfano mzuri na kwamba wako nyuma yake.