26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Brela yawaita wakulima kusajili nembo, alama za biashara

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewashauri wakulima kusajili alama za biashara na huduma (nembo) ili kuzitofautisha bidhaa zao na zingine zilizopo sokoni.

Akizungumza leo Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Ofisa Usajili kutoka BRELA Dodoma, Gabriel Girangay, amesema wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanapozalisha mazao wanayaongezea thamani hivyo kuhitaji kusajiliwa nembo au alama za biashara.

“Wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanazalisha bidhaa mbalimbali na kuzipeleka sokoni ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu watambue kwamba BRELA ni muhimu kwao katika kusimamia au kulinda bidhaa zao. Tutalinda vumbuzi zao katika masuala mbalimbali yanayohusiana na kilimo na teknolojia,” amesema Girangay.

Ofisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Dodoma, Gabriel Girangay, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Amesema wakala huo unafanya kazi ya kusajili kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

“Tuko kwenye maonesho ya Nanenane kwa ajili ya kutoa elimu na huduma mbalimbali, ukifika katika banda letu utapata huduma za kusajiliwa jina la biashara na kila Mtanzania mwenye nia ya kuanzisha biashara afike kuna wataalam wa masuala ya Tehama, biashara, alama za biashara na huduma na shughuli zetu nyingi zinafanyika kidijitali.

“Tunatoa leseni za biashara kundi A ambazo ni zile zenye sura ya kitaifa na kimataifa, utaelimishwa kwanza na kama unataka kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi au kutoa bidhaa kutoka nje na kuleta nchini utapata leseni BRELA,” amesema.

Amesema wanatoa leseni za viwanda vikubwa na vya kati vyenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 100 kwenda juu lakini Sh milioni 100 kwenda chini ni viwanda vidogo ambavyo pia wanavisajili.

Ofisa hiyo amesema kama mtu anahitaji kupata taarifa yoyote kuhusu kampuni, majina ya biashara, leseni au wanaotaka kukopa na kuingia ubia wa kibiashara wafike katika banda hilo au ofisi za wakala huo kuelimishwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles