FORTALEZA, Brazil
WENYEJI wa fainali za Kombe la Dunia, Timu ya Taifa ya Brazil,
wataingia uwanjani kesho katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo dhidi ya wababe wa Amerika Kusini, Colombia.
Colombia itajitupa kwenye Uwanja wa Estadio Castelao mjini Fortaleza, ikiwa ni baada ya kufanikiwa kuitupa nje Uruguay kwa mabao 2-0 wakati Brazil iliitoa Chile kwa penalti 3-2.
Wakati huo huo staa wa Brazil, Neymar ambaye alizua hofu ya kukosa mchezo dhidi ya Colombia amedaiwa kupona majeraha yake hivyo atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza kesho.
Kwa mujibu wa daktari wa Shirikisho la soka nchini humo (CBF), Jose Luiz Runco alisema kuwa Neymar atakuwa imara kiafya hivyo yupo tayari kwa mchezo dhidi ya Colombia mjini Fortaleza.
Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari alipata wasiwasi juu ya afya ya nyota wake kutokana na mchezo mbaya aliochezewa na Chile.
Baada ya mchezo dhidi ya Chile, Neymar anadaiwa kulalamikia maumivu ya paja la mguu wa kushoto.
“Ni maumivu yake ndiyo kitu kinachotuumiza. Atapumzishwa kwenye mazoezi lakini daktari Runco amesema hakuna sababu za kuhofia kwani atamudu kucheza mechi dhidi ya Colombia,” alsiema Rodrigo Paiva msemaji wa CBF.