29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Brandy: Wazazi walinifanya niwe baamedi

PICHA YA KAVA ITUMIKE NUSU PLZ, KUANZIA TUMBONI

Na MWANDISHI WETU,

INAWEZEKANA umesikia mengi kuhusu stori za  wasichana wanaofanya kazi za kuhudumia katika baa mbalimbali maarufu mabaamedi, lakini hii inaweza kuwa simulizi ya kipekee zaidi.

Mara kadhaa imekuwa ikielezwa kuwa, wahudumu hao pamoja na kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa, pia wamekuwa wakijihusisha na shughuli nyingine haramu kwa lengo la kujipatia kipato zaidi.

Madai yanasema kuwa, wakati na baada ya kumaliza majukumu yao hufanya ‘biashara’ ya kukodisha miili yao kwa njia isiyo rasmi.

Tofauti na machangudoa ambao hujipanga barabarani au kwenda kwenye kumbi za starehe kusaka wateja, baadhi ya akinadada hawa, hudaiwa kuwawinda wateja wao wanaofika sehemu zao za kazi.

Hata hivyo, kiuhalisia ni kwamba wateja wao hujipeleka wenyewe katika maeneo yao ya kazi huku wengine wakishawishika baada ya kukolea kilevi.

Msichana Brandy (siyo jina halisi), 22, aliyezungumza na mwandishi wa Juma3tata, anasimulia mengi anayokutana nayo akiwa kwenye majukumu yake ya kujipatia riziki, huku akidai kuwa wazazi wake, ndiyo chanzo hasa cha yeye kufanya kazi ya kuhudumia baa.

Brandy, msichana mrembo wa sura na umbo, anayehudumia katika baa moja iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam, alijikuta akiwa wazi kwa paparazi wa Juma3tata, baada ya kujenga naye urafiki kwa siku kadhaa, kama mteja wa baa hiyo.

 

MIPANGO YAWEKWA

Suala la mabaamedi kudaiwa kutoka na wanaume mbalimbali kwa lengo la kujiongezea kipato siyo jambo jipya kwa jamii, lakini katika kutaka kupata ukweli, paparazi wetu alilazimika kujenga urafiki na dada huyo kwa lengo la kumchimba ili kujua undani wa maisha halisi wanayoishi.

Gia namba moja iliyotumiwa na mwandishi wetu ilikuwa ni kutaka kuhudumiwa naye pekee huku akijenga mazoea ya  kumwachia chenji kila anapolipa bili yake.

Taratibu ukaribu huo ukazaa urafiki na kujikuta wakianza kupiga soga za hapa na pale, hadi alipomuweka kwenye mstari na kufunguka maisha yake na wasichana wenzake wakiwa kwenye kazi hiyo.

 

MWANZO WA UKWELI

Ilikuwa usiku wa saa 6 kasoro, ambapo baa ilikuwa imeshafungwa na kubaki wateja wachache waliokuwa wakimalizia bia zao kaunta. Paparazi wetu alikuwa miongoni mwao.

Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda na wahudumu karibu wote walikuwa wameshaondoka eneo la kazi, mwandishi wetu alipata nafasi ya kukaa na Brandy na kupiga soga za hapa na pale.

Ghafla alitokea mwanaume mmoja, mtu mzima ambaye alizungumza na mlinzi wa baa hiyo akihitaji kuitiwa mmoja wa wahudumu ambaye alikuwa ameshaingia kwenye chumba chao cha kulala ‘gheto’.

Mlinzi huyo hakukaidi, alikwenda kwenye mlango wa gheto na kugonga na muda mfupi baadaye msichana husika alitoka na kuongozana na mwanaume yule ambaye kiumri walikuwa sawa na mtu na bintiye!

Hapo ndipo mwandishi wetu alipopata mwanya wa kufukunyua zaidi kwa Brand, akampachika swali moja: “Hao vipi tena? Ni mtu na mpenzi wake au?”

Brandy akajibu: “Hapana… siyo mtu na mpenzi wake, sema mtu na mtu wake. Hakuna mapenzi hapo kaka yangu, kuna maumivu, mateso na majonzi matupu. Unadhani yule mzee ana ujanja wa kutoka na msichana mzuri kama yule?”

Paparazi wetu akiwa na shauku ya kutaka kujua zaidi, akamwuliza: “Unamaanisha nini sasa Brandy? Mbona wameondoka pamoja sasa?”

Brandy akasema: “Ni maisha. Njaa tupu. Yule hawezi kumpenda yule mzee. Angalia alivyo mnene, mtu mzima na kitambi vile, wakati yule (anamtaja jina) ni binti wa miaka 20 tu. Anafanya vile kwa sababu ya maisha tu.

“Hana namna. Sanasana hapo atampa shilingi 10,000 au 15,000 akiwa mstaarabu sana basi atampa labda shilingi 20,000, maisha yanakwenda. Lakini si kwamba anampenda. Hakuna mapenzi hapo.”

 

KILIO CHA BRANDY

Mwandishi wetu akitaka kujua ukweli zaidi, akamuuliza ikiwa naye huwa anafanya mchezo huo; kwa sauti ya majonzi Brandy akajibu: “Ndiyo… mara chache, lakini sipendi. Mimi siyo mhuni, lakini nitafanyaje sasa?

“Sidhani kama kuna msichana anayefanya hizi kazi zetu eti asiwe na wanaume, hapo tutakuwa tunadanganya. Mimi nakueleza ukweli kwa sababu wewe ni rafiki yangu, ila kiukweli hali ya maisha ndiyo sababu.”

Huku akifuta machozi Brandy anaendelea kusimulia: “Mimi ni mtu Tabora. Natokea Urambo. Mama yangu alifariki nikiwa darasa la saba, sikuwahi kumjua baba.

“Mama alisema baba alinikataa tangu nikiwa tumboni. Sina taarifa zake zaidi ya kusikia alikuwa dereva wa mabasi. Sifahamiani na ndugu yeyote upande wa baba yangu. Baada ya kifo cha mama, maisha yakawa magumu nyumbani.

“Nilipomaliza darasa la saba, nilikaa miaka miwili nikifanya vibarua nyumbani kwetu, rafiki yangu mmoja akanishawishi twende mjini (Tabora) kutafuta kazi. Huko ndipo nilipopata kazi kwenye baa moja pale Ipuli na baadaye tukaamua kuja huku Dar.”

 

TATIZO KIPATO DUNI

Brandy anasema tatizo kubwa linalowakabili ni kipato kidogo na kukatwa mishahara yao huku manyanyaso yakiwa makubwa kutoka kwa mabosi wao.

“Watakaokuambia eti tunawakataa wanaume, ni waongo. Utawezaje kukataa wakati una matatizo? Kwanza mazingira ya kazi ni magumu, mabosi wanatunyanyasa, lakini hatuna namna.

“Tunanyanyaswa kijinsia, baadhi ya sehemu kabla hujaingia kazini, meneja anataka kutembea na wewe kwanza. Angalia kama siyo kunyanyasana ni nini? Kama hiyo haitoshi, vyumba vyetu siyo rafiki kabisa.

“Chumba kidogo mnaweza kulala hata wasichana kumi, hapa sisi tuko sita, watano tunahudumia nje na kaunta mmoja. Wote tunalala humo gheto. Kiafya siyo sahihi. Lakini ikitokea mtu akaenda na mwanaume, mliobaki mnalala kwa raha kidogo,” anasema na kuongeza:

“Hebu ona kaka, mishahara yetu mara nyingi ni kuanzia shilingi 50,000 hadi 100,000, siyo zaidi ya hapo. Mfano hapa tunalipwa 70,000, lakini kuna shoti – mteja akiondoka na bili ujue imekula kwako.

“Sasa unakuta mara nyingi mpaka mwisho wa mwezi una shoti ya shilingi 20,000 wakati mwingine mpaka 30,000, mwajiri bila huruma anaifyeka, unabaki na nini sasa?

“Je, unadhani kwa hiyo 40,000 au 50,000 inayobaki, inaweza kuendesha maisha kwa mwezi mzima? Haiwezekani. Hapa chakula tunakula bure asubuhi na mchana ukiwa getho, usiku tunajitegemea.

“Kifupi lazima ujitegemee mlo mmoja na maji ya kunywa kila siku. Utawezaje kumudu kwa fedha hiyo? Ni ngumu sana kaka yangu. Hiyo ndiyo sababu inatufanya tujikute tunashawishika, lakini ukweli ni kwamba wengi wetu hatupendi kabisa hii tabia, hata mimi sipendi.”

 

MARADHI YA NGONO

Akizungumzia kuhusu namna anavyojikinga na maradhi yanayotokana na njia ya ngono ikiwemo ukimwi, Brandy anasema daima hutumia mpira kama njia ya kujikinga.

“Bila kinga siendi, sina haya na maisha yangu. Mapema huwa namuuliza mtu… kama hana nakwenda kununua mwenyewe. Siwezi kuweka maisha yangu rehani hata siku moja. Wakati mwingine huwa nakuwa nazo mwenyewe kabisa.” anasema akionyesha kujiamini Brandy.

 

MIPANGO YAKE

Brandy anasema, pamoja na ugumu wa maisha yake ya kazi anayoishi, hana mpango wa kuendelea kufanya hiyo kazi kwa muda mrefu; akipanga kuachana nayo baada ya kupata mtaji wa biashara.

“Nilipokuwa nyumbani Tabora, nilijifunza mambo ya salon, kwa kiasi fulani nina utaalamu. Hapa najichangisha tu ili nikamilishe vifaa vyangu na pesa ya fremu ya biashara, niachane na hii kazi,” anasema Brandy.

Katika kuonyesha alichokisema ni kweli, Brandy alimwonyesha mwandishi wetu picha za baadhi ya vifaa vikiwemo mashine za kukaushia nywele na viti vitatu vya wateja wanaohudumiwa zilizokuwa kwenye simu yake.

“…hivi vitu vipo Sinza kwa dada yangu wa hiyari. Sidhani kama nina miezi sita kwenye hii kazi. nikikamilisha nakwenda kuanzisha salon yangu, naachana na haya mateso na kujidhalilisha,” anasema Brandy.

Saa 7:20 usiku, mwandishi wetu aliagana na Brandy na kumwachia shilingi 10,000 ya kuanzia maisha siku inayofuata, akaingia gheto kupumzika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles