21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Bouteflika ang’ang’ania Ikulu, umri, afya vyamtesaHASSAN DAUDI NA MITANDAO

HALI ya kisiasa nchini Algeria si shwari kutokana na maelfu ya wananchi kuendelea kuingia mitaani kupinga kitendo cha Rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika, kutaka kurejea madarakani kwa awamu ya tano.

Licha ya nguvu ya vyombo vya dola, ikiwamo kutumia mabomu ya machozi, bado wanaume na wanawake wamekuwa wakiandamana katika mitaa jijini Algiers, wakiwa na mabango yenye jumbe za kukataa nia ya kiongozi huyo kugombea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 18, mwaka huu.

Walio wengi wanakerwa na uamuzi wa Bouteflika ambaye hivi sasa anatembea kwa msaada wa kiti cha magurudumu kugombea tena, wakisema si tu afya yake kuendelea kudhoofu, bali umri wake wa miaka 82 unaweza kuwa kikwazo katika utendaji kazi wake.

Bouteflika hajaonekana hadharani tangu alipougua kiharusi mwaka 2013 na amekuwa akienda nje ya nchi mara kadhaa kwa matibabu, safari hii akiwa Uswis alikokwenda tangu Februari 24, mwaka huu.

Kutokana na hilo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria waliotajwa kufikia 1,000 waliingia mitaani, wakisema hali ya afya ya kiongozi wao huyo inatosha kuthibitisha kuwa hapaswi kurejea Ikulu.

Kwa upande mwingine, huenda hali ilivyo sasa ikawa inampasua kichwa Rais huyo kwani haya ni maandamano makubwa zaidi ya kumpinga tangu alipoingia madarakani miaka 20 iliyopita.

Wachambuzi wa siasa wanayaona machafuko haya kuwa ni makubwa zaidi kuliko yale ya mwaka 2002, ambayo yalisababisha watu wapatao 150,000 kupoteza maisha.

Je, ni umri na afya pekee kuwa ndiyo sababu ya Bouteflika kutotakiwa na idadi kubwa ya wananchi wa Algeria? Hapana, yapo mengine yaliyozorotesha uhusiano wake na wapiga kura hao kama makala haya yanavyochambua.

Wafuatiliaji wa siasa za Kaskazini mwa Afrika hawana shaka kuwa hali ilianza kuwa mbaya mara tu Serikali ya Bouteflika iliposhindwa kuzuia kuporomoka kwa bei ya mafuta nchini humo.

Ikumbukwe kuwa mafuta huchangia asilimia 60 ya bajeti ya nchi na nishati hiyo ni asilimia 95 ya bidhaa inayotegemea Algeria katika soko la nje.

Hiyo ilisababisha kushuka kwa uchumi wa Algeria, hivyo Serikali kushindwa kuendesha mradi wa ANSEJ uliokuwa ukiwapa mikopo maelfu ya vijana.

Ukiacha hiyo, wananchi wa Algeria walikerwa na skendo ya usafirishaji wa dawa za kulevya ingawa baadaye baadhi ya viongozi wa Serikali walitumbuliwa. Kipindi ambacho asilimia zaidi ya 30 ya vijana hawana ajira, haya yanatokeaje?

Hilo ndilo swali lililogonga vichwa vya Waalgeria, ikizingatiwa kuwa iliwahi kuripotiwa kwamba maelfu ya vijana wa Algeria wamekuwa wakiikimbia nchi hiyo kwenda kusaka maisha kwingineko.

Kukamatwa kwa meli iliyokuwa na kilo 700 za dawa za kulevya aina ya cocaine ni taarifa iliyowaumiza wengi, hasa baada ya kusikia aliyekuwa amehusika katika uhuni huo ni mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa.

Pia ni kipindi hicho, ndipo wananchi hawakuwa na imani na urafiki kati ya Serikali yao na wafanyabiashara wakubwa.

Kuifanya Algeria kuwa mali ya watu wachache, akiwamo mdogo wake wa kiume, Said Bouteflika (61), ambaye huwezi kukutana na Bouteflika bila yeye, ni jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa wananchi wa taifa hilo.

Nguvu ya wafanyabiashara matajiri imekuwa kubwa, nikitolea mfano tukio la mwaka 2017, ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdelmadjid Tebboune, alifukuzwa kazi miezi miwili tu baada ya kuzuia wafanyabiashara wasiagize bidhaa kutoka nje.

Aidha, kwa kipindi kirefu, kumekuwapo na matukio ya uminywaji wa uhuru wa kujieleza, ukiwalenga zaidi waandishi wa habari, sifa ambayo imekuwa ikizipamba serikali nyingi barani Afrika.

Mwaka 2016, mwandishi wa habari ambaye ni raia wa Marekani mwenye asili ya Algeria, Mohamed Tamalt, alifariki akiwa kizuizini nchini humo. Tamalt alishikiliwa na polisi mara baada ya kutumia ukurasa wake wa Facebook ‘kuposti’ ujumbe uliotajwa kumchafua Rais Bouteflika.

Mwandishi huyo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani na hata hali yake ilipokuwa mbaya, mamlaka za Algeria ziligoma kumwachia. Kifo chake kiliibua hasira kali za wananchi dhidi ya Serikali ya Bouteflika.

Uongozi wa Bouteflika umekuwa ukinyooshewa kidole mara kadhaa na watetezi wa haki za binadamu, ukitajwa kuwa na mahakama zisizojitegemea, kwa maana ya zinazofanya kazi kwa matakwa ya viongozi wa Serikali.

Serikali kupitia mashirika yake imekuwa ikivinyima matangazo vyombo vya habari vinavyoripoti habari za vyama vya upinzani na kama hiyo haitoshi, waandishi wa kigeni wamekuwa wakinyima ‘visa’.

Licha ya kuwapo kwa zaidi ya magazeti 80 katika Jiji la Algiers, ni magazeti sita pekee, ambayo wananchi wanayaamini kwani mengi yanamilikiwa na wafanyabishara walio karibu na Serikali.

Hata hivyo, bado wadukuzi wa masuala ya siasa hawaoni kama vyama vya upinzani viko imara kuweza kumwangusha Bouteflika.

Imebaki kwenye kumbukumbu kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014, alifanikiwa kushinda licha ya ukweli kwamba wala hakuwa na mpambe wa kumpigia kampeni.

Tatizo linaloelezwa ni kwamba kumekuwa na mpasuko ndani ya upinzani, ambao kwa kiasi kikubwa umesababisha chama tawala, National Liberation Front (FLN), kibaki madarakani tangu kilipoingia mwaka 1962.

Si hivyo tu, wachambuzi wa siasa hawajaacha kuibua madai kuwa wapo viongozi wa upinzani wanaoshirikiana na Serikali kwa masilahi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles