Na Esther Mnyika, Mtwara
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka waandishi wa habari nchini kutumia nafasi zao kuelimisha jamii na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa kwa kuibua masuala ya kifedha, biashara, na uwekezaji.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 25, 2025, na Mkurugenzi wa Tawi la BoT, Mtwara, Nassoro Ali Omary, kwa niaba ya Naibu Gavana wa BoT, Julian Raphael, wakati wa ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari wa masuala ya uchumi, fedha na biashara kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Omary amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutumia majukwaa yao kuelimisha jamii kuhusu masuala ya kifedha, ikiwemo taratibu za mikopo na umuhimu wa kuzingatia sheria za kifedha.
“BoT tunatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari katika kuelimisha umma, ndio maana tunaendelea kushirikiana nao. Kupitia semina hii, tunatarajia kuwa mtakuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria na taratibu za mikopo ili kuepuka mikopo haramu inayojulikana kama ‘kausha damu’,” amesema Omary.
Ameongeza kuwa, kutokana na maendeleo ya teknolojia, BoT inatarajia waandishi wa habari kuelewa mfumo mpya wa utekelezaji wa sera ya huduma za kifedha unaotumiwa na serikali katika kukuza uchumi na maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa BoT, Vick Msina, amesema lengo la semina hiyo ni kukuza uelewa wa waandishi wa habari kuhusu masuala ya benki kuu na kujenga uhusiano mzuri kati ya BoT na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa za kifedha zinawafikia wananchi kwa haraka na kwa usahihi.

Ameeleza kuwa BoT imekuwa ikiandaa semina hizi kwa miaka 17 mfululizo, tangu zilipoanzishwa na aliyekuwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, na zimeendelea kuwa chachu ya ushirikiano mzuri kati ya BoT na waandishi wa habari katika kuboresha uelewa wa masuala ya kifedha nchini.
“Tunafanya mafunzo haya kila mwaka kwa lengo la kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa kuripoti masuala ya uchumi na fedha kwa usahihi, huku tukihimiza ushirikiano kati ya BoT na vyombo vya habari,” amesema Msina.
Semina hiyo imewakutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Zanzibar, ili kuwapa uelewa wa kina kuhusu masuala ya kifedha na mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.