27.4 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

BoT yatoa sababu dola kupanda dhidi ya shilingi

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza sababu nane za kupanda kwa Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi huku ikieleza kwamba hatua hiyo haijaathiri uchumiwa nchi.

Hadi kufikia jana Dola ya Marekani ilikuwa ikiuzwa Sh 2,420 kwenye baadhi ya maeneo.

Akizungumza na MTANZANIA jana Mkurugenzi wa Sera za Uchumi na Utafiti wa BoT, Dk. Suleiman Misango, alisema kuimarika kwa dola dhidi ya shilingi ni suala la mpito linalotarajiwa kuisha kuanzia Machi.

Akitoa sababu za hali hiyo, alisema dola imeimarika pia dhidi ya sarafu nyingine duniani ikiwamo Euro ambayo imekuwa ikipoteza thamani kuliko hata shilingi ya Tanzania.

Pia alisema suala la mauzo ya mazao nje kama korosho, pamba, kuanza msimu wa watalii kuwa ni baadhi ya mambo yanayotarajiwa kusaidia shilingi kuimarika dhidi ya dola.

Alisema pia wasiwasi unaosababishwa na uvumi kama ambao walizisha mawakala waliotaka kununua korosho kwa kuwalangua wakulima, inaweza kuwa sababu ya kuogopesha watu na dola kuimarika.

 “Ukiangalia Euro nayo ilikuwa ikipoteza sana lakini sisi Shilingi yetu bado iko imara sana. Tena wao wamepoteza kwa kiasi kikubwa kuliko sisi tulivyopoteza.

“Kwa hiyo kama dola inakuwa inapanda thamani yake kutokana na wawekezaji zaidi hasa kwa kipindi hiki wanakwenda zaidi Marekani ambapo kipindi cha hivi karibuni uchumi wao ulikuwa ukifanya vizuri na hata riba kule zimekuwa zikifanya vizuri.

“Kwa hiyo unakuta wawekezaji wanakwenda kule jambo ambapo wanapokuwa huko wanahitaji zaidi dola, jambo linaloifanya inakuwa ghali dhidi ya fedha yako, ila tu huwa ni kipindi cha msimu,” alisema Dk. Misango.

Alisema dola inapokuwa ghali hupanda thamani yake hasa kutokana na mahitaji ya wakati huo.

“Mfano jana tulikuwa tunabadili Shilingi kwa dola moja labda kwa Shilingi 2,400, sasa wewe ukiwa na dola ni lazima utasema kwamba hela yangu inahitajika zaidi huko duniani. Ili niweze kukupatia inabidi kulinganisha lakini mwanzoni soko lilikuwa limepanda kidogo,” alisema

Pamoja na hali, alisema “ila unapoangalia mahitaji bado yapo ya kutosha, tunaweza kusema labda wasiwasi tu kama unakumbuka kipindi cha uchaguzi 2005 watu walivumisha kwamba hali inaweza kuwa si nzuri. Hata aliyekuwa anakula kilo moja ya wali akaamua kufanya stoking ya kutosha ya chakula,  jambo lilosababisha chakula kupanda bei kutokana na wasiwasi tu.

“Hii hali baada ya muda si mrefu itakaa sawa, nimeona leo kwenye vyombo vya habari Serikali ikialika wanunuzi wa korosho, sasa wanunuzi watakuja na hivi karibuni tutapata mauzo ya korosho na hata kuna fedha nyingine ambazo Serikali itapata kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema

Alisema hali kama hiyo ilitokea mwaka 2005  kuanzia Desemba lakini ilipofika Machi hali ilikuwa sawa na ilipofika Aprili iliongezeka kuwa nzuri zaidi.

“Na ilipofika Mei hali ilitengemaa kwa sababu mauzo yalipanda kama mazao ya pamba ambapo huwa msimu wake huwanzia kipindi hicho ikiwamo pia watalii ambapo huendelea hadi Desemba.

“Hizi sababu za msimu tu ila hadi mwezi wa tatu itakuwa sawa kama mauzo haya ya mazao yakiwa mazuri itakuwa nzuri zaidi. Kama kungekuwa na mahitaji ya fedha za kigeni hata wewe huko mtaani tungekuwa tunaulizana hivi vitu tunaagiza viko wapi.

“Kwenye import (uagizaji bidhaa kutoka nje) tumebaki hivyo hivyo ingawa imebaki ya Serikali tu. Bei ya mafuta duniani kwa sasa hali si mbaya.

“Importation kubwa imekuwa ya Serikali ya ajili ya miradi ya maendeleo kama barabara ambazo zinajengwa, madaraja hapo Ubungo na barabara hiyo ya Morogoro na miradi mingine. Kwa hiyo Serikali ndiyo wana import zaidi kuliko sekta binafsi ambapo hatuoni kama kuna mabadiliko makubwa,” alisema

Dk. Misango alisema hata wakati Serikali inatangaza uamuzi wa kununua korosho, kuna baadhi ya watu walivumisha taarifa potofu kwa sababu tu ya kunyang’anywa masilahi yao.

“Hata wakati ule Serikali inanunua korosho kuna watu walivumisha, maana wakati mwingine kumnyang’anya mtu tonge mdomoni mawakala lazima waeneze yao kuhusu soko kila mtu anakuwa anaongea lake.

“Ninashie kwamba korosho ipo hapa, lazima itauzwa na kuna wanunuzi wamejitoza ni suala la muda tu. Wapo watu ambao wanasema acha ninunue sasa hivi ili baadae nije niuze lakini wanaweza kupata hasara kama hawatauza sasa,” alisema

Taarifa ya awali

Januari 30, mwaka huu Benki Kuu ya Tanzania, ilitoa taarifa na kusema kuwa kuna akiba ya kutosha ya fedah za kigeni kwani suala la kushuka kwa dola ya Marekani ni sababu ya msimu.

Hatua hiyo iliyokana na kuibuka kwa mijadala kuhusu thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni hususan dola ya Marekani imekuwa ikipungua na kusababisha mijadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Mijadala hiyo inaonesha kwamba, ama shilingi iko kwenye hali mbaya, au kuna upungufu wa akiba ya fedha za kigeni nchini.

“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutarifu umma kwamba mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya doal ya Marekani kunatokana na msimu huu ambapo mapato ya fedha za kigeni yanayotokana na utalii na mauzo ya nje ya mazao hupungua.

“Hali hii ni ya kawaida na hubadilika kuanzia sehemu ya pili ya kila mwaka, mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na utalii na mauzo nje huongezeka. Aidha, dola ya Merakani imekuwa ikiimarika thamani kwa siku za karibuni na kufanya fedha za nchi nyingine kupungua thamani.

“Aidha, Benki Kuu inapenda kuutarifu umma kwamnba Tanzania ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, ambayo inaweza kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 4.9. Kiwango hiki ni juu zaidi ya kiwango kinachotakiwa kwa nchi yetu cha uwezo wa kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa muda wa miezi 4 na kile cha Jumuiya ya Afrika Mashariki cha miezi 4.5,” ilieleza taarifa hiyo ya BoT

Taarifa hiyo ilieleza kwamba kiwango cha kubadilisha fedha huamuriwa na nguvu za soko zinatokana na mahitaji na kiwango cha fedha za kigeni kilichoko sokoni.

“Benki Kuu ya Tanzania hushiriki mara kwa mara katika soko kwa ajili ya kuhakikisha kuna utulivu katika kiwango cha kubadilisha fedha unaendana na vigezo vya kiuchumi.

“Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni katika soko na kuhakikisha kwamba washiriki katika soko hilo wanazingatia kanuni na maadili ya uendeshaji wa soko la fedha za kigeni,” ilisema BoT

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,672FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles