27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

BOT : AKAUNTI ZA SERIKALI HAZIJAPUNGUZA UKWASI

*Yaeleza mwenendo wa madeni ya nje, ulipaji

Na Bakari Kimwanga


JANUARI 27, mwaka jana Serikali kupitia kwa Msajili wa Hazina, ilitangaza uamuzi wa kuzitaka taasisi za umma kufungua akaunti za mapato Benki Kuu (BoT) kama njia ya kupunguza ukwasi katika uchumi.

Hatua hiyo ilipokewa kwa hisia tofauti na Watanzania na hata kueleza fedha itakuwa imepotea mitaani na kuondoa ukwasi kwa wananchi wa kawaida.

Lusajo Mwankemwa ni  Mchumi Mwandamizi wa BoT kutoka Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi, anasema ni vyema jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu na amana za muda maalumu.

Anasema akaunti za matumizi bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika na taasisi kufanya malipo kupitia akaunti hizo.

Kutokana na hali hiyo, anasema  bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukuma benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa (corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani za Serikali.

Anasema uamuzi huo umesaidia katika usimamizi wa mapato na matumizi ya mashirika hayo na pia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha kupitia Benki Kuu.

“Serikali imeacha kukopa fedha zake kwa gharama kubwa.Kwa kuwa amana za Serikali kwenye mabenki ya biashara ni sehemu ndogo tu (asilimia tatu) ya amana zote za mabenki, madai kwamba uamuzi wa Serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi kwenda kwenye akaunti za mapato BoT umesababisha kupungua kwa ukwasi hayana uzito,” anasema Mwankemwa.

Mwenendo wa Deni la Taifa

Akizungumzia mwenendo wa Deni la Taifa, anasema linajumuisha mikopo ambayo hukopwa na Serikali kutoka nje na ndani ya nchi kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kujaza nakisi ya bajeti.

Ambapo deni la nje hukopwa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile Benki ya Dunia, nchi wahisani na pia kutoka kwenye benki za biashara wakati deni la ndani linapatikana kwa kuuzwa kwa dhamana za Serikali na hatifungani (Treasury bonds), mikopo kutoka Benki Kuu na benki za biashara za ndani.

“Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na misaada Sura 134. Aidha, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa kikamilifu, Serikali inakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada  ili kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa.

“Hadi kufikia Desemba mwaka jana, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje lilifikia Dola za Marekani milioni 19,021.9  ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 18,459.3 Juni, mwaka jana, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.05.

“…kiasi hiki cha deni hakijumuishi deni la mifuko ya hifadhi ya jamii linalokadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 1,725.8, ingawaje deni hilo limezingatiwa katika tathmini ya uhimilivu wa Deni la Taifa,” anasema Mwankemwa.

Mchumi huyo anaongeza kuwa ongezeko la deni hilo limetokana  na mikopo iliyopo, mikopo mipya iliyopokelewa na Serikali na ambayo bado haijaiva kutoka mikopo ya ndani na nje ya nchi kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile reli ya Tazara, daraja la Kikwete Mto – Malagarasi, barabara za Morogoro–Dodoma, Dodoma–Singida–Arusha, Mwanza-Bukoba, mradi wa Maji ziwa Victoria, Bomba la Gesi Mtwara–Dar es Salaam, barabara ya Dodoma-Singida–Mwanza, miradi ya umeme Kinyerezi I & II, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano n.k.

Ulipaji Deni la Taifa

Akifafanua kuhusu ulipaji wa Deni la Taifa, anasema hauangalii ukubwa wa deni lililopo bali kadiri deni linavyoiva (debt maturity).

Anasema hali ilivyo sehemu kubwa ya Deni la Taifa linaiva kwa kipindi cha muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, kwa wastani wa deni lililopo sasa litaiva katika kipindi cha miaka isiyopungua 11.9, jambo linaloashiria athari zake kwenye bajeti ziko chini.

“Serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa mujibu wa mikataba. Katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi kufikia Desemba mwaka jana, Serikali ilitumia jumla ya Sh bilioni 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni Sh bilioni 1,822.3 na deni la nje ni Sh bilioni 747.8.

“Malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya shilingi bilioni 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2,” anasema.

Tathmini ya uhimilivu Deni la Taifa

Mchumi Mwankemwa anasema katika tathmini iliyofanyika Novemba mwaka jana, viashiria vinaonesha kuwa,  thamani ya sasa ya jumla ya deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56, thamani ya sasa ya deni la nje pekee kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.

Anasema sasa thamani ya  deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150 na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250.

“Kutokana na tathmini, ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20.

“Kwa kuzingatia vigezo hivyo, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa toka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati,” anasema.

Kutokana na muundo wa deni la Tanzania, anasema sehemu kubwa ya madeni yake yanaiva kwa muda mrefu (miaka 5 hadi 50).

“Hivyo, upimaji wa deni la Taifa huangaliwa kwa kutumia thamani ya sasa ya deni  badala ya kutumia thamani halisi ya deni, hii inaiwezesha tathmini kufanyika kwa madeni yanayoiva kwa muda mrefu kinyume na thamani halisi ya deni kwa pato la Taifa (nominal value of debt to GDP), ambayo inaangalia hali ya deni kwa muda mfupi.

“Kwa kuzingatia hali hiyo, viashiria vilivyooneshwa hapo juu ndio viashiria sahihi vilivyokubalika kimataifa katika upimaji wa uhimilivu wa Deni la Taifa,” anasema.

Mtaalamu huyo wa uchumi anasema kwa kuzingatia vigezo hivyo, uwiano wa deni lote la ndani na nje kwa thamani ya sasa kwa pato la Taifa kwa mwaka 2015/16, Kenya ilikuwa asilimia 45.6, Tanzania asilimia 34.2, Uganda asilimia 24.1.

“Na Rwanda asilimia 22.7. Vilevile uwiano wa deni la nje kwa thamani ya sasa kwa Pato la Taifa Kenya ilikuwa asilimia 19.4, Tanzania asilimia 19.9, Uganda asilimia 10.7 na Rwanda asilimia 17.3 ambavyo vyote bado viko chini  ya ukomo,” anasema Mwankemwa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,608FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles