27.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah Kamoli: Nimedhamiria kumaliza kero za wananchi wangu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema amedhamiria kutatua kero zote zinazowakabili wananchi wake na kuwataka wapime mambo ambayo yamefanyika kuanzia 2020 – 2023.

Baada ya kuahirishiwa kwa mkutano wa Bunge, Bonnah amekuwa akiendelea na shughuli mbalimbali zikiwamo za usimamizi wa utekelezaji miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kufanya mikutano ya hadhara kwenye kata mbalimbali jimboni Segerea.

Naibu Spika wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Segerea na kufanyika Stendi ya Kimanga, Dar es Salaam.

Septemba 15,2023 alikabidhi barabara mbili kwa wakandarasi zitakazojengwa kwa kiwango cha lami ambazo ni Majichumvi – Migombani – Kokomtama na ile ya Segerea – Bonyokwa kisha kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Kimanga.

Mbali na Kata mwenyeji ya Kimanga mkutano huo pia ulizishirikisha Kata za Tabata, Liwiti na Kisukuru.

Akizungungumza katika mkutano huo, Bonnah amesema ataendelea kuchapa kazi ili kumaliza kero za jimbo hilo.

“Naomba wananchi muendelee kutuunga mkono, tumuunge mkono Rais Samia, mimi mbunge wenu na madiwani wangu lakini pia mpime mambo ambayo tumeyafanya kwa miaka mitatu kuanzia 2020 mpaka 2023.

“Nilikuwa mbunge 2015 – 2020 kwa sababu sikupata ushirikiano kazi nyingi hazikufanyika, lakini kwa sasa nyie wenyewe mnaona mambo yanavyofanyika kwa kasi kubwa.

“Sasa hivi hatutasema mchakato, tunataka kuwaonyesha kwa vitendo, tutajitahidi kuhakikisha barabara zote za Jimbo la Segerea zinapitika. Tutahakikisha maji yanapatikana, tutahakikisha wananchi wanapata mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi,” amesema Bonnah.

Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jimbo la Segerea, wakimsikiliza mbunge wao (Bonnah Kamoli), wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Kimanga, Dar es Salaam.

Aidha amesema kazi kubwa imefanyika ya ujenzi wa miundombinu, afya na elimu lakini wanatarajia awamu ya pili ya mradi wa DMDP itamaliza changamoto za miundombinu.

“Tunaomba watu wa DMDP watekeleze mradi huu kwa haraka kwa sababu wananchi wanausubiri kwa hamu, wangependa wawaone wakandarasi ‘site’ wanaanza kujenga barabara.

“Kata ya Kimanga ndiyo ambayo imekuwa ikisubiri maendeleo kwa muda mrefu, kupitia DMDP Stendi ya Kimanga itajengwa, masoko na barabara,” amesema.

Mbunge huyo amesema pia tayari Serikali imetenga fedha za ujenzi wa kituo cha afya Kimanga na kwa sasa tathmini inaendelea ili uweze kuanza.

Aidha amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kukatika kwa umeme na kukosekana kwa huduma ya maji na hata machache yanayopatikana ni kwa mgawo.

Naibu Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, amepongeza juhudi zinazofanywa na mbunge huyo katika kuwaletea wananchi maendeleo akisema ni miongoni mwa wabunge wanaochapa kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, Edward Mpogolo, amesema mradi wa DMDP awamu ya pili uko katika hatua za mwisho kuanza kutekelezwa.

Amezitaja barabara mbalimbali ambazo zitakarabatiwa na nyingine kujengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni Barakuda – Chang’ombe – Majumba sita – Segerea (kilomita 3.5),

“Mbunge wenu (Bonnah) amepigania na kupata zaidi ya kilomita 75 ambapo anaongoza kwa majimbo yote. Tumejipanga kuongeza makusanyo kutoka Sh bilioni 87 hadi kufikia Sh bilioni 100 na kabla ya uchaguzi tutakuwa tumejenga vituo vyote vya afya…tunawahakikishia tunakwenda kuleta mapinduzi makubwa Jimbo la Segerea,” amesema Mpogolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles