27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Bonnah awahakikishia wananchi ahadi zote zitatekelezwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli amesema ahadi zote walizotoa kwa wananchi zitatekelezwa na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano na kumuamini kwani amedhamiria kuwaletea maendeleo.

Bonnah ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika mitaa mbalimbali ya Kata za Mnyamani na Kimanga ambapo pia alifanya mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wananchi.

Akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Shule ya Sekondari Wazazi iliyopo Kata ya Kimanga, Bonnah amesema hadi kufikia mwakani changamoto ya miundombinu katika Jimbo la Segerea itapungua kwa sababu baadhi ya kata tayari utekelezaji wa mradi wa DMDP unaendelea.

Aidha amesema soko lililopo Mtaa wa Faru Kata ya Mnyamani litabadilishwa matumizi ili kujengwa shule ya msingi kwa sababu kata hiyo haina shule ya msingi hatua inayosababisha watoto wemekuwa kwenda kusoma mbali kutokana na shule zilizo karibu kuelemewa.

Amesema pia Sh 6,894,919 zitatolewa kupitia mfuko wa jimbo kujenga mfereji uliopo Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Mnyamani uweze kupitika ili kuwapunguzia adha wakazi wa maeneo hayo hasa wakati wa mvua.

“Kata ya Kimanga kuna matatizo makubwa ya miundombinu na kwa sasa tumeanzia Kwa Swai Tembo Mgwaza tunajenga mfereji wenye urefu wa kilomita 2.3, itakayofuata ni barabara ya Maji Chumvi inayoanzia External ambayo itakuja mpaka Segerea pamoja na ujenzi wa stendi,” amesema Bonnah.

Naye Diwani wa Kata ya Kimanga, Pastory Kiyombya, amesema kata ina changamoto kubwa za miundombinu ambazo zimesababisha adha kwa wananchi hasa wakati wa mvua.

“Tutasimamia kwa ukamilifu miradi itekelezwe ili iweze kukamilika kwa wakati wananchi wetu waondokane na kero,” amesema Kiyombya.

Mmoja wa wananchi wa Kata ya Kimanga, Moses Nyenyembe amesema; “Kero kubwa zinazotukabili ni stendi, barabara na soko lakini mheshimiwa mbunge ametupa mwanga kwamba kero zetu zote zitatatuliwa.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side, amempongeza mbunge huyo kwa jitihada anazochukua kumaliza kero za wananchi sambamba na ufuatiliaji miradi ya maendeleo.

“Mimi kama msimamizi wa Ilani ya CCM Wilaya ya Ilala nimeridhika na kazi inayofanyika, naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazozifanya kuleta maendeleo katika kata zetu,” amesema Side.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles