24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah aahidi kutatua kero barabara Hospitali ya Harmony

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo Segerea, Bonnah Kamoli amesema atahakikisha barabara inayoingia katika Hospitali ya Harmony iliyopo Bonyokwa Darajani inatengenezwa kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kuzindua hospitali hiyo amesema Kata ya Bonyokwa ni mpya na huduma za kijamii bado ni chache lakini wako kwenye mikakati ya kuhakikisha inakuwa na mundombinu bora.

“Serikali inajitahidi kuongeza vityo vya afya lakini bado tunalemewa, nawapongeza sana ambao walikaa na kufikiria tuwe na hospitali hii. Changamoto ya barabara inayoingia hospitali tutashirikiana iweze kutengenezwa kwa sababu hii iko ndani ya uwezo wetu,” amesema Bonnah.

Aidha amesema barabara inayotokea Masia tayari Wakala wa Barabara (Tanroads) walishafanya usanifu na ile inayotoka Segerea kipande kilichobaki cha kilomita 1.5 iko kwenye mpango wa kujengwa na Tarura.

Mbunge huyo pia ameahidi kupeleka wataalam kesho waangalie namna ya kunusuru Mto Luhanga ulio jirani na hospitali hiyo ili usiendelee kuleta madhara.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Jullyan Mmary, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni ubovu wa miundombinu ya barabara hasa inayoingia hospitalini hapo na Mto Luhanga ambao umeendelea kula barabara hiyo.

“Tunaomba kipande cha barabara inayotoka Segerea kuja Bonyokwa kimaliziwe na ujenzi wa kingo za mto ili barabara isiendelee kuharibika,” amesema Jullyan.

Aidha amesema wamekuwa wakipata majeruhi wengi wa ajali na kushindwa kuwapatia huduma kwa wakati kutokana na kituo cha polisi kuwa mbali na kuahidi kuwa watatoa mifuko 50 ya saruji na tofali 1,000 kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi Bonyokwa.

Mwanasheria na Msemaji wa hospitali hiyo, Eneza Msuya, amesema wazo la kuianzisha lilianza baada ya mwanzilishi wake Issa Vitus kuhamia eneo hilo na kubaini lina changamoto ya ukosefu wa huduma za afya.

“Mji wa Bonyokwa una milima na miinuko mikali hivyo kuna wakati alilazimika kuwasaidia watu kufika katika vituo vya afya kwa kutumia usafiri wake, hakukuwa na vituo binafsi hapa karibu. Mama mjawazito akipata uchungu alikuwa akibebwa kwenye bajaji na inapofika kwenye mwinuko inashindwa kupanda…jambo hilo lilikuwa likimuumiza sana,” amesema Msuya.

Amesema malengo yao ya baadaye ni kuwa na hospitali kubwa inayotoa huduma zote za kibingwa na chuo cha kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali za afya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles