24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah aahidi kushirikiana na madiwani kuibua vipaji vya vijana

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema ataendelea kushirikiana na madiwani wote wa jimbo hilo kuibua vipaji vya vijana katika michezo mbalimbali.

Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, akisalimiana na timu ya wanawake wakati wa ufunguzi wa mashindano ya mpira wa miguu aliyoyaandaa katika uwanja wa Shule ya Msingi Majani ya Chai.

Bonnah ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano ya mpira wa miguu yaliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Kipawa (Kipawa Diwani Cup), amesema licha ya michezo kujenga afya pia ni ajira.

“Nampongeza diwani kwa kuandaa mashindano haya yanasaidia kuwaweka vijana karibu, mpira ni afya lakini mpira ni ajira kwa sababu vijana wengi wanaanzia chini, wanaanza katika timu ndogondogo hadi wanafikia hatua ya kucheza timu kubwa. Kwahiyo nitaendelea kushirikiana na madiwani ili tuibue vipaji vingi vya vijana na pia tutaandaa mashindano ngazi ya jimbo,” amesema Bonnah.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimji, amewataka madiwani wengine waige mfano wa Kwezi kwa kuandaa mashindano kama hayo ili kuacha kumbukumbu katika maeneo wanayoongoza.

Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimji (kulia) akimpongeza Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, kwa kuandaa mashindano ya mpira wa miguu.

“Ni vema madiwani tukawa na jambo ambalo tutakuwa tunalifanya kila mwaka kwa ajili ya kuacha kumbukumbu katika maeneo tunayaongoza, suala la mpira si burudani tu au afya, michezo kwa ujumla ni ajira kwa vijana. Vijana wengi sana wamenufaika kupitia mpira wa miguu mfano Mbwana Samata ameanzia kwenye michezo kama hii,” amesema Khimji.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, amesema kata hiyo ina vipaji vingi lakini katika miaka ya karibuni michezo ilikuwa imelala kwahiyo amejipanga kuiinua.

“Nilivyoingia kwenye nafasi hii mwaka 2020 moja ya malengo yangu ni kuhakikisha tunainua michezo na kuwakusanya vijana pamoja ili tuweze pia kushirikishana mambo mengine ya kuinuana kiuchumi,” amesema Kwezi.

Amesema mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atapata ng’ombe mwenye thamani ya Sh milioni moja wakati mshindi wa pili atapata mbuzi na mpira na timu nane zitakazoingia kwenye hatua ya robo fainali zitapata jezi. Pia kutakuwa na zawadi za mfungaji bora, kipa bora na kikundi bora cha ushangiliaji.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akisalimiana na timu ya mpira wa miguu wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Kipawa Diwani Cup kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Majani ya Chai. Katikati ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimji.

Katika ufunguzi wa mashindano hayo uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Majani ya Chai, timu ya FC Bontown iliibuka mshindi kwa kupata mabao 2 – 1 dhidi Falsafa FC.

Mashindano hayo yatahusisha timu 32 za mpira wa miguu na timu nane za mpira wa pete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles