28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

BONGO FLEVA SOMENI NAMBA ZA DIAMOND

UONGOZI wa kambi ya Wasafi umesema Diamond yuko bize sana na shoo kwa sasa. Kila kukicha Diamond Platinum ni lazima aangalie ratiba ya wapi atakuwepo. Inachosha japo inafurahisha na kutajirisha.

Inachosha kwa sababu kama binadamu inabidi apumzike, ila inafurahisha kwa sababu mbali ya kufanya kitu anachokipenda, ila pia anazidi kuongeza uzito wa akaunti yake. Ni ipi basi raha ya kazi kama hupati pesa? Inafurahisha zaidi ya inavyochosha.

 Hii ni tofauti na wasanii wengi. Wengi waliozoea shoo za Mbagala, Masaki na Kinondoni wanalalamika shoo hakuna. Ndiyo, hawapati shoo kama ilivyo mwanzo. Unategemea mtu aende katika shoo wakati hela ya kula inampiga chenga?

Diamond haathiriki sana na hali hii ya mabadiliko ya uchumi Tanzania. Wakati Bongo kukiwa na hali ya mabadiliko kitu kinachofanya hali ya maisha kubana kwa namna fulani ila Kenya, Marekani na nchi zingine hali iko vema tu.

 Watu wanakula bata kama zamani, wanatumia pesa kama ilivyo kawaida na maisha yanaenda.

 Diamond kufika alipofika si jitihada zake binafsi wala uchawi kama wengi wanavyopenda kujidanganya. Wakati Diamond akiwa studio au Gym akifanya mazoezi, mameneja wake wanakuwa bize kila kona ya nchi na dunia kuangalia namna ya kumpatia shoo na mikataba minono ya matangazo.

Hii ni tofauti na wasanii wengi. Wengi hudhani wanaweza kufanya kila kitu wenyewe ama kwa kushirikiana na mameneja washikaji. Hili ni jipu.

 Katika dunia ya kisasa, msanii ni lazima awe na meneja makini mwenye kujua nini anachofanya. Ni lazima awe na mtu mwenye uwezo wa kumwambia afanye nini na kwa wakati gani.

  Inabidi awe na mtu ambaye ataumiza kichwa usiku na mchana kuangalia namna ya kukuza thamani na hadhi ya msanii wake.

    Katika shoo ya miaka kumi ya ODM, moja ya vyama vikubwa vya kisiasa nchini Kenya iliyofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, Diamond alilipwa takribani milioni mia moja za Kitanzania kwa shoo ya takribani dakika tisini, ikiwa tofauti na wasanii wote wa Kenya na wale wale walioalikwa kutoka Tanzania kwa ajili ya shoo hiyo.

   Hii inaonesha ni kwa namna gani thamani yake iko juu, hii inaonesha ni kwa namna gani watu waliomzunguka walivyo mtengeneza Diamond kuwa bidhaa adimu. Haishangazi hata kidogo.

    Timu ya Diamond ni ya watu makini. Kila mtu aliye katika lebo ya wasafi ana aina tofauti na wasanii wengine. Haya ni matokeo ya kuwa na watu kama wakina Saidi Fela, Babu Tale, Sallam SK na wengineo. Nani ana shaka na uwezo wa watu hawa katika duru la burudani?

    Wasanii wengi wanawaza milioni 5 za kula bata na kubadilishia magari. Hawawazi kesho yao na matokeo yake wanabaki kuwa wa hapa hapa tu. Ona sasa wanahaha baada ya hali ya uchumi kuwa mbaya wakati wakina Diamond na wenzake wanazidi kutengeneza pesa.

   Wasanii wengi wanapenda kujipa majibu mepesi katika maswali magumu. Wao wamekariri ili msanii awike inabidi awe na kiki. Wanasahau kuwa bila muziki mzuri na jitihada makini kiki haziwezi kumpa msanii heshima.

    Nuh Mziwanda alitamba sana na Shilole ila hakutamba katika muziki. Alitamba katika muziki baada ya kutoa wimbo kali yenye hadhi ya kutamba, Jike shupa. Tena hii inatokea akiwa kaachana na Shilole.

   Kwa vipaji vilivyopo Tanzania vikipata uongozi mzuri na makini, wasanii wakiacha kuwa wajuaji, miaka kadhaa ijayo wakina Diamond watakuwa wengi  wakituwakilisha Watanzania huko duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles