NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
MKONGWE wa ngumi za kulipwa nchini, Maneno Osward maarufu Mtambo wa Gongo, amemuomba Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa kuisapoti Peaktime Media kutokana na kujikita katika kuinua vipaji vya mchezo wa masumbwi.
Mtambo wa Gongo ametoa kauli hiyo jana wakati wa mapambano ya nusu fainali ya kumtafuta Champion wa Kitaa Wilaya ya Temeke yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala jijini Dar es Salaam.
“Ombi langu ni kwa Waziri anayehusika na michezo kumsapoti Promota Meja Selemani Semunyu muandaaji wa Champion wa Kitaa kwa sababu amekuwa akiibua vipaji vya ngumi kutoka chini,” amesema mkongwe huyo wa masumbwi.
Katika mapambano hayo miongoni mwa mabondia waliopanda ulingoni alikuwa ni mtoto wa bondia huyo anayejulikana kwa jina Maneno Osward Junior ambaye alifanikiwa kuibuka mshindi kwa kumchapa kwa pointi Halfan Ukala.
Katika pambano kuu lilikuwa na raundi sita kilo 57, Hamad Furahisha amemdunda Maganga Kulwa kwa pointi, huku mkongwe Shaaban Kaoneka akipoteza kwa akichapwa na bondia chipukizi Kennedy Samweli.
Wengine walioibuka kidedea katika mapambano ya raundi nne nne ni Sebastian Deo aliyempiga Enock Enock, Swaibu Ramadhani amemchapa Anthony Mnyandwa.
Naye Peter Tosh akimtwanga Salum Zahoro.Omary Salum aliibuka mshidi dhidi ya Bakari Katogo.