31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bonde la mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imesema imepanga kulibadili eneo la bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali ambapo tayari usanifu wa mradi huo umekamilika.

Hayo yameelezwa jana bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema kuwa hata hivyo, ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Katika swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kinondoni Mhe. Tarimba Abbas alitaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025.

Katika maelezo ya awali Mhe. Chande alisema Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inatekeleza mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) kwa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.

Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID), inatekeleza program ya “Tanzania Urban Resilience Programme (TURP)” ambayo imelenga kuzisaidia Halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuanzia, programu itaanza kutatua changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Msimbazi.

“Tayari DFID imeshatenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 20 kwa ajili ya Bonde la Mto Msimbazi. Pia Benki ya Dunia, kupitia mradi wa DMDP, imekubali mkopo wa nyongeza wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi,” alisema Naibu waziri Chande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles