24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Bomoa bomoa kuanza leo nchi nzima

Ardhi - 6CHRISTINA GAULUHANGA NA IDDY ABDALLAH, DAR ES SALAAM

SERIKALI imetangaza kampeni maalumu ya kubomoa nyumba, vibanda vya biashara pamoja na kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya wazi kinyume cha sheria.

Bomoa bomoa hiyo inatarajiwa kuanza leo katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, huku mkakati huo ukitarajiwa kuendelea nchini kote kuanzia sasa.

Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari na Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Moses Kusiluka.

Alisema shughuli hiyo ya ubomoaji itafanyika nchi nzima ambapo kwa kuanzia leo wataanza na Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam.

“Hakuna asiyefahamu kuhusu umiliki au ujenzi wa eneo lake, hivyo taarifa za shughuli hii tunayoanza leo wote wanaifahamu, na tutapita nyumba moja ama nyingine. Hatutakuwa na mzaha katika hili,” alisema Kusiluka.

Alisema Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni watasimamia shughuli hiyo ya kubomoa nyumba na vibanda kwa kuwaondoa wale wote waliojenga kwenye maeneo ya wazi.

Kusiluka alisema na hata waliojenga bila kibali na kutofautiana na michoro ya mipango miji nao nyumba zao na maeneo ya biashara yatabomolewa.

“Kazi hii ya ubomoaji itafanywa na Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na watasimamia sera za ardhi na taratibu za uendelezaji kuhakikisha zinafuatwa na kila mmiliki wa ardhi,” alisema Kusiluka.

Alitaja maeneo ambayo yamekiuka ujenzi kusudiwa na yatahusika na ubomoaji huo kuwa ni pamoja na Mbezi, Tegeta, Bunju, Mwenge na Kinondoni-Biafra.

“Kazi hii itafanyika kwa siku tatu na baada ya hapo tutahamia wilaya nyingine kwakuwa ni zoezi endelevu kwa nchi nzima,” alisema Kusiluka.

Alisema jambo la kusikitisha, maeneo yaliyotengwa mjini kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja na maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyinginezo za umma, yamevamiwa na kutumiwa na waendelezaji binafsi, hivyo kuukosesha umma manufaa kusudiwa.

“Serikali itahakikisha maeneo yote ya mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yanalindwa ili yasivamiwe.

“Katika hili Serikali za mitaa zitawajibika kuhakikisha zinashirikiana na wizara husika katika usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao,” alisema Kusiluka.

Wakati huohuo, wizara hiyo imesema mchakato wa kuliendeleza eneo la Coco Beach upo katika ngazi ya manispaa ambapo michoro mbalimbali inaangaliwa.

Kusiluka alisema Serikali itahakikisha inatunza fukwe ili zibaki ziwe za umma na zenye kuwanufaisha.

“Serikali inatunza fukwe kuhakikisha zinalindwa na kuwa matumizi ya umma. Coco Beach inaendelea kuangaliwa kwa undani namna ya uboreshaji wake, na kwa sasa mchakato huo upo ngazi ya manispaa,” alisema.

Machi 21, mwaka 2011, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliomba akingiwe kifua na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ili kuweza kurejesha viwanja vilivyoporwa.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo wizara yake ilikuwa inashughulikia wakati huo, ni pamoja na kurejesha viwanja vilivyoporwa, vikiwamo vile vya wazi.

Ilielezwa kuwa asilimia 90 ya ardhi nchini haijapimwa na kumilikishwa, hali ambayo imekuwa ikizua migogoro kila kukicha.

Kutokana na hali hiyo, wizara hiyo iliwahi kutangaza mpango kabambe wa kujenga miji mipya katika maeneo ya Kawe, Buguruni na Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa watu.

Maeneo ambayo yalitangazwa kujengwa miji hiyo, ni Buguruni, ambako watatumia wakazi wa Wilaya ya Ilala; Kawe (wakazi wa Wilaya ya Kinondoni); na Kigamboni (wakazi wa Wilaya ya Temeke).

Licha ya mikakati hiyo ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, bado wizara hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kwa baadhi ya wananchi kujitwalia na kumiliki ardhi kinyume cha sheria.

Pamoja na kutangazwa kwa oparesheni kadhaa kubwa za kubomoa nyumba na majengo ya watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi au yasiyoruhusiwa, lakini suala hilo limekuwa likikumbana na vikwazo kadhaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles