23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

BOMBARDIER YAZUA KIZAZAA MWANZA

Na  BENJAMIN MASESE-MWANZA

NDEGE  ya  Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q Dash 400 namba   5H TCB, juzi ilizua taharuki kwa abiria baada ya kushindwa kuruka katika  uwanja  ndege wa Mwanza, imefamika.

Kitendo hicho kilisababisha abiria kupiga kelele wakitaka  kushushwa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 1.00 jioni wakati ndege hiyo ikijiandaa kuruka   kwenda Dar es Salaam ikiwa na abiria zaidi ya 30.

 Mmoja wa abiria wa ndege hiyo, Juma Robi mkazi wa Musoma alisema ndege ilishindwa kuondoka  huku   ikitoa mlio tofauti ilivyo kawaida yake.

Hilo ni tukio la pili kutokea kwa ndege  za shirika hilo baada ya mwezi uliopita kuruka na baada ya dakika mbili  ikarejea na kutua  tena katika uwanja huo.

Ilidaiwa  kuwa ilitokana na kutofungwa   vizuri mlango wa mizigo huku taarifa nyingine zikidai ilikuwa ni hitilafu ya  kawaida.

Abiria waelezea 

Mwandishi aliyefika  katika uwanja huo alikuta abiria  wakiwa wameshushwa huku kila mmoja akiwa anampigia ndugu yake simu kujumlisha hali ilivyokuwa.

Nao uongozi wa uwanja huo  ulilazimika kuwachukua abiria  wote  na kuwapeleka katika hoteli kwa ajili ya chakula.

Robi akizungumza na MTANZANIA  akiwa katika Hoteli ya Kigdom,  alisema alifika  uwanjani  saa 11 jioni kwa mujibu wa tiketi yake na akapanda kwenye ndege hiyo saa 1.00.

Alisema wakati wanajiandaa kuondoka    ndege   ilitoa sauti   ambayo si ya kawaida hali iliyosababisha abiria waangaliane kwa mshangao na hofu.

“Ilipojaribu kuisogea  mbele ilishindikana maana sauti ilikuwa kubwa ya muungurumo,  yaani kila mmoja alikuwa na hofu na wengine wakaanza kupiga kelele kutaka kushushwa, hali ilivyozidi tukawa hatuelewani ndipo walipoamua kutushusha na mizingo yetu.

“Walitupandisha  kwenye gari lao na kutuleta mitaani kula, tumeanzia katika  Hoteli ya  Starmax ya Kirumba lakini hatukupata chakula.

“Tumehamishiwa hapa  Kigdom  na  kupata chakula, wametueleza saa 6.00 tutaondoka kwenda Dar es Salaam lakini hii ni hasara maana wengine tulikuwa tumekodi nyumba, gari za kutupokea sasa sijui itakuaje.

Kauli ya ATCL

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL,  Emmanuel Koroso, alikiri ndege hiyo kupata hitilafu wakati ikijiandaa kuruka   kwenda Dar es Salaam.

“Ni kweli  kuna tukio la  moja ya ndege zetu kupata hitilafu wakati ikijiandaa kuruka hapa ikiwa na abiria,    kilichotokea katika ndege yetu ni hitilafu ya mawasiliano baada ya kutoa  indicator (viashiria) ya mfumo wa mafuta ambayo  kwa namna moja au nyingine si sahihi.

“Baada ya hapo kama unavyojua ATCL ina ndege nyingine…ilikuja nyingine na kuwachukua usiku huo huo na kuwapeleka Dar  es Salaam, walifika salama muda wa saa 7.00  usiku.

“Tunavyozungumza hivi tayari mafundi wamefanya utafiti wa tatizo hilo lililojitokeza na wamerusha ndege hiyo kwa majaribio hapa uwanjani wakiwa na rubani.

“Wamejiridhisha ni salama, tulichoamua ni kwmaba ndege hii irudi Dar es Salaam bila abiria   iweze kupangiwa ratiba nyingine ya safari,” alisema.

Uongozi wa TAA

  Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Tanzania (TAA), Mkoa wa Mwanza, David Matovolwa, alisema ndege hiyo ilikuwa katika ratiba yake ya kila siku na iliwachukua abiria hao kama kawaida lakini kabla ya kuruka ikatokea kuwapo na hitilafu.

 Mazoezi ya ndege hiyo

Baada ya ndege hiyo kushindwa kuruka juzi usiku, iliwekwa pembeni ya uwanja ambapo jana asubuhi ilikuwa ikifanyiwa marekebisho  huku ikiwasha mara kwa mara na baadaye kuijaribisha kuruka na kutua.

Ilipofika saa 3.50 ilijaribiwa kurushwa angani ambako ilizunguka na kurejea tena saa 4:01 asubuhi. Hata hivyo ilipofika saa 4.40  iliruka kwenda Dar es Salaam ikiwa na rubani na wahandisi waliokuwa wakiifanyia uchunguzi wa tatizo lake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles