Bodi kumfutia mkataba mkandarasi REA

0
860

Veronica Simba, Mtwara

Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeweka kusudio la kufuta mkataba mmojawapo wa mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mtwara na sehemu ya Mkoa wa Tanga.

Wakala huyo ambaye ni muunganiko wa kampuni za Radi Services Ltd, Njarita Contractors Ltd & Aguila Contractors Ltd.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi hiyo, Mhandisi Styden Rwebangila, amesema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Rwebangila alikuwa akitoa majumuisho ya ziara ambayo yeyé na wajumbe wa Kamati husika walifanya mkoani Mtwara kwa siku mbili, wakiiwakilisha bodi nzima, ambayo ililenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

“Kamati imeamua kuweka kusudio hilo kutokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni kusuasua kwa utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo mkandarasi husika amepewa kimkataba kuyafanyia kazi huku akiwa haoneshi dhamira ya kufanya mabadiliko chanya.

“Kamati iliambatana na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo ya ukandarasi ambapo walikagua sehemu kadhaa ambako mradi unatekelezwa lakini tumeshangaa leo hajaonekana katika kikao hiki muhimu kilicholenga kujadiliana namna ya kumsaidia ili akamilishe kazi yake vizuri,” amesema.

Alisema, kitendo cha Mkandarasi kutoonekana kwenye kikao, kinadhihirisha kuwa hatoi kipaumbele kwa mradi huo muhimu na wa kimkakati kwa serikali.

Akieleza zaidi kuhusu kusudio la kufuta mkataba, Rwebangila alieleza kuwa, Kamati yake imetoa maagizo kwa REA, kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Huduma za Ufundi, Mhandisi Jones Olotu, kufanya tathmini kati ya Mtwara na sehemu ya Tanga, ambako mkandarasi husika anatekeleza mradi, wapi panasuasua zaidi ili mkataba wake ufutwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here